ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 17, 2018

MAONYESHO VIVUTIO VYA UTALII YAAANZA BEIJING NCHINI CHINA

Afisa  Habari - Utalii (Bodi ya Utalii Tanzania) Bi.Irene F.Mville (Kushoto) akizungumza na baadhi ya Wateja waliojitokeza kwa nia ya Utayari wa Kupata taarifa juu ya Vivutio vya Utalii nchini  Tanzania kwenye maonyesho ya vivutio vya utalii yaliyofanyika jijini Beijing nchini China.
 Afisa Mipango kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar Bw.Hassan Ameir Vuai (Katikati) akitoa huduma kwa moja ya wateja waliotembelea banda la Tanzania kwenye maonyesho ya vivutio vya utalii yaliyofanyika jijini Beijing nchini China.
 Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania Bw. Eugen S. Malley (kulia) akifafanua jambo mara baada ya kutembelewa na wadau wa Utalii katika banda la Tanzania kwenye maonyesho ya vivutio vya utalii yaliyofanyika jijini Beijing nchini China.
Mkurugenzi wa Hango Trade Company  ambaye pia ni Mtanzania anayesoma nchini China  Bi.Angelina Makoye akitafsiri lugha ya kingereza kwenda kichina wakati akielezea fursa za  Utalii  zilizopo nchini Tanzania kwenye maonyesho ya vivutio vya utalii yaliyofanyika jijini Beijing nchini China.
Umati mkubwa ukiwa umefurika katika banda la Tanzania kwenye maonyesho ya vivutio vya utalii yaliyofanyika jijini Beijing nchini China.
Moja ya Kampuni inayojishughulisha na Shughuli za Utalii hapa nchini, wakimhudumia mteja aliyetembelea Kampuni hiyo

Na Ripota Wetu, China
MAONESHO ya vivutio vya utalii (China Outboard Travel & Tourism Market – COTTM) kwa mwaka 2018 yameanza leo jijini Beijing China, na kuhusisha  mataifa zaidi ya 150. Tanzania imewakilishwa na Bodi ya Utalii kwa kushirikiana na  Kamisheni ya Utalii Zanzibar wakiambatana na baadhi ya kampuni ya kitalii hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya  Bodi ya Utalii nchini, Irene  Mville ambaye pia ni Ofisa Utalii habari ameeleza lengo la maonesho hayo ni kutangaza utalii, ambapo Tanzania  inatumia  fursa hiyo kutangaza vivutio vinavyopatikana nchini.  Ameitaja China kama  soko jipya wanalopatikana watalii.

"Kwa kadri uchumi wa China unavyozidi kukua ndivyo idadi ya watalii kutoka China itazidi kuongezeka.  Mwaka 2016 Wachina milioni 120 walikwenda nje ya nchi kutalii na kutumia dola za Kimarekani Bilioni 1.2.

"Hivi sasa nyumbani Tanzania tunaendelea kupokea watalii kutoka China. Idadi ya watalii waliokwenda mwaka 2016 ni 37,000. Ukilinganisha na milioni 120 hiyo idadi ni ndogo sana,"amesema Irene

Aidha,amepongeza ushirikiano mkubwa na hatua kadhaa ambazo zimekuwa zikichukuliwa na ubalozi wa Tanzania nchini China ikiwa ni pamoja na uwepo wa maonesho na makongamano ya kitalii  na kutumia mitandao ya kijamii ya China  kutangaza vivutio vya utalii nchi yetu.

"Natambua jitihada za Shirikisho la  wanafunzi watanzania nchini China,  ambao pamoja na shughuli zao za kimasomo,wamekuwa wakitumia sehemu ya muda wao kuendelea  kutangaza vyema vivutio vya utalii katika taifa la China,"ameongeza.

Irene  ameielezea China kama taifa linalofanya vizuri katika sekta ya utalii.

Kwa upande wa Ofisa Mipango kutoka Kamisheni ya Utalii ZanzibarHassan Ameir Vuai , amesema matarijio yaliyopo ni pamoja na ongezeko la watalii kutoka nchini China pamoja na ushirikiano wa baina ya wafanyabiashara wa pande zote, hatua itakayochochea ongezeko hilo.

Baadhi ya kampuni kutoka Tanzania yaliyohudhuria maonesho hayo ni pamoja na  Puffback Safaris,Chabo Africa Safaris,Zagas Explorer,Dazzling  Sunshine Tourism LTD, GBT Tanzania Adventures LTD, Kilema Kyaro Hotel & Lodge na Big five Voyage.

Maonyesho hayo ambayo ufanyika kila mwaka jijini hapa yatamalizika tarehe Aprili 18 mwaka huu.

No comments: