ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 20, 2018

Wadau wa Sekta ya Filamu Mkoa wa Songwe waipongeza Serikali

 Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo akiwaahidi wadau wa sekta ya filamu Halmashauri ya Tunduma (hawapo pichani) kuhusu kupokea maombi yao na kuwaahidi kuaanda mafunzo ya siku tano yatakayohusu uandaaji wa miswada na elimu juu ya upigaji picha wa filamu alipokuwa akizungumza katika warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa filamu Mkoa wa Songwe iliyoandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania yaliyofanyika leo Mjini Vwawa Wilayani Mbozi.
 Mmoja wa wezeshaji Bibi.Christa Komba akiwasilisha mada ya uhusiano kati ya mwigizaji na mwongozaji kwa kuwataka wadau wa filamu kuchagua wahusika wenye vigezo vya kuvaa uhusika badala ya kuangalia sura katika warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa filamu Songwe yaliyoandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania na kufanyika leo Mjini Vwawa,Wilayani Mbozi.
 Kamada wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe Bw.Damas Sutta (kulia) akizungumza na wadau wa sekta ta filamu mkoa huo (hawapo pichani) walipokuwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania yaliyofanyika leo Mjini Vwawa,Wilayani Mbozi kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo.
Wadau wa sekta na filamu Mkoa wa Songwe wakimsikiliza kwa makini mtoa Mada ya elimu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka kwa Afisa wa TAKUKURU Bw.Audronicus Kivyiro katika warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau hao yaliyoandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania na kufanyika leo Mjini Vwawa,Wilayani Mbozi.

Na Anitha Jonas – WHUSM- Vwawa, Mbozi
Wadau wa Sekta ya Filamu Mkoa wa Songwe waishukuru serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kwa kuwapatia fursa ya mafunzo ya kujenga uwezo katika uandaaji wa kazi za filamu kwa lengo la kuboresha kazi za filamu zinazoandaliwa nchini.
Shukrani hizo zimetolewa leo Mjini Vwawa, Wilayani Mbozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Wanatasnia wa Filamu Mkoa wa Songwe Bw.Tegemea Hasunga mara baada ya kuwasilishwa mada mbalimbali ikiwemo mada ya uandishi wa Miswada ya filamu na Utafiti ambazo zinawajengea uwezo wa kujua namna ya kuaanda miswada hiyo ambayo ndiyo roho ya kazi za filamu. 
“Kiukweli kabisa nimejifunza mengi sana kupitia warsha hii ya siku mbili kwanza nimepata kuelewa kuwa katika uandaaji wa kazi za filamu ni lazima kufanya utafiti wa kile unachotaka kuigiza na pili ni lazma kuandaa mswada kwani mswada ndiyo utakaonipa mwelekeo mzima wa filamu nitakayoandaa na pia miswada hii inatakiwa kuandaliwa katika mifumo ya kitekinolojia ambayo ipo mitandao ambapo hapo mwanzo sikuwa nafahamu haya,”alisema Bw.Hasunga.
Akiendelea kuzungumza kuhusu warsha hiyo Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa mafunzo haya yamemsaidia sana pia kufahamu namna ya kuboresha kazi zake na kulijua soko lake kulingana na utafiti aliyofanya na kile atakachotaka kuigiza.
Kwa upande wa Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi.Joyce Fissoo alitoa pongezi kwa wadau wa filamu mkoa huo wa Songwe kwa kutoa ushirikiano katika mafunzo hayo na kutoa ahadi ya ofisi yake kuandaa mafunzo ya siku tano kwa halmashauri ya Tunduma kutokana na kuonekana kuwa na wadau wengi ambao wanajihusisha na uandaaji wa kazi za filamu.
“Katika warsha hii wadau waliyotoka Tunduma wamejitokeza kwa wingi sana na ofisi yangu imepokea kwa mikono miwili maombi yao yakuiomba ofisi yangu kufika katika halmashauri yao kwa ajili ya kuwapatia mafunzo katika suala la uandaaji wa kazi za filamu pamoja na utalaamu wa upigaji picha katika kazi za filamu (cinematography),”alisema Bibi. Fissoo. 
Katibu Mtendaji huyo aliendelea kuwa sisitiza wadau hao kuwa ni muhimu waendeshe shughuli zao za uandaaji wa kazi za filamu kwa kuzingatia sheria na utaratibu uliyowekwa na serikali kwani serikali haitamuonea haya mdau yeyote atakaye peleka kazi yake soko bila kupitisha Bodi ya Filamu kwa ajili ya ukaguzi kwani kinyume na hilo mhusika atapigwa faini ya kulipa pesa nyingi.
Pamoja na hayo nae mmoja wa wawezeshaji Bi. Christa Komba aliwasihi waongozaji wa kazi za filamu kwamba ni lazma kuzingatia upangaji wa wahusika kwa kuangalia uwezo wa mhusika huyu kuvaa uhusika badala ya kuangalia sura au vigezo ambavyo haviendani na tukio husika katika filamu hiyo.

Halikadhalika nae mmoja wa wadau aliyehudhuria warsha hiyo ambaye ni muigizaji  Bw.Franckreen Sebenza alieleza kufurahishwa na elimu ya kupambana na rushwa iliyotolewa katika mafunzo hayo kwani kama mwigizaji amepata uelewa mpana na namna usiri wa mtoa taarifa unavyoweza kulindwa na kupitia elimu hiyo basi anaweza kutoa elimu kwa jamii inayomzunguka.

No comments: