Dar es Salaam. Siku moja baada ya mtandao wa Jamii Forum kusitisha huduma, mbunge wa Mtama, (CCM) Nape Nnauye, amelumbana na wafuasi wake katika mtandao wa kijamii wa twitter.
Nape ndiye aliyeanza kuandika jana katika akaunti yake ya twitter, akisema;
“Hili la JF linafikirisha! Ukizuia watu kusema wayawazayo unaweza Kutana nao...kimya kimya!”
Baada tu ya kuandika hayo, wafuasi wake walimiminika na kuanza kumuhoji maswali naye hakusita kuwajibu na kuwahoji.
Mmoja wa wafuasi wake, mwenye jina la Thadey alimjibu akisema;
“Makosa ulianza wewe kupeleka mswada wa vyombo vya habari bungeni,”
Nape akamjibu: “Una uhusiano gani katika hili?”
Mfuasi mwingine, mwenye jina la MimivsDunia akamjibu Nape akisema:
“Hili siyo swali brother @Nnauye_Nape . Safari moja huanzisha nyingine. Ulipoanza kuwanyamazisha Wabunge ilikuwa hatua kubwa ya kuwanyamazisha Watanzania wote. Tutakushukuru kama ukilipokea kosa lako. #Muungwana akivuliwa nguo huchutama,”
Malumbano yakaendelea, mfuasi mwenye jina la BondeniTz akamjibu Nape akisema:
“Sheria uliisimamia ikapita kwa mbwembwe ukafanya party ya kujipongeza nyumbani kwa Makamba Dom ukajiita ni waziri mjanja kuliko wote, ukajisifu kuwa mawaziri wote waliopita walishindwa kuupitisha muswada ule bali ww uliweza, nilikuwepo kwenye party, acha unafiki hifadhi aibu yako.”
Nape akamjibu BondeniTz akimwambia:
“Thibitisha uhusiano uliopo kati ya sheria ya Habari na Sheria ya Mitandao vinginevyo acha kutoka mapovu hovyo..... kukaririshwa jambo usilolijua kiswahili inaitwa uzwazwa.”
Mfuasi mwingine mwenye jina la Andrew Mariki akamwambia Nape hivi: “Mkuu haya ni matokeo ya ulichokuwa unapigania kipindi ukiwa waziri mwenye dhamana. Tuambie kama ulishinikizwa na kikombe hiki kikuepuke.”
Nape akahoji tena akasema: “Kuna uhusiano gani??? Ni vizuri kusema unachokijua.”
Mfuasi mwingine aitwaye WillbJr akamjibu Nape akisema: “Yajayo yanafurahisha sana na tutaona mengi sana Ila Mh. ulikuwa sehemu ya kutungwa kwa sheria hizi ukiwa waziri leo hii inakuumaje kwa sheria husika kuanza kufanya kazi, ipo siku na tweeter na Whatsapp nayo tutaikuta gizani maana maumivu huanza polepole.”
Mfuasi mwingine aitwaye Edmond akauliza: “Lakini mkuu, sheria (tena iliyotungwa wakati wewe ni waziri mwenye dhamana), inalazimisha kila mwenye Blog, OnlineTV, forum etc., wajisajili TCRA... Kwa sababu ambazo mimi sizijui JF wamechelewa kujisajili; Ulitegemea TCRA wafanye nini?”
Nape akamjibu: “Unahakika na sheria unayoinukuu au umekaririshwa?”
No comments:
Post a Comment