JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
nchini
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt.
Akinwumi Ayodeji Adesina atafanya ziara ya siku nne (4) nchini kuanzia tarehe
25 hadi 28 Aprili, 2018 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Lengo la ziara ya Dkt. Adesina nchini ni kuimarisha
ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi
kikubwa maendeleo ya miradi ya miundombinu nchini.
Akiwa nchini, Mhe. Dkt. Adesina ataonana kwa
mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuzindua Barabara kutoka
Dodoma kwenda Babati hafla itakayofanyika katika eneo la Mradi wa Barabara wa Mayamaya-Mela-Bonga
Wilayani Kondoa.
Aidha, Dkt. Adesina atatembelea Mtambo wa
Kusafirisha Umeme wa Iringa kwenda Shinyanga pamoja na Kituo Kidogo cha Umeme
cha Zuzu cha Mkoani Dodoma.
Dkt. Adesina ambaye ameambatana na Makamu wa Rais
wa Benki hiyo anatarajiwa kushiriki Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa
Tanzania yatakayofanyika Mkoani Dodoma tarehe 26 Aprili, 2018.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika
zinazoongoza kwa kupokea misaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia
Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF). Aidha, tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa
nchini mwaka 1971, Tanzania imenufaika kwa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani
bilioni 3.5 huku miradi ya maendeleo ya miundombinu ikipewa kipaumbele.
Aidha, hadi kufikia mwezi Novemba 2017 Benki ya
Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitekeleza miradi 25 yenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 1.9. Kati ya miradi hiyo, 22 ni ya Sekta ya Umma yenye thamani
ya Dola za Marekani bilioni 1.8 huku miradi mitatu (3) ikiwa chini ya Sekta
Binafsi kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 187.0.
Kati ya miradi yote, miradi ya maendeleo ya miundombinu
inachukua asilimia 73 ambapo kati yake miradi ya Barabara ni asilimia 51, Maji
na Usafi wa Mazingira asilimia 12 na Nishati asilimia 10. Asilimia 27
zilizosalia zinasaidia miradi ya sekta binafsi hususan katika kilimo na ustawi
wa jamii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Aprili, 2018
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment