Advertisements

Monday, June 11, 2018

HII NDIO HISTORIA YA MUZIKI WA DISCO TANZANIA

 Image may contain: 12 people, indoor
Na Mwandishi wetu, Washington, DC
Nimeona nikae chini niipitie maandiko ya mhenga moja aliyeandika habari ya DISCO iliyokua na kichwa cha habari "WAHENGA TULITESA SANA ENZI ZETU DISCO LA MCHANA (BOOGIE) NA MA-DJ WAKALI!!!" mwandishi wa habari hiyo amejitahidi sana kuelezea kwa mapana ya ufahamu wake jinsi gani alivyoujua muziki wa Disco wa enzi zile waliwemo maDj wake.

Mimi nimeamua kuweka sawa baadhi ya mambo Dj Kalikali yeye alishapiga muziki YMCA wakishirikiana na Dj Niga Jay na kuna wakati pia walipiga pamoja na Dj John Peter Pantalakisi na muda mwingi John Peter Pantalakis walikua wakishirikiana na Dj Chogy Sly Dico la Born City na kuna kipindi fulani Dj Kalikali alikua Dj wa Disco la RSVP ambalo Mbowe walianzisha tawi la DICO  katika hotel ya New Africa ghorofa ya saba.
Muziki wa Disco unasafari ndefu maDj wengi wa zamani walikua wanamuziki wa bendi na baadae kubadili mwelekeo na kuwa maDj kwa mfano Dj Sweet Francis na Dj Addy Sally chimbuko lao walitokea kwenye bendi na baadae miaka ya 1970 wakahamisha mawazo yao na kuwa maDj wakati huo kukiwa na Disco la Banda Beach, Sea View na madisco mengine Kilimanjaro Hotel Summit

Nataka nikupe historia ya muziki na disco theque.Africana Gogo Disco lilianza mwaka 1971 na aliyeanza kupiga disco hapo ni Bhoka Wilson (Mzimbabwe) wakati ule ikiitwa Southern Rhodesia naye alikuwa cabbaret singer Simba Grill Kilimanjaro hotel. August 1972 Dj Sweet Fransis akawa Dj hapo mpaka Nov.1973 kisha akawa Dj. Judy Kingui (Msouth Africa ambaye alikuwa mkewe Kingui aliyekuwa mwenye The Rifters Band. Judy alikuwa Dj.hapo Gogo Disco mpaka 1975.

Katika historia ya muziki wa disco Tanzania ambayo inabeba Madj wengi wengine wakiwa wametangulia mbele ya haki 
Disco la XTC ambalo maDj hawa wamepitia David , Lawrance , Pailonga, TNT Jackson

Disco la Valentinos/Continental haliwezi kutajwa bila ya watu hawa Ibrahim G ,Camal, Mr A, Salai, Meb, Guru, Sabry Kube

Disco la Rungwe 110 halijakamilika bila ya watu hawa Chogy Sly JP Pantelakis, Roma Pop Juice, Amon Washington, Agib Show, Ibony, Ntimizi, Bhester, Kim and the boyz, John Bure na wengineo

Madisco ya mikoani nayo yana historia hii kama Disco Landau Mbeya na ma dj akina Musa, Dodoma kulikua na NK Disco, Korogwe kulikua na Disco la BS ukija Moshi utamkuta Dj Issa Kibaya yote ni katika kuleta utamu katika historia ya muziki wa Disco Tanzania.
Image may contain: 5 people, including Muhidin Issa Michuzi, people smiling, people standing, stripes, beard and outdoor
Dj Sweet Francis jina kamaili ni Francis James Bundala,mwaka 1964 alianzisha bendi iliyoitwa The Screemers na Dj Sweet Francis akiwa mwimbaji(singer) hapo ndipo alipopewa jina la SWEET baada ya kusikia sauti yake na jinsi alivyokuwa akiimba iliwakuna sana na wakawa wanasema "YOUR VOICE IS SO SWEET " na ndiyo hapa akawa anaitwa Sweet. Hiyo ni hapa Dar.Bendi The Screamers ilidumu muda mfupi. Mwaka 1965 alianzish a bendi nyingine ya watu 5 wakaiita The Hot Five wakawa wanapiga bugi kila Jumapili mchana hapo Arnatoglo hall Mnazi mmoja. Wakawa wanashindana na bendi ilikuwa inaitwa The Flamming Star.

 Mwaka 1967 June The Hot Five ikavunjika. 1967 Sept. Dj Sweet Francis na aliyekuwa Solo guitarist wakaanzisha bendi nyingine wakapata watu wengine 3 ambao walianza kuwafundisha ambao walikuwa mpiga bass, mpiga rythym na drummer. Bendi wakaiita The TONICS. Mwimbaji- Sweet, Solo- Michael Jackson, Rythym- Green Jackson. Bass- John Morand na Drums- Charles Alowasa. 

Baada ya mazoezi makali mwezi November1967 wakaapata mkataba wa kupiga muziki kila siku hapo Splendid Hotel iliyokuwa inamilikiwa na mtaliano aliyeitwa MOSKA mtaa wa Samora zamani ukiitwa Independence Ave.

Siku moja wakati wanapiga muziki jamaa mmoja ambaye hawakuwa na mazoea naye akaja kwenye stage akaomba apige bongos wakamruhusu, wakati Dj Sweet Francis anaimba na yule jamaa akawa amapiga bongos vizuri sana Dj Sweet Francis akawaambia wenzake kuwa anafaa kuwa drummer lakini wenzake walimkatalia na baada ya kuwasihi sana walikubali kwa sharti kuwa amfundishe kupiga drums mpaka ajue. 
Image may contain: 10 people, including Ahmed Chande and Peter Moe, people smiling, people standing and outdoor
Baada ya kumfundisha kwa muda mfupi akaona ameelewa na baada ya kumpa nafasi kwenye stage alipiga drums na wenzangu wakamfurahia, huyo alikuwa anaitwa Adam Salehe Mwambile (R.I.P.) na tangu siku hiyo Dj Swett Francis akamwambia kuazia leo utaitwa ADDY SALLY,  ilikuwa mwezi April 1968, hilo ndiyo lilikuwa chimbuko la ADDY SALLY. 

May 1968 mkataba ulimalizika hapo Splendid  wakaamua kwenda mikoani.Wakati wote huo Dj Sweet Francis alikuwa mfanyakazi wa NPF sasa ni NSSF.

Dj Sweet Franacis aliamua kuacha kazi maana alivutiwa sana na muziki. July 1968 walifika Arusha wakiwa wanamuziki 5 na fundi mitambo aliyejulikana kwa jina Joseph Magali. 

Yule drummer wa kwanza .walimwacha baada ya kumwona Dj Addy Sally anafaa zaidi. March 1970 Dj Sweet Francis walirudi Dar. May1970  Dj Sweet Francis na Addy waliacha bendi kwa kutoelewana na Michael Jackson ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa Bendi.

July 1970 Dj Sweet Francis alienda Mombasa na kuanza kuimba na Sunshine club. Mwezi Sept.1970 Dj Sweet Francis alimwita Dj Addy Sally Mombas akawa anapiga drums Central night club, May 1971 wakarudi wote Dar. 
Image may contain: 1 person, sitting
Wakati huo The Tonics wakiwa Nairobi waliwaita Dj Sweet Francis na Addy Sally huko, Dj Sweet Francis alikataa ila Dj Addy Sally akaenda.

Dj Sweet Francis akawa anaimba mara moja moja Simba grill Kilimanjaro Hotel wakiwa na bendi kutoka Spain iliyoitwa Los Valdos na hotel ikiwa ya chini ya raia kutoka Israel aliyejulikana kwa jina la LEVY na meneja mkuu wa hotel akiitwa FERGUSON raia wa Canada.

Kwa vile Africana hotel ilijengwa kutokana na faida ya pesa za Kilimanjaro hotel hivyo mmiliki alikuwa mmoja na mwaka 1971 ilianzishwa Gogo Disco baada ya kuhamisha disco kutoka Summit, Kilimanjaro hotel kwenda Afrikana.  Bokha Wilson alikuwa msanii wa Cabaret Simba grill pia kuwa Dj. Summit akahamishiwa Gogo disco hotel Africana. August 1972 Bokha Wilson akarudishwa Simba grill na Dj Sweet Francis akapelekwa Africana Hotel kuwa Disc Jockey Gogo Disco Theque.

Wote waliotajwa hapo mwanzo wameshatangulia mbele ya haki isipokuwa Dj Sweet Francis na Bhoka Wilson hatuna taarifa zake, miaka ya 80 alikuwa Ujerumani. baada ya kuwa Dj wa Gogo disco.
Image may contain: 3 people
Mwisho wa mwaka wa 1972 alikuja Dj. Mactwist akaanza kupiga disco Sea view hotel, nalo likaitwa Sansui disco,

Dj Mac twist hakudumu sana alikuja kuwa Makamu Mwenyekiti wa FAT enzi hizo ikiwa chini ya Mzee Mohamed Mussa. Akaja kugundulika sio raia akatimuliwa na kurudi kwao Kenya

Mark Twist aka Peter Kinyanjui baada ya kugundulika sio raia akapigwa PI na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani enzi hizo Lyatonga Mrema aliyeamuru apewe asindikizwe hadi mpakani. Alipovuka Namanga akala kona na kuelekea UK na alikuja kufariki 2016 nchini Kenya. Mara tu Dj Mc Twist kuacha disco Sansui, Dj.Addy Sally akawa Dj hapo.

Mwezi Nov.1973 Dj Sweet Frncis akapata mkataba mwingine wa kupiga disco Lusaka Zambia katika Club Lagondol.

Baada ya muda fulani Dec.1974 Di Sweet Francis alirudi Dar kwa lilizo na alipotembelea Kilimanjaro Hotel wakampa kazi ya kutafuta bendi wafanye mazoezi kisha tarehe 25 Dec 1974 wakapige kwenye sherehe ya Ubalozi wa Marekani, Dj Sweet Francis aliichukua bendi ya The Rifters wakaenda kupiga na wote wa Ubalozi walifurahia sana mpaka Kilimanjaro Hotel wakawapa nafasi ya kupiga Simba grill mkesha wa mwaka mpya tarehe 31, Dec 1974 na cha ajabu siku hiyo wote wafanyakazi na Maafisa wa  Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania walikuja Simba grill.
Image may contain: 2 people, indoor
Baada ya hapo Dj Sweet Francis alirudi Lusaka. Wakati ule karibu wote kwenye Ubalozi wa Marekani walikua Wamarekani weusi.

Mwaka 1975 July Dj Sweet Francis alirudi tena Dar kwa likizo ndipo alimkuta Dj Addy Sally akipiga disco Mlimani Park huo ulikuwa wakati wa BUMPING. Baada ya mwezi mmoja alirudi Lusaka. 

Mwezi June 1976 Dj Sweet Francis aliitwa Arusha kufungua The Cave Disco Safari hotel, alifika Arusha tar.28 June 1976 kutoka Lusaka, alifungua The Cave Disco tar. 17June.1976, pia alimkuta Arusha Dj Addy Sally na disco la ARUSHA BY NIGHT. January 1977 Dj Addy Sally akaagiza wacheza show Nairobi na Dj Sweet Francis akaleta wacheza show watatu kutoka Dar nao walikuwa Dj Choggy Sly (R.I.P.), Anna Simba na Mwanahamisi hata hivyo Dj Sweet Francis na Dj Addy Sally walikuwa wanashirikiana sana hapo Arusha. March 1977 Dj Addy Sally akurudi Dar. na baadae nae Dj Sweet Francis July 1977 akarudi Dar  na kumwachia Dj Choggy Sly akiwa Dj wa Cave Disco Safari Hotel- Arusha. 
Image may contain: 1 person, indoor
Mwaka 1977 Dec. Dj Sweet Francis alienda Durban Afrika Kusini alienda kuimba Cosmo night club, Febr 1978 alienda Brazil, kwa vile kule wanatumia lugha ya kireno ilibidi ajifunze nyimbo za kiportugese, alirudi Dar. May 1978 na Aug. 1978 akaaenda kuwa mwimbaji wa Cabaret Simba Grill, alikuta bendi ya vijana Watanzania wakipiga Simba Grill baada ya muda wakamaliza mkataba wao, akaingia mzee Makassy ikabidi wajifunze nyimbo zake za show na mzee Makassy aliipenda sana nyimbo moja ya kireno.

Dj Sweet Francis nae mkataba wake ukaisha. Cabaret singer au cabaret artist ni kuwa bendi ikiwa inapiga musiki Wateja huwa wanacheza lakini wakati wa cabaret huwa ni muziki maalum wa muda wa dakika 30 au 45, watu wanakuwa wamekaa na musiki huwa umesimama, cabaret singer unatangazwa kwa kishindo kisha anaingia kwa mbwembwe ukumbini watu wanampigia makofi kisha unaanza kuimba kisha anazungumza nao kwenye kipaza sauti au unatoa matani kisha anaendelea kuimba kwa mpangilio aliouweka baada ya muda wake wa show kuisha anawaaga na wakati anatoka anapigiwa makofi na muda wake unakuwa umeisha na musiki wa bendi unaendelea kama kawaida. 
Image may contain: 3 people, people smiling
Na wakati anafanya cabaret hasimami kwenye jukwaa Bali anaimba huku akizungukia wateja. Hii ndiyo CABARET.

Sept.1978 Dj Addy Sally alienda Lusaka kuwa Dj Club 2000 disco, huko Dj. Addy Sally alipata umaarufu sana kutokana na ujio wa James Brown, kwa kuwa mipigo ya drums nyimbo za James Brown Addy alikuwa anapatia sana. James Brown alifanya show Intercontinental Hotel na Addy Sally akampigia drums. 

James Brown alimfurahia sana Addy Sally na siku ya pili James Brown akaamua kutembelea Disco la Addy Sally na ndipo Addy Sally alipopata umaarufu sana Lusaka. Dj Sweet Francis alienda Lusaka Jan.1979 kumtembelea Addy na kukutana na hizo sifa na Addy Sally akampa picha aliyopiga na James Brown ambayo Dj Sweet Francis anayo mpaka leo na mwisho wa Jan.1979 Dj Sweet Francis akarudi Dar. na Addy Sally akaendelea kupiga Disco hapo Club 2000, Lusaka. 

Mwezi May 1979 Dj Sweet Francis alienda Bandari Grill ghorofa ya 6 New Africa Hotel, Makassy Orchestra walikuwa wanapiga hapo , Dj Sweet Francis akawa amekaa kwenye meza wakiwa wanne ila mmoja walikuwa hawafahamiani, baada ya bendi kupata mapumziko,  Mzee Makasy alipita karibu ya meza waliyokuwa wamekaa Dj Sweet Francis na wenzake alipomuonana akamuomba wakirudi kwenye stage Dj Sweet Francis akaimbe wimbo wa kireno aliokua akiuimba Simba Grill. 
Image may contain: one or more people and outdoor
Dj Sweet Francis alipanda kwenye stage na kuanza kuimba, cha ajabu kila mtu aliufurahia sana huo wimbo na walimshangilia sana na aliporudi mezani kwake, yule jamaa ambaye hakumjua alisimama akampa mkono akasema " Kumbe hapa tumekaa na mwanamuziki mzuri hivi, (akaendelea) Sikia kijana mimi najenga hotel hapo mtaa wa Uhuru na karibu kumalizika, hivyo ikiwa tayari wewe nataka uanze muziki hapo. Dj Sweet Francis akamkubalia, Hotel ikawa tayari Nov.1979  na kabla ya Dj Sweet Francis hajajiunga na Keys Hotel alipiga Disco kwa muda mfupi Mbowe Hotel na hapo ndipo alipomfundisha Dj.Jerry Kotto na Dj Sweet Francis akaanza kupiga Disco Keys Hotel  Dec.1979.

Baada ya Addy Sally kurudi toka Lusaka, mwezi April 1980 wakawa pamoja hapo Keys Hotel akiwa vyombo vya Disco vipya kabisa vikiitwa M3. waliendelea pamoja hapo Keys Hotel lakini kufika Dec.1980 Dj Sweet Francis walishindwa kuelewana na Addy, ikabidi Addy aondoke.

Jan.1981 Dj Sweet Francis akawa na Dj. Seydou na baada ya muda kidogo Dj.Seydou akaondoka baada ya mzee Ndesamburo (R.I.P) kununua vyombo vya Disco na baada ya hapo Dj Sweet Francis akapiga Disco na Dj Johnson Pantaleo (R.I.P) na ndiye Dj Sweet Francis aliyemuacha Keys hotel,
June 1981 ndio ukawa mwisho Dj Sweet Francis wa kupiga disco.
Image may contain: 5 people, people sitting
Mwezi Sept.1981 Dj Sweet Francis alienda Ujerumani na nchi zingine za Ulaya, alirudi Dar. Sept.1983 baada ya mapumziko 1993 Oct. akaanza tena kuwa Cabaret singer hapo International Pub, Kijitonyama nyuma ya Sayansi na Teknolojia mpaka June-August 1994.  Sept 1994 Simba Grill Kilimanjaro Hotel. Nov.2003--June 2004 Cine Club. Hii ndiyo historia yake katika tasnia ya muziki. Mwanamuziki na Disc Jockey "SWEET FRANCIS."

Baada ya kumalizana na hiyo historia ndefu na nzuri ya Dj Sweet Francis sasa turudi tena kwenye historia ya Disco wakiwemo maDj wake.

kumbukumbu inaniambia Motel villa de Tanzania kule Mwananyamala alianza kupiga Dj Agib Show na binti mmoja aliemfundisha alikua anaitwa Diana miller(Rukia) then baada ya Agib akaja Kapten Ngomeley na Dj Pascal baada ya hapo Akaja David Joseph Kim 'Usungu "Lewes 'Seydou
Disco la Motel Villa pamoja na madj wengi kupitia hapa lakini dj maarufu wa hapo alikua Kim and The Boys ambaye pia kuna wakati alikua maarufu katika kupromoti madansa.

Historia ya DiscoTanzania haiwezi kupita bila kuitaja YMCA na ndio moja ya kiwanja kimepitiwa na maDj wengi wazuri, wenye majina na waliovuma sana na hii ni stori ambayo inakumbukwa jinsi ilivyotokea YMCA enzi zile YMCA.

Dj Franco Soferino B aka Frank Kabigi (RiP) ambae nakumbuka aliibuka baada ya kutokea ugomvi wa YMCA na Space 1900 baada ya kutokea kutoelewana baina yao na Space 1900  wakaondoka na vyombo na mataa wakati huo YMCA ikiwa chini ya Arthur Mallya wakaleta vyombo vingine ila hawakuwa na disco lights. Franco akisaidiana na Gibson Mwakamboja (R.I.P.) wakiwa waajiriwa wa YMCA hawakutaka jumapili zipite hivi hivi. Wakatumia glopu za kawaida na vitaa vya krismas kama disco lights. YMCA ikaendelea kuwepo, ndipo akaja Pop Juice(R.I.P.) na vyombo vya discona lights. Disco likaendelea.

Baadaye suluhu ikaja na Space 1900 wakarudi safari hii in charge akawa Super Deo na ma Dj Kalikali na Neagre J

Paul Mc Ghee alianzia Morogoro akiwa na disco la Biribi likiwa chini ya usimamizi wa kaka yake Joseph Kusaga anayeitwa Justine Kusaga. Baadae Disco lilikua chini ya usimamizi wa Joe Kusaga nakubadilika jina na kua Mawingu Dj alikua Paul Mc Ghee na baadae Disco lilihamia Dar likiwa linapiga muziki wake Salender Bridge na ndio ukawa mwanzo wa kukua kwa Disco hilo na kuendelea kupiga Motel Agip, Pool side hotel ya Kilianjaro kila Jumapili, New Africa ghorofa ya Saba, Twiga na baadae wakaanzisha Disco la Bolingo Tazara, na kuendelea kupanua wigo wao mpaka Arusha. Clouds walikua na maDj wengi na Disco hili lilikuza vipaji, vijana wengi wa enzi hizo wakiwemo Boni Luv, Stev B (R.I.P.), Rankim Ramadhani (R.I.P.) na wengine wengi wakiwasaidia maDj Jesse Malongo, Dj Young Ray akiwemo Joseph Kusaga  mwenyewe.

 Hapa ni baadhi ya maDj waliokua chini ya Joe Kusaga Dj Jesse Malongo, Sterwat Chiduo (Dj Young Ray), Elliud Pemba, Dj Louis, Ebonite Who jack, Julius Tandau, Julius Kagaruki, Boni. Luv, Stev B (R.I.P.), Clouds Ma Dj tulikuwa Elliude Pemba (Elliwood), Jesse Malongo (Babyface), Joseph Kussaga (Emperor), Stuart Chiduo (Young Ray), Julius Tandau (Jet), Richard Mazula (Ebonite woo Jack)
Elliud Pemba (Dj Elliwood) safari yake ya muziki imeanzia Clouds pale Motel Agip Snack Bar, Kilimanjaro Pool Side, Seventh Floor New Africa Hotel, Dar es Salaam Institute na Twiga.

Dj Ellud Pemba ndio niliyemwachia Dj Boni luv U Dj mwaka 1992 baada ya kwenda Shule na 1994 Kuanza kazi nyingine ITV.

Disco la Space 1900 wakati huo likiwa chini ya usimamizi Sudi Ally Salehe lilianzia Mbowe chini ya maDJ Saydou na Gerry Kotto na Sudi Ally Salehe walikua washirika na Dj Saydou walichangia vyombo vya muziki disco pamoja.

Baada ya Sudi Salehe kuwa kushirikiana na Dj Saydou kwa muda, siku moja maelewano hayakua mazuri wakafarakana na Dj Saydou kuondoka space 1900 na ndio ukawa mwanzo wa kuingia maDj Chris Phaby, Ebony woo Jack na wengineo.

Mwaka 1987 Disco la Space 1900 liliingia mkataba na Ushirika Club (Magoti) kufanyia matengenezo jengo na wao kufunga vyombo vipya vya muziki kwa muda wa makubaliano yao mpaka watakapo maliza deni Disco lao lilikua likiitwa Vision 1900 na baadae walianzisha Disco lingine hotel Continental lililokua maarufu kwa jina la Valentino na huo ndio ukawa mwanzo wa kuingia kwa Dj Danny Star ambaye alitokea Zambia wakishirikiana na Dj Lawrence Kadri, Richie Dillon na baadae space 1900 walianzisha Dico toto YMCA, na Vision 1900 na pia Space 1900 walishapiga muziki wao Msasani Beach Club kabla ya Jetset ya Dj Russell kukamata Club hiyo ya jeshi la JWTZ.

MaDj wengine waliofanya kazi na Space 1900 walikua ni Joe Holela, Paul Mc Ghee, Super Deo, Young Millionaire, John Kitambi, Mr A na Dj Luke Joe.

Dj Richie Dillon ndie Dj alikuwa kati ya maDj wa kwanza kwanza kuingiza mixing ya beat to beat Tanzania  miaka ya 1990 huko Mwanza yeye alianzia muziki wake 1984-85 Disco la Alshars Tikkha Disco na baadae akajiunga na Golden Gates Discotheque Mwanza hotel, baadae alijiunga na Disco la Magnum kabla hajahamia Nairobi mwaka 1987-88 alipokwenda kupata ujuzi wa kumix beat to beat mixing katika club ya Boomerang chini ya marehemu Majid Fundikirs(Dj Tubbs) na boss wake Dj Pacco Perez kabla ya kurudi tena na kujiunga na Disco la Magnum 1990 na baadae aliingia Dar kwa kupiga Disco la Valentino, Club Mix (cassanova Masaki) na kurudi tena Continental wakati huo akiwa na Dico la Club Mix, pia alishapiga ghorofa ya saba Clouds, Twiga Hotel na Clouds na kuhamia Club ya Bilicanas upande wa Casino.

Madisco mengine aliyopiga ni - Masuka Motel - Morogoro- Butiama Hotel - Shinyanga
- Pamba Roof Hotel Mwanza- Oysterbay Hotel - Club Mix- XTC - Oysterbay Hotel- La Dolce Vita
- Dar Institute- Kilimanjaro Hotel - Swimming Pool (Clouds)- Bahari Beach Hotel (Clouds)

Disco lingine lililotamba miaka hiyo ni Disco Parliament chini ya maDj Big Joe na Dj Piopose katika miaka 1986-1990 waporomosha muziki wao Kunduchi Beach hotel, Dj Big Joe ambaye jina halisi ni Joseph Shawa na Dj Piopose akijulikana kama Pius Ntare walipiga muziki pia katika sherehe mbalimbali.

Disco la Parliament lilipiga muziki wake kwenye club ya Princes chini ya Dj Joe na Dj Edo Cool.

Dj Eddie Grant uDj wake ulianzia mtaani enzi hizo alipokua akiishi Kurasini mwaka 1988 na baadae akajiunga na Biashara Club akiwa kama dj wa Silver Town Disco Sound maisha yake ya uDj ndio yakawa yameanzia hapo na baadae alijiunga na Studio 35 pale High Way wakiwa pamojana Dj Cool Joe (R.I.P) hii ilikua ni 1989 wakati huo akiwa mwanafunzi NVTC Chang'ombe na baada ya kumaliza chuo alijiunga na FM55 Disco Iringa Club, mkoani Iringa 1989-1989 na baadae 1991 alihamia jijini Mwanza na kujiunga na Disco lililokua likiendesha shughuli zake Nata Hotel na kwa umahiri wake wa kupiga muziki alifanikiwa kuwakamata wadau na wapenzi wa muziki wa Disco wa jiji hilo.

Mwaka 1993 alirudi Dar na kuanza kupiga Disco Imasco Club ambako alidumu kwa miezi 7 tu kabla hajanunuliwa na tajiri kurudishwa Mwanza na yeye kuambatana na Dj Young Millionaire wakati huo Dj Young Millionaire akiwa anapiga muziki Vision 1900 wakati huo Disco hilo la Vision likiwa halifanyi vizuri. Dj Eddie Garant na Dj Young Millionare wakaelekea Mwanza na kuwa waajiriwa wa na KAM Disco ndani ya hotel ya Deluxe. Dj Eddie Grant alipiga muziki hapo kwa miaka 8 na kupata mafanikio makubwa na kuweza kununua sound yake mwenyewe na kuanza kupiga muziki wa party na matamasha mbalimbali na mwaka 1999 wakaanzisha yeye na Clouds Disco la Bolingo Yatch Club na mwaka 2000 mpaka 2003 akaanzisha Disco Club Capri Cabana , mwaka 2005 akapiga Rumours Pab muziki wa Old school na katika ufunguzi huo aliwaalikamaDj Saydou, JP Pantalakis, Kim and The Boys na Dj Coll Joe.

Dj mwingine aliyetamba ni Dj Habib ambaye kwa sasa anaendesha maisha yake nchini Uingereza, Dj Huyu mahiri alianza muziki wa Disco Club ya Bilicanas 1994 wakati huo akiwa na Dj 45 na Dj Luke Joe na baadae alijiunga na Mambo Club 2000-2001. Kwa sasa Dj Habib yupo Uingereza anapiga Club ya Tiger Tige ambayo alianzia kupiga kuanzia 2010.

Dj Luke Joe alianza safari yake ya uDj mwaka 1978 wakati huo akiwa sekondari baada meneja wa Disco la Stereo II Michael Kisaka kufuata na kumwomba ajiunge na Disco hilo baada ya Dj Agib Show kuwazengua kwa kudai kulipwa zaidi. Dj Luke Joe alijiunga rasmi na Stereo II ambayo ilikua chini ya mmiliki Kessy Sakapala (R.I.P.) meneja akiwa Michael Kisaka na baada ya muda Disco lilihamia Kunduchi beach hotel.

Mwaka 1981 Disco liliingia mkataba na Ushirika Club (Magoti) na Dj Luke Joe akipiga Disco peke yake na wakati huo kulikua na bendi ya Ushirika wana njatanjata iliyokua ikipiga muziki wa dansi siku ya Jumatatu hadi alhamisi na Disco likianzia Ijumaa hadi Juamapili. Dj Franco Kabigi (R.I.P.) alijiunga baadae mwaka 1982 na kuendelea kusumbua kwenye jiji la Dar enzi hizo huku wakichuana vikali na Mbowe Hotel iliyokuwa chini ya madj wake Saydou na Jerry Kotto na YMCA kukiwa na DJ Kalikali (R.I.P.) na Niga Jay.

Enzi hizo madisco hayo yalikua yakishindana na nyimbo mpya kila Disco utakuta madj kupiga nyimbo kali huku baadhi yao wakiwa na baadhi ya nyimbo zisizo fanana.

Mwaka 1987 Kessy Sakapala aliumuuzia Disco shemeji yake Mvungi wakati huo akiwa meneja wa Tanesco Iringa na Stereo II ikaendeleo kutesa Railway Club Iringa na DJ Sweet Coffee alijiunga kumwongezea nguvu Dj Luke Joe na mwaka 1989 ulikuja ujio wa Disco la XTC na kupiga muziki wake Iringa Club na ndio ikawa chanzo cha Disco la Stereo II kuporomoka na kupiga sabasaba Iringa na baadae Makambako na mwaka 1990 Dj Luke Joe alifiwa na baba yake na yeye kuelekea Tarime kwa mazishi, wakati Dj Luke Joe akirudi kutoka tarime alikutana na Dj Richie Dillon Mwanza na kukubaliana amwonyeshe jinsi ya kumix beat na beat kwani Dj Richie Dillon alikua dj wa kwanza Tanzania kujua kupandishia muziki kwa beat zinazofanana.

Dj Luke aliporudi Iringa alihamia Disco la Ruaha International wakati huo likiwa chini ya Hussein Kipara aliyekua amekuja na vyombo vya Disco pale na baadae Disco lilihamia kwenye uwanja Samora kabla halijamaliza muda wake. na Dj Luke Joe kurudi Dar na kujiunga na Space 1900 na kuanza kupiga Disco Vision 1900 pale ushirika Club (Magoti).

Dj Luke Joe aliendelea kuwa chini ya Disco la space 1900 kwa kupiga madisco ya Space 1900 kama vile Lang'ata, Valentino, Boogie YMCA na baadae kuwa mshindi wa mashindano ya madj yaliyofanyika Lang'ata chini ya marehemu Shaban Sato.

Mwaka 1994 Dj Luke Joe alijiunga na Bilicanas akiwana Madj wengine Dj Habib na Dj 45, hapo alipiga Disco kwa mwaka mmoja kabla hajahamia Mambo Club mwaka 1995 na baada ya miaka miwili Mambo Club ilifungwa kwa kufanyiwa marekebisho na maDj wengine aliopiga nao hapo Mambo Club walikua ni Dj MacKay, Dj Vumi, Dj Rico (R.I.P) na Dj Ommy.

Mwaka 1997 Dj Luke Joe alipiga Disco la Bolingo FM Club (Lang'ata) likiwa chini ya Felician Mutta akiwa na Dj Kishoka na baadae akajiunga Dj Venture na FM wakaanzisha Dico lingine IMASCO Temeke na Dj Luke Joe na Dj Kishoka wakahamishiwa huko wakimwacha Dj Venture FM Club akishirikiana na bendi ya FM Academia.

Mwishoni mwa 1998 Dj Luke Joe alirejea Mambo Club na kupiga Disco hapo mpaka mwaka 1999 na baadae kuondoka kuelekea Marekani na kupiga muziki wa Disco katika club mbalimbali na majimbo tofauti.

Dj Mr A huyu yeye alianzia muziki wa disco kama dansa alishinda mashindano mengi enzi hizo akiwa na patna wake wa kudansi Bi. Zainab safari yake ya uDj alianzia Rungwe Oceanic Hotel Disco 110 kuanzia 1984 mpaka 1987 baada ya hapa ndio alijiunga na Space 1900 pale Hotel Continantal na Valentinos/Club mix

Hii ni historia ya baadhi ya madj waliotamba Tanzania shukrani kwa madj waliokubali kushirikiana kuandika historia hii wakishiirikiana na Dj Luke Joe.

1 comment:

Anonymous said...

Safi sana! Dj Rachy Cuty je?