ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 11, 2018

Tanzania na Namibia kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Elimu ya juu

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akijadili jambo na Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Namibia, Dkt. Tjama Tjivikua mara baada ya kuwasili chuoni hapo kwa mazungumzo rasmi ya kikazi yaliyofanyika tarehe 09 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia. Pembeni ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester Ambokile.
Katibu Mkuu, Prof. Mkenda akitembelea maeneo ya chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia ili kuweza kujionea uendeshaji wa vipindi vya masomo na mpangilio wa majengo kwa ajili ya madarasa na malazi ya wanafunzi. 
Katibu Mkuu, Prof. Mkenda na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na uongozi wa chuo, wa kwanza kulia ni Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria, kulia kwa Prof. Mkenda ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Ambokile na pembeni yake ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Bw. James Lugaganya. 

Serikali ya Tanzania imeonesha nia ya wazi ya kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu na Serikali ya Namibia ambapo ushirikiano huo utawezesha walimu na wanafunzi kuwa na progamu za kubadilishana kwa lengo la kupeana uzoefu na kujengeana uwezo.

Hayo yamesemwa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf F. Mkenda katika chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia Mjini Windhoek, Namibia tarehe 09 Agosti 2018.

Katika ziara hiyo Prof. Mkenda aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake mjini Pretoria nchini Afrika Kusini, Mhe. Balozi Sylivester Ambokile, Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe. Theresia Samaria na Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. James Lugaganya.

Lengo la ziara hiyo ni kujadili namna ya kuongeza ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu kwenye masuala ya utafiti na ugunduzi katika taaluma za teknolojia zinazotolewa na vyuo vitakavyoingia makubaliano ya ushirikiano.

“Nimekuja tushirikishane mikakati mbalimbali tunayoweza kujiwekea ili kuvifanya vyuo vyetu viwe bora ndani ya kanda na Afrika kwa ujumla pia tujadili mbinu mpya za kielimu ambazo Tanzania na Namibia zinaweza zikashirikiana,”alisema Prof. Mkenda

Pia akaeleza nchi nyingi za Afrika zinapata changamoto ya uwezo mdogo na uhaba wa rasilimali fedha katika kuhakikisha upatikanaji wa malazi kwa wanafunzi, upatikanaji wa elimu kwa vitendo na kwamba ni vema Tanzania na Namibia zikatumia fursa za ushirikiano wa elimu zinazosainiwa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia, Dkt. Tjama Tjivikua alieleza kuwa hadi sasa chuo kimefanikiwa kuanzisha ushirikiano na taasisi, makampuni na viwanda mbalimbali nchini humo na hata nje ya nchi ili kuwawezesha wahitimu katika chuo hicho kupata nafasi ya elimu kwa vitendo.

“Jitihada hizi zimeshaanza kuleta matunda kwa kuwa kwa sasa wahitimu wa chuo hiki wamefanikiwa kupata ajira katika taasisi hizo na wengine walifanikiwa kupata ajira kabla ya kuhitimu muda wa mafunzo” alisema Dkt. Tjivikua

Vilevile chuo kinashirikiana na wadau mbalimbali ambapo alieleza Tanzania ni mmoja wa wadau kupitia chuo cha Sayansi ya Kilimo Sokoine(SUA) na chuo kikuu cha Ardhi, wadau wengine ni pamoja na Afrika Kusini, Cameroon, Kenya, Botwana, Uswiss, na mashirika mengine ya kimataifa.

Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Sylivester Ambokile naye alisema kwa kuwa jumuiya ya wanamibia imezungukwa na jamii inayozungumza Kiswahili hivyo ni vema ushirikiano uliopo ukazidi kuimarishwa kwa kuingiza lugha ya Kiswahili katika idara za lugha za kigeni kwenye vyuo vikuu nchini Namibia.

“Katika hafla ya utambulisho wangu kwa Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Hagae Geingob niliwasilisha wazo la Kiswahili kuingizwa katika Idara za Lugha ya kigeni na lilipokelewa vizuri, hivyo kwa sasa ofisi za ubalozi zinafanya jitihada za kukumbushia katika sekta husika ili utekelezaji wake ukamilike mapema”. alisema Mhe. Balozi Ambokile

Nchini Namibia elimu ya juu imeanza mwaka 1979/1980 kutokana na kuchelewa huko kuliifanya Namibia kuhitaji Walimu wa taaluma mbalimbali kutoka mataifa mengine. Tanzania ni miongoni mwa nchi yenye walimu wengi katika vyuo vikuu ya Namibia. Pamoja na kuwepo kwa ushirikiano huo Chuo kikuu cha Namibia cha Sayansi na Teknolojia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992 kimekuwa kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) katika kupata wataalamu wazuri wa masuala ya mifugo ambao wamekuwa wakirejea baada ya masomo na kulitumikia taifa kwa tija.
Mazungumzo yakiendelea.

No comments: