Maandalizi kwa
ajili ya uzinduzi wa michezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (Sirro CUP
Kibiti 2018) hatua ya 16 bora yamekamilika kwa asilimia tisini na yanatarajiwa
kuzinduliwa siku ya Jumatatu na IGP Simon Sirro katika uwanja wa Samora
wilayani Kibiti.
Akizungumza wilayani Kibiti baada ya kukagua maandalizi hayo, Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Barnabas Mwakalukwa amesema lengo
la Michezo hiyo ni kuwaweka pamoja wakazi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na
Rufiji baada ya matatizo yaliyowakumba kumalizika.
« Michezo hii ni fursa nyingine ya kuwakutanisha wakazi wa Wilaya hizi
na kuihakikishia dunia kuwa sasa maeneo haya ni salama na Tanzania ni salama
baada ya wahalifu waliosumbua hapo awali kudhibitiwa » Alisema Mwakaluka.
Aidha amewaomba wakazi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia
burudani mbalimbali pamoja na maneno ya viongozi mbalimbali yatakayotolewa
katika ufunguzi wa michezo hiyo.
Kwa
upande wake Mratibu wa Kombe hilo, Koplo Ramadhan Tamimu amesema michezo hiyo
itakapofikia tamati bingwa atajinyakulia kombe na fedha taslimu Milioni moja
huku yakichagizwa na kauli mbiu ya “Kibiti
Salama, Jamii Salama”
Naye Katibu wa Chama
cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kibiti Rashid Mkinga amesema wamejiandaa vyema na anauhakika wa kombe hilo kubaki
wilayani Kibiti kwa kuwa pamoja na kuwa na timu bora lakini pia wanatarajia
kupata mashabiki wengi.
Ufunguzi
huo utapambwa na burudani mbalimbali zikiongozwa na Bendi ya dansi ya Jeshi la Polisi, Msanii wa nyimbo za asili
Ndolela, Man Prince na vikundi mbalimbali kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na
Rufiji.
No comments:
Post a Comment