Advertisements

Saturday, August 4, 2018

ZANZIBAR YAJIVUNIA UHUSIANO NA INDONESIA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Indonesia, Muhammad Jusuf Kalla. Viongozi hao wamesisitiza haja ya kuzidisha ushirikiano katika maendeleo.

Viongozi hao walizungumza Ofisi ya Kalla mjini Jakarta Indonesia na mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri wa pande zote mbili.

Rais Dk Shein alimpongeza Makamu wa Rais wa Indonesia kwa mwaliko wake huo muhimu unaoimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Indonesia, na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla na makhsusi kwa Zanzibar.

Alimweleza makamu huyo wa Rais Tanzania inajivunia kwa kiasi kikubwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo ulioasisiwa na viongozi wa nchi hizo tangu miaka ya 60 na kuahidi utaendelezwa.

Alisema tangu mwaka 1964 kulikuwa na uhusiano na ushirikiano mkubwa wa Zanzibar na Indonesia katika biashara ya karafuu ambapo zao hilo lilikuwa likizalishwa kwa wingi zaidi na bei yake ilikuwa juu katika soko la dunia Indonesia, ikiwa moja ya wanunuzi wakubwa.

Dk Shein alieleza Indonesia imekuwa ikiunga mkono juhudi za Zanzibar kwa kusaidia maeneo mbali mbali ikiwemo kuwajengea uwezo wananchi katika elimu na kilimo na kusisitiza haja kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano.

Kwa upande wa kilimo, Rais Dk Shein alieleza haja ya kuongeza uzalishaji mpunga sambamba na kuangalia kilimo cha mwani na mazao yake.

Dk Shein alieleza haja ya kuirejesha biashara ya karafuu na kuwawezesha vijana kujiajiri katika kilimo kwa kuwapatia taaluma ya teknolojia mpya kwenye kilimo cha mikarafuu.

Katika uvuvi, eneo jipya la ushirikiano, Rais Dk Shein alieleza kuwa ni vyema na eneo hilo likaangaliwa kwa upeo mkubwa zaidi hasa katika kuimarisha uvuvi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwenye kuvua hasa katika bahari kuu.

Kuhusu sekta ya utalii, Rais Dk Shein alisema juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuhakikisha watalii wanaongezeka ikizingatiwa sekta hiyo inachangia asilimia 80 ya mapato ya serikali kwa fedha za kigeni sambamba na kuchangia kiasi kikubwa katika pato la Taifa.

Kuhusu utalii kipengele cha ukarimu, alisema ni vyema ushirikiano ukaimarishwa kati ya pande mbili hizo hasa ikizingatiwa tayari Indonesia yenyewe imeshapata mafanikio makubwa.

Dk Shein alisema mbali na juhudi hizo pia, hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha utalii wa Zanzibar unatangazwa na kusisitiza ili utangazwe vizuri, ni vyema kukawa na njia nzuri za kuwasafirisha watalii.

Rais Dk Shein pia alitumia fursa hiyo kueleza haja ya kuwepo na kuimarisha ushirikiano wa nyanja ya utafiti na maendeleo ambalo ni eneo lingine la ushirikiano na kupelekea taasisi za elimu kuhusishwa ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Taasisi ya Afya pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo.

Alisema taasisi hizo ni vyema zikashirikiana na na za Indonesia katika nyanja mbali mbali na kubadilishana taaluma na uzoefu chini ya Mpango wa Ushirikiano wa Nchi za Kusini mwa dunia katika utalii, kilimo, afya na elimu.

Dk Shein alieleza tayari Zanzibar ina vyuo vitatu vya Amali kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana wa kujiajiri, hivyo aliona haja kwa mawaziri husika kukutana pamoja kujadili namna bora ya kushirikiana katika nyanja hiyo.

Akieleza suala la uchumi wa kisasa, Rais Dk Shein alieleza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano katika kuimarisha uchumi huo kwa kuangalia uwezekano kuwekeza katika miradi ya miundombinu kushirikiana na sekta binafsi.

Rais Dk Shein alimwalika Makamu huyo wa Rais wa Indonesia kuhudhuria sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 2019 ambapo kiongozi huyo alikubali mwaliko huo.

Makamu wa Rais wa Indonesia, Muhammad Jussuf Kalla alimpongeza Rais Dk Shein kwa kukubali mwaliko wake huo akisema Indonesia itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo ambao umewekwa na waasisi wa mataifa hayo.

Alisema uhusiano huo ulianza kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Baba wa Taifa hilo, Soekarno Hatta.

Alisema kuna haja ya kuongeza ushirikiano hasa katika sekta ya biashara kati ya pande mbili hizo kutokana na soko kubwa la bidhaa za nchi hizo.

Kuhusu sekta ya utalii, alitaka ushirikiano kati ya pande mbili hizo utasaidia kuimarisha sekta hiyo hasa ikizingatiwa Zanzibar ina vivutio vingi vya kitalii zikiwemo fukwe nzuri.

Alieleza kutokana na Indonesia kuwa na Chuo Maalum cha Kitalii, wanaona iko haja ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya utalii katika nyanja ya mafunzo.

Aliahidi kuunga mkono uimarishaji sekta ya kilimo kwa kutoa mafunzo kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga na kueleza haja ya vijana wa Kizanzibari kwenda kujifunza nchini humo kutokana na nafasi maalum watakazozitoa.

Alisema Agosti 26 mwaka huu Indonesia itafanya mkutano wa kimataifa wa kilimo ambao utagusia kilimo cha mpunga na kutafuta njia za kuwasaidia vijana kujihusisha na kilimo.

Alitilia mkazo kubadilishana uzoefu kwa vijana huku akieleza namna ya kuwasaidia vijana kwa kuwapa ufadhili kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo utalii, uvuvi, mifugo na kilimo.

Alisema nchi yake imekuwa ikitoa mafunzo ya amali kwa vijana na mbali ya mafunzo hayo pia, wataongeza maeneo mengine ya uvuvi, utalii, mifugo, kilimo kwa vijana wa Zanzibar.

HABARI LEO

No comments: