Advertisements

Monday, May 7, 2018

Wabunge CCM Waibana Serikali kupanda kwa bei ya mafuta ya Kula

Wabunge wa CCM, Juma Nkamia (Chemba) na Hussein Bashe (Nzega Mjini), wameibana Serikali wakitaka ishughulikie kupanda kwa bei ya mafuta na kuondoa kodi ya tende ili kuwapunguzia mzigo wa gharama waislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hayo yamejiri leo Mei 7, 2018 bungeni mjini  Dodoma, wakati Nkamia aliposimama kuomba mwongozo kuhusu  mafuta na Bashe kutaka kuahirishwa kwa shughuli za Bunge kwa dakika 30 ili kujadili suala la kodi ya tende ili iondolewe kama ilivyo kwa nchi jirani.

Nkamia alikuwa wa kwanza kuzungumza akisema, kubainisha kuwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuna taarifa za kuadimika kwa mafuta ya kula, “hali hii inasababisha  mafuta kupanda bei kwa haraka, Serikali inatoa kauli gani ili kuwaondolewa wananchi hofu.”

Kwa upande wake Bashe akitumia kanuni ya 69 ya kuahirisha shughuli za Bunge, amesema, “mwezi wa Ramadhani unakaribia na kama alivyosema Nkamia, bei ya mafuta imepanda, sukari imepanda, lakini nchi zinazotuzunguka zimefuta kodi za tende.”

Akijibu mwongozo huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema tatizo lililojitokeza ni suala la kodi kwani kwa sasa Taifa lina hifadhi ya mafuta ghafi tani 40,000 na meli zilizopo nje zina tani 50,000.


“Jumla zilizoko nje na ndani  zina tani 90,000. Kinachoweka tatizo ni kodi kwa sheria tulizopitisha Tanzania, tunatoza kodi (meli kutoka nje ya nchi) asilimia 10 kwa mafuta ghafi,” amesema.

“Ila kwa vipimo vinaonyesha si mafuta ghafi ni mafuta masafi hivyo wanataka kutoza asilimia 25 na hapo ndipo kuna tatizo la hadi kufikia leo au kesho tutatoa majibu ya tulipofikia.”

Kuhusu hoja ya tende iliyoulizwa na Bashe, Waziri Mwijage amesema, “ni suala la kwenda kuzungumza na waziri wa fedha, tutalipeleka kuweza kumshawishi ili Bunge na nchi ichume thamani.”

Naye, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amesema suala la mbegu za pamba kutumika kukamulia mafuta zilipatikana mwaka jana zaidi ya laki moja.

“Suala la mafuta yanayotokana na pamba, kwa uhakika hayakutarajia kuwa mengi, sasa Serikali inachokifanya inaagiza kutoka nje, niseme tu suala la mafuta linafahamika na Serikali inalifanyia kazi na haitapanda bei sana kama mbunge (Nkamia) alivyoonyesha wasiwasi,” amesema Tizeba.

No comments: