Advertisements

Monday, June 11, 2018

Balozi Seif afanya ziara kijiji cha Bubujiko

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko alipofika kukagua Maendeleo ya Mtaro waliojenga kwa nguvu zao ili kuepuka athari za mafuriko hasa wakati wa mvua za Masika.
 Mhandisiwa Ujenzi wa Mtaro wa Kijiji cha Bubujiko Bwana Bwana Mohamed Abdullah kutoka Wizara ya Kilimo, Mali Asili, Uvuvi na Mifugo Pemba akimuonyesha Ramani ya Mtaro huo Balozi Seif na Ujumbe wake wakiwa mbele ya Karo inayoingiza maji hayo.
 Balozi Seif akiwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko kwa hatua waliyochukuwa ya ujenzi wa Mtaro utakaonusuru na majanga ya mafuriko ya mavua.
 Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko wakisikiliza Balozi Seif hayupo pichani wakati alipokuwa akizungumza nao kwenye Mtaa wa Kijiji hicho kiliopo pembezoni mwa Mji wa Wete.
 Mkaazi Muathirika nambari moja wa majanga yaliyokuwa yakitokea kwenye Kijiji hicho wakati wa Mvua za Masika Maalim Omar Hamad kwa niaba ya Wananchi wenzake akiishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inazochukuwa za kuwahudumia Wananchi wake.
 Wawakilishi wa Wananchi wa Mikoa Miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba wakitekeleza Ibada ya Sala ya Magharibi  katika Kiwanda cha Makonyo Wawi kabla ya futari ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
 Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Hemed Suyleiman Abdullah akitoa neon la shukrani kwa niaba ya Balozi Seif  baada ya futari ya pamoja iliyowakutanisha Wawakilishi wa Wananchi wa Mikoa Miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba pamoja na Balozi Seif.
Picha na – ompr – znz.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuwapunguzia gharama za ujenzi wa Mtaro wa Maji ya Mvua Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko waliojitolea kuanzisha Mradi huo kwa lengo la kujiepusha na Mafuriko yanayosababishwa na mkusanyiko wa maji mengi yanayoleta maafa wakati wa mvua za Masika.

Kauli hiyo imetolewa na Makamuwa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Wananchi wa Bubujiko mara baada ya ziara fupi ya kukagua hatua za ujenzi wa Mtaro huo uliosimamiwa na Wananchi wenyewe na kuungwa mkono na Uongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na washirika wa maendeleo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema  kitendo cha Wananchi wa Bubujiko kujenga Mtaro huo kimekuja mara baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kutoa kauli ya Serikali ya ujenzi wa Mtaro huo ambacho kinapaswa kupongezwa.

Alisema Serikali Kuu itaangalia namna ya kusaidia hatua iliyobaki ya kukamilika kwa ujenzi wa Mtaro huo uliobakia Mita 65 zinazotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 30,000,000/- ambapo hadi kukamilika kwake unatarajiwa kufikia Milioni 50,000,000/-.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Umoja na Mshikamano waliyouonyesha Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko ndio chanzo cha mafanikio hayo yanayopaswa kuigwa na Wananchi wa Vijiji vyengine hapa Nchini.

“ Nafarajika kuona Mtaa wa Bubujiko kwa sasa utabakia katika Historia ya kuepuka na Mafuriko yaliyokuwa yakileta simanzi na hasara kubwa kwa Wakaazi wake”. Alisema Balozi Seif.

Mapema Msimamizi ambae pia ni Mhandisi wa Ujenzi wa Mtaro huo Bwana Mohamed Abdullah kutoka Wizara ya Kilimo, Mali Asili, Uvuvi na Mifugo Pemba alisema Mtaro huo umekisiwa kuwa na urefu wa Mita  Mia 200 ambapo kwa hatua ya awamu ya kwanza umeshafikisha Mita 165.

Mhandisi Mohamed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mtaro huo uliojengwa kwa kianzio cha Mita Moja na Nusu hadi Mita Nnne unayawezesha Maji ya Mvua kusafiri kwa haraka bila ya athari yoyote huku mchanga na taka taka zinazotembea katika Mtaro huo hutolewa katika mapokeo maalum yaliyotengwa katika Ujenzi huo.

Alisema juhudi za ziada zilizofanywa na Wananchi katika kuondokana na hatari ya mafuriko ya mara kwa mara ya maji ya Mvua zimewezesha Mtaro huo kujengwa ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja na Nusu.

Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Mtaro huo wa Kijiji cha Bubujiko Mkuu wa Wilaya ya Wete Nd. Abeid Juma Ali alisema Utekelezaji wa Mradi huo umefanywa na Wataalamu Wazalendo.

Nd. Abeid alisema uzoefu unaonyesha kwamba Mtaro kama huo ungeamuliwa kujengwa na Wataalamu wa Kigeni ungekadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 200,000,000/-.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Wete alifahamisha kwamba Mvua kubwa za Masika zilizomalizika hivi karibuni hazikuleta athari yoyote kwa Wakaazi wa Kijiji hicho kilichopo pembezoni mwa Mji wa Wete baada ya kuanza kazi kwa Mtaro huo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko Mkaazi Muathirika nambari moja wa majanga yaliyokuwa yakitokea kwenye Kijiji hicho wakati wa Mvua za Masika Maalim Omar Hamad kwa niaba ya Wananchi wenzake wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inazochukuwa za kuwahudumia Wananchi wake.

Maalim Omar alisema jitihada za Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein na Msaidizi wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wamekuwa wakizishuhudia na kuzifuatilia kiasi cha kuleta faraja kwa Wananchi wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema Wananchi wa Bubujiko wameahidi kuendelea kuunga mkono jitihada hizo za Serikali katika kuona ustawi wa Wananchi wa Zanzibar unazidi kuimarika na kukua kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemaliza ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba ambapo pamoja na mambo mengine alipata wasaa wa kufutari pamoja na Wawakilishi wa Wananchi wa Mikoa Miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba.

Futari hiyo iliyohudhuriwa pia na baadhi ya Viongozi wengine wa Serikali na Vyama vya Kisiasa ilifanyika katika Ukumbi wa Makonyo uliopo Wawi Chake Chake Kisiwani Pemba.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Hemed Suleiman Abdullah aliwaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu wazidishe  Ibada hasa katika Kumi hili la Mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ili kupata baraka za Mwenyezi Muungu.

Alisema hayo yatapatikana na kulifanya Taifa liwe na baraka zaidi iwapo Waumini wenyewe wataendeleza Utamaduni wao wa kudumisha Umoja na Mshikamano kama Maamrisho ya Dini yenyewe yanavyoagiza.

Alisema Taifa linahitaji zaidi Mshikamano na upendo miongoni mwa Wananchi wake bila ya kujali itikadi za Kisiasa na Kidini ili faida ya Wanaadamu kuishi ndani ya Ardhi hii iweze kupatikana.

No comments: