ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 24, 2018

Watu 27 wakamatwa kwa madai ya kuchoma kituo cha polisi

Watu 27 wanashikiliwa mkoani hapa kwa tuhuma za kuchoma moto kituo kidogo cha Polisi cha Mwandoya katika Wilaya ya Meatu na kuteketeza samani na mali zote zilizokuwa zikitumiwa na jeshi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mshongi alisema tukio hilo lilitokea Machi 22 mwaka huu, saa 2:45 usiku.

Kamanda Mshongi alisema wahalifu hao walivamia kituo hicho wakiwa na matofali, mawe na silaha za jadi na kuharibu samani zote na kisha kuchoma moto nyaraka mbalimbali za kituo hicho.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, mali nyingine zilizoharibiwa kwa kuchomwa moto na majambazi hayo ni milango sita, meza tatu, viti vitano vya mbao na vingine 16 vya plastiki na kabati la kutunzia mafaili ya kituo.

Vingine vilivyoharibiwa ni mashine ya kupimia kilevi na pikipiki yenye namba DFPA 1171 mali ya polisi.

“Baada ya kutekeleza uhalifu huo, kundi hilo lilikwenda kwenye makazi na vibanda vya biashara vya askari polisi wanaofanya kazi kituoni hapo pamoja na duka la kuuza dawa za binadamu la Magreth Isapi wakafanya uhalifu pia kwa kuchoma moto mali hizo,” alisema


Aliongeza, “Walikwenda pia nyumbani kwa askari ambaye anaishi uraiani kitongoji cha Muungano na walichoma moto nyumba aliyokuwa akiishi na kuunguza vitu vyake vyote pamoja na vyeti vya taaluma ikiwamo vyeti vya sekondari, udereva na walichoma pia cheti cha ndoa na kompyuta ya askari huyo.”

Alisema kuwa watuhumiwa hao walichoma maduka yanayomilikiwa na askari kisha kuiba kompyuta, kamera na vifaa vingine vinavyotumika kusafishia picha.

Kamanda Mshongi alisema kundi hilo pia lilikwenda kwenye duka la dawa la Magreth Isapi na kuvunja mlango na kuiba dawa mbalimbali za binadamu ambazo thamani yake haijajulikana na baadaye kulichoma moto.

‘’Wakati kundi hilo likiendelea na uharibifu kuelekea maeneo mengine, polisi Meatu wakiongozwa na OCD F. Bongole akisaidiwa na Kaimu OC/CID Nassib waliwahi eneo la tukio na kuwadhibiti wahalifu hao, na hadi sasa thamani ya vitu vilivyoharibiwa na kuibiwa bado haijafahamika’’ alisema Kamanda Mshongi.

No comments: