Dar es Salaam. Jina la mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji ni miongoni mambo sita makubwa yaliyotikisa Mkutano Mkuu wa Klabu ya Yanga uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam jana.
Mkutano huo ulioanza 5:14 asubuhi, ulifunguliwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
MANJI AZUA GUMZO
Ingawa Manji hakutokea katika mkutano huo, jina lake lilikuwa likitajwa zaidi na wanachama kuliko kiongozi yeyote wa klabu hiyo.
Wakati mmoja wa wanachama Bakili Makere aliyekuwa ‘MC’ alipouliza wajumbe kama Manji ajiuzulu, walipaza sauti wakidai hawako tayari kuona jambo hilo likitokea.
Makere aliuliza wanachama wangapi wanataka Manji aendelee kuwepo madarakani shangwe kubwa iliibuka ukumbini hapo.
Hata hivyo, baada ya uongozi wa Yanga kushindwa kutoa majibu stahiki, ghafla hali ya hewa ndani ya ukumbi ilibadilika na kuanza vurugu za chinichini kabla ya mkutano huo kuahirishwa.
Baada ya Manji kujiweka kando kutokana na hali ya afya, nafasi yake inashikwa na makamu wake Clement Sanga, timu hiyo imekuwa ikipitia wakati mgumu katika ushiriki wa mashindano mbalimbali.
KAMATI YA USAJILI MPYA
Katika kuhakikisha kwamba inakuja na mabadiliko mapya, Bodi ya Wadhamini imeunda kamati mpya ya usajili ambayo inajumuisha baadhi ya vigogo waliowahi kuongoza Yanga.
Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Abbas Talimba, Makamu Mecky Sadick na wajumbe ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Mashauri Lucas, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwan Kikwete, Majid Suleiman na Hussen Ndama.
Kamati hiyo wakati inapitishwa wanachama walionekana kushangilia huku wakisikika wakisema itashusha vifaa vya maana katika klabu hiyo.
MWANACHAMA AIBUA TAFRANI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwanachama aliyefahamika kwa jina moja la Jitu aliyeonekana kupinga mapendekezo ya wanachama, alitolewa kwa nguvu ndani ya ukumbi.
Kabla mkutano haujaanza mwanachama huyo alianza kubishana kwa hoja na wanachama wengine kabla ya kubebwa na kutolewa nje na Polisi.
MKWASA AFUNGUNGUKA
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema klabu hiyo imepitisha mabadiliko na wana imani italeta mabadiliko ya kiutendaji.
“Mpaka hivi sasa bado Yusuph anaendelea kutambulika kama Mwenyekiti wetu, kikubwa ambacho tunakiangalia ndani ya mwezi ni kukamilisha uendeshaji wa timu,” alisema Mkwasa.
WADAU WAFUNGUKA
Aliyekuwa mchezaji wa Yanga zamani, Ally Mayay, alisema hawajakubaliana kujiuzulu kwa Manji kwa mujibu wa katiba.
“Mabadiliko ya katiba yote yalishafanyika lakini kama mlivyoona katika ajenda ya mwisho wanachama hawakuridhia kutokana na katiba kutoruhusu Mwenyekiti kujiuzulu,”alisema Mayay.
Nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo alisema mabadiliko ya klabu kuwa kampuni yalipitishwa, lakini tatizo lilikuwa upande wa Mwenyekiti.
Waziri huyo alisema Serikali inafuatilia kwa karibu mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu unaofanywa na Yanga na amepongeza uongozi wa Yanga kuanza mchakato huo.
Viongozi wa Yanga walianza kuwasili ukumbi saa nne mchana ambapo Kaimu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Clement Sanga alifika saa 4:07 asubuhi akifuatiwa na Dk Mwakyembe aliyewasili saa 4:15
Baada ya kufungua mkutano huo, Dk Mwakyembe alitoa siku 60 kwa klabu hiyo kuhakikisha inajaza nafasi za viongozi waliojiuzulu nyadhifa zao.
"Kubwa zaidi ninachowashauri ni kuhakikisha mnaziba mapengo yaliyowazi sijasema muitishe mkutano wa uchaguzi hapana, wenyewe kwa umoja wenu mkubaliane kuziba nafasi zilizowazi ndani ya siku 60 nadhani zinawatosha.
"Kama Serikali kwa upande wangu nikiwa kama Waziri mwenye dhamana napongeza juhudi za viongozi wa Yanga na wanachama kwasababu mchakato wa mabadiliko unaenda vizuri, mpira unahitaji pesa, hivyo tumelazimika kuruhusu uwekezaji ndani ya klabu," alisema Dk Mwakyembe
Katika mkutano huo, wanachama 1445 walipitisha mabadiliko katika uendeshaji wa klabu.
Imeandikwa na Thomas Ng’itu, Charty James na Khatimu Naheka. MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment