Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Bukama, wilayani Bunda, Septemba 19, 2018.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukama wilayani Bunda, wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika eneo hilo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Busore, Septemba 19, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lydia Bupilipili akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) na wananchi wa kijiji cha Salama ‘A’ (hawapo pichani), akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili-kushoto) akipokea fimbo maalum inayoashiria uongozi mahiri kutoka kwa wazee wa kijiji cha Bukama wilayani Bunda; wakati wa hafla ya uwashaji rasmi umeme katika eneo hilo iliyofanyika Septemba 19, 2018. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lydia Bupilipili.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu akizungumza, wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia), alipofika ofisini kwake kabla ya kuanza ziara ya kazi wilayani humo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme. Ziara hiyo ilifanyika Septemba 19, 2018.
Kutoka kushoto ni Mbunge wa Serengeti Marwa Warioba, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu wakijadiliana jambo, wakati Waziri alipotembelea Jengo la Upasuaji na Maabara ya Hospitali ya Wilaya hiyo na kuwasha rasmi huduma ya umeme. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme Septemba 19, 2018.
Na Veronica Simba – Mara
Wananchi wametakiwa kuondoa hofu kuwa umeme unaosambazwa vijijini kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ni mdogo usioweza kutumika kwa shughuli kubwa za kibiashara kwani si kweli, kwakuwa umeme huo una nguvu sawa na umeme mwingine na unaweza kutumika kwa matumizi yote ikiwemo viwanda.
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, wakati akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali katika Wilaya za Bunda na Serengeti mkoani Mara, pamoja na Bariadi mkoani Simiyu, Septemba 19, 2018 akiwa katika ziara ya kazi.
Waziri Kalemani alisema kuwa, baadhi ya watu wamekuwa na hofu kuwa huenda umeme huo ambao Serikali inausambaza vijijini ni mdogo usioweza kuendesha shughuli kubwa za kibiashara zinazohitaji umeme mkubwa.
“Naomba niwahakikishie kwamba, umeme wa REA hautumiki kwa ajili ya kuwashia taa tu, bali ni umeme kama ulivyo umeme mwingine na una uwezo wa kutumika katika shughuli zote hata kuendeshea viwanda vikubwa.”
Akieleza zaidi, Waziri alifafanua kuwa, lengo la Serikali kupeleka umeme vijijini kupitia Mradi wa REA ni kuhakikisha umeme huo mbali na kutumika kwa matumizi madogomadogo ya kawaida, utumike zaidi kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo na hata vikubwa, ili kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Alisema kuwa, katika kuwezesha uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria viwanda hivyo vianzishwe vijijini ambako ndiko kwenye rasilimali nyingi, na kwamba Serikali inatambua kuwa umeme ndiyo ‘injini’ ya uchumi wa viwanda; hivyo ni lazima upelekwe umeme unaoweza kukidhi matakwa hayo.
Aidha, Waziri kalemani alisema sababu nyingine ya Serikali kupeleka umeme vijijini ili kuwezesha shughuli kubwa za kiuchumi ni ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya watu wengi hususan vijana kukimbilia mijini ili kujitafutia maisha. “Tunataka vijana, ambao ndiyo nguvu-kazi ya Taifa wabaki katika vijiji vyao na kufanya shughuli za maendeleo wakiwa hapahapa.”
Waziri Kalemani aliwahamasisha wananchi, wakiwemo wanawake na vijana, kuutumia umeme ambao Serikali inawapelekea kwa shughuli mbalimbali za ujasiriamali kama vile saluni, kuchomelea vyuma, mashine za kusaga na kukoboa nafaka na shughuli nyingine mbalimbali za kimaendeleo.
Vilevile, alihamasisha uongozi wa halmashauri za Wilaya, Vijiji na Kata, kuhakikisha taasisi mbalimbali za umma zinaunganishiwa nishati hiyo muhimu, kwa kushirikiana na timu ya wataalam kutoka TANESCO, REA na Wakandarasi katika kubainisha maeneo kulipo na taasisi husika.
Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliwasha rasmi umeme katika Majengo ya Maabara na Upasuaji ya Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Vijiji vya Bukama na Nyangere wilayani Bunda, Shule ya Sekondari Itilima na Kijiji cha Luguru vilivyopo wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Pia, alizungumza na wananchi wa maeneo hayo pamoja na wa Kijiji cha Salama ‘A’ kilichopo Bunda, ambapo Mradi wa Ujazilizi wa Umeme (Densification) unatekelezwa.
No comments:
Post a Comment