Wednesday, April 25, 2018

KIVULINI YAKUTANA NA WANA MABADILIKO NA WADAU WA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


Shirika la Kivulini limeendesha vikao vya tathmini na mipango mikakati ya utekelezaji wa mradi wa Usawa wa Kijinsia kiuchumi kwa wanawake na vijana unaotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini na Kishapu mkoani Shinyanga.

Vikao hivyo vilivyofanyika Aprili 23, 2018 na Aprili 24,2018 katika ukumbi wa Katemi Hotel Mjini Shinyanga vimewaleta pamoja wadau wakuu katika kupinga ukatili wa kijinsia na wana mabadiliko wa kujitolea ngazi ya jamii kutoka vijiji vya Nyida, Nsalala, Welezo, Nduguti na Nyida kwa wilaya ya Shinyanga vijijini.
Akizungumza wakati wa vikao hivyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Deus Masili Muhoja alisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwezi Septemba mwaka 2017 kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika jamii kwani sasa wananchi wana elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.
“Suala la ukatili haliwezi kuisha leo,tunapaswa kushirikiana wadau wote,tutoe taarifa za matukio ya ukatili na tuendelee kutoa elimu kwani jamii ikipata elimu matukio haya yatapungua”,aliongeza Muhoja.
Aidha alisema bado halmashauri ya wilaya ya Shinyanga inakabiliwa na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake ambapo wanawake wamekuwa wakikatwa mapanga hivyo kuomba wadau kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ukatili huo.
Awali akizungumza, Afisa Mwandamizi Msaidizi wa mradi huo,Vaileth Elisa wakiwa ukumbini alisema lengo la vikao hivyo ni kufanya tathmini ya shughuli na matokeo ya mradi huo mwaka 2017 na kupanga mikakati ya shughuli za mradi huo kwa mwaka 2018 ambao unatekelezwa na shirika la Kivulini kwa kushirikiana na Shirika la OXFAM.
Alisema katika kutekeleza mradi huo mwaka 2017 wamefanikiwa kuwafikia watu 14,988 kati yao wanawake ni 7652 na wanaume 7336 ambapo walitoa elimu ya mafunzo ya usawa wa kijinsia,sera na sheria zinazohusu usawa wa kijinsia kwa njia ya mafunzo,midahalo jamii na sinema.
Nao washiriki wa vikao hivyo walisema kutokana na jitihada zinazofanywa na shirika la Kivulini walisema kumekuwepo na ongezeko la uelewa kwa jamii na makundi maalum kuhusiana na sheria,sera na mifumo iliyopo inayohusiana na ukatili wa kijinsia na matumizi ya mifumo inayowasaidia wahanga wa ukatili.
Naye Afisa kutoka Jeshi la Polisi wilaya ya Shinyanga,Joseph Christopher alisema hivi sasa jamii ina mwitikio mkubwa kwa sababu wengi wamekuwa wakifika katika dawati la jinsia na watoto kutoa taarifa za matukio ya ukatili.
“Jamii imebadilika,mfano mwaka 2017 tulipokea matukio 52 ya ukatili wa kijinsia lakini mwaka huu tumepokea matukio 82,hii ni hatua kubwa,tunachosisitiza sasa ni wahanga wa matukio ya ubakaji wawe wanatoa taarifa ndani ya saa 72 (siku tatu) na kuepuka kumaliza kesi kifamilia”,alieleza.
Kwa upande wake,Afisa Mtendaji wa kata ya Nyida Daudi Lazaro alisema jamii inaendelea kubadilika na kuachana na mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke na wamekuwa wakitoa elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia katika vikao na mikutano mbalimbali.
Na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Deus Masili Muhoja akizungumza wakati wa kikao cha tathmini na mipango mikakati ya utekelezaji wa mradi wa Usawa wa Kijinsia kiuchumi kwa wanawake na vijana uliohudhuriwa na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia wakiwemo viongozi wa serikali za vijiji,kata,maafisa maendeleo,dawati la jinsia na watoto katika ukumbi wa Katemi Hotel mjini Shinyanga Aprili 23,2018 
Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Deus Masili Muhoja akizungumza wakati wa kikao cha tathmini na mipango mikakati ya utekelezaji wa mradi wa Usawa wa Kijinsia kiuchumi kwa wanawake na vijana.
Wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia wakiwa ukumbini 
Afisa Mwandamizi Msaidizi wa mradi huo,Vaileth Elisa akielezea lengo la kufanya lengo la vikao hivyo ni kufanya tathmini ya shughuli na matokeo ya mradi huo mwaka 2017 na kupanga mikakati ya shughuli za mradi huo kwa mwaka 2018. 
Marzia Nzota kutoka shirika la RUDI akizungumza wakati wa kikao hicho. Shirika hilo linashirikiana na shirika la Kivulini kutekeleza mradi wa Usawa wa Kijinsia kiuchumi kwa wanawake na vijana 
Afisa Mwandamizi Msaidizi wa mradi huo,Vaileth Elisa akiangalia kazi inayofanywa na kikundi
Afisa kutoka Jeshi la Polisi wilaya ya Shinyanga,Joseph Christopher akiwasilisha kazi ya kundi lake kuhusu mwamko wa jamii kutoa taarifa juu ya matukio ya kikatili dhidi ya watoto na wanawake
Mwenyekiti wa kijiji cha Welezo Janeth Mabula akichangia hoja wakati wa kikao hicho
Kikao kinaendelea..
Mdau akiandika dondoo muhimu
Wadau wakiwa ukumbini
Aprili 24,2018 ; Afisa Mwandamizi Msaidizi wa mradi huo,Vaileth Elisa akizungumza na wana mabadiliko wa kujitolea ngazi ya jamii kutoka vijiji vya Nyida, Nsalala, Welezo, Nduguti na Nyida kwa wilaya ya Shinyanga vijijini.
Afisa Mwandamizi Msaidizi wa mradi huo,Vaileth Elisa akizungumza na wana mabadiliko.
Wana mabadiliko wa kujitolea ngazi ya jamii wakiwa ukumbini
Wana mabadiliko wa kujitolea ngazi ya jamii wakiwa ukumbini
Wana mabadiliko wa kujitolea ngazi ya jamii wakifanya kazi ya kikundi
Afisa Mwandamizi Msaidizi wa mradi huo,Vaileth Elisa akielezea jambo wakati wa kazi za vikundi
Mwana mabadiliko Lucia James  kutoka kijiji cha Nduguti akiwasilisha kazi ya kundi lake
Wana Mabadiliko wakiwa ukumbini
Mwana mabadiliko Aron Marco kutoka kijiji cha Butini akiwasilisha kazi ya kundi lake
Picha ya pamoja wana mabadiliko
Picha ya pamoja wana mabadiliko.


Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments: