Advertisements

Saturday, April 14, 2018

Tundu Lisuu Aiaga TLS

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu anayemaliza muda wake amewaaga wanachama wa chama hicho huku Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali akieleza kuwa wanafanya kila linalowezekana kukomesha rushwa kwenye mfumo wa sheria.

Jaji Wambali akifungua mkutano mkuu wa TLS jana, alisema rushwa inawanyima haki wananchi. 

Aliwataka wanasheria kujitathmini kama malengo ya kuanzishwa taasisi hiyo yanaakisi shughuli zao sasa kulinganisha na idadi kubwa iliyopo ya wanasheria.

Alisema katika kuharakisha huduma za kisheria, mfumo wa Mahakama umeboresha utendaji kazi kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa haraka.

Lissu akiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu, aliwaandikia wanachama wenzake barua ya kuwaaga akisema; “Jioni ya Machi 18 mwaka jana, nilisimama mbele yenu na kutoa hotuba yangu nikiwa rais mpya. Juni 30, 2017 nilizungumza nanyi tena Dar es Salaam katika mkutano wa dharura wa TLS, lakini leo nazungumza nikiwa katika kitanda cha Hospitali ya Ubelgiji nikiuguza majeraha kama mnavyojua.” 

Katika salamu hizo zenye kurasa 10, Lissu ameelezea tukio la Septemba 7 mwaka jana, aliposhambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi zaidi ya 38 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma kisha kusafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi kabla ya kwenda Ubelgiji.

“Mlinipa nafasi ya kuwahudumia kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini kipindi hicho kilikatishwa miezi saba,” alisema Lissu huku akielezea kwa ufupi mafanikio aliyoyafanya kwa muda huo.

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) amezungumzia masuala mbalimbali huku akiwataka wanasheria hao kupigania utawala wa sheria kwani bila kufanya hivyo hali itakuwa mbaya na hakuna atakayekuwa salama.

No comments: