ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 22, 2018

WATOTO WA WAFUGAJI WAGUSWA NA SOKO LA KIMKAKATI LA MIFUGO LONGIDO

 Baadhi ya watoto wa wafugaji, kijiji cha Eworendeke, kata ya Kimokouwa, Wilayani Longido wakipata maziwa kwa ajili ya matumizi yao kwa kukamua bure mbuzi waliofikishwa muda wa jioni katika Soko la kimkakati la mifugo Longido kuuzwa, Soko hilo limejengwa na Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).
 Mmoja wa watoto wa wafugaji, kijiji cha Eworendeke, kata ya Kimokouwa, Wilayani Longido akipata maziwa kwa ajili ya matumizi yake kwa kukamua bure mbuzi waliofikishwa muda wa jioni katika Soko la kimkakati la mifugo Longido kuuzwa, Soko hilo, limejengwa na Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).


Katika kijiji cha EWORENDEKE, kata ya KIMOKOUWA, Wilayani LONGIDO mkoani ARUSHA, kijiji hicho kipo takriban kilomita 4 kutoka Namanga, mpaka wa Tanzania na Kenya.

Hapo kuna Soko la Kimkakati la mifugo Longido, linalohusika na uuzaji wa mifugo kutoka mikoa takribani 7 ya hapa nchini Tanzania. Wafugaji huuza mifugo hiyo hapa nchini na nchi za jirani, soko hilo ambalo limejengwa na Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), limekuwa ni neema kwa watoto wa kaya zinazozunguka soko hilo.

Watoto wa wafugaji wa jamii ya kimaasai ambao ndiyo wanufaika wa soko hilo wameguswa na uwepo wa soko hilo kwa kupata maziwa ya mbuzi bure. Watoto hao hukamua maziwa hayo kutoka kwa mbuzi ambao hufikishwa sokoni hapo muda wa jioni na kusubiri kuuzwa usiku ambapo mnada wa mifugo kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hufanyika sokoni hapo.

Mratibu wa Kitaifa wa Program ya MIVARF,Walter Swai, amebainisha kuwa tangu Program hiyo ianzishwe kutekelezwa rasmi mwaka 2011, katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar imekuwa ikichochea faida nyingi, zaidi ya malengo mahususi yaliyokusudiwa na Program ambayo, ni kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania ya kuongeza kipato kwa wananchi pamoja na uhakika wa chakula kwa kaya zenye kipato cha chini hususan maeneo ya vijijini.

“’Kuna maeneo tumejenga barabara za vijijini hasa kutoka maeneo ya uzalishaji, lakini tumekuta katika maeneo hayo ardhi imepanda thamani, hivyo hivyo katika soko la Kimkakati Longido tayari tunaona hata akina mama wameanza biashara ya mama lishe lakini na watoto wao wanapata maziwa ya mbuzi bure kwaaajili ya lishe yao” alisema Swai.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mifugo wilayani Longido, Saruni Laizer amesema kuwa hayo ni mojawapo ya manufaa ya soko hilo lililojengwa na Program ya MIVARF, kwani watoto wao wanakuwa na afya bora kwa kunywa maziwa ya mbuzi ambayo huyapata bure na kisha huyachemsha na kuyatumia kwa matumizi ya nyumbani.

Soko hilo litawanufaisha wananchi wapatao 14,2000 wa wilayani Longido ambapo asilimia 95 ni wafugaji na wanaojishughulisha na biashara za mifugo, pamoja na kuwa wafugaji ni walengwa wa Program hiyo , walengwa wengine ni wakulima wadogo, wavuvi na wafanyakazi wa kazi za mikono (artisans), Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo walioko vijijini.

MIVARF; ni Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko na Huduma za Kifedha Vijijini iliyobuniwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo yaani (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Dhumuni la kuanzishwa kwa Programu ya MIVARF ni; Kuboresha miundo mbinu ya masoko, barabara za vijijini, maghala na masoko, Kuwawezesha wananchi waishio vijijini na kuongeza thamani mazao ya kilimo.

No comments: