Gavana wa Jimbo la Shandong lililopo mjini Beijing nchini China Yu Xiao-ming akimsililiza mtoto aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kusubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo. Gavana huyo pamoja na ujumbe wake walitembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akipokea zawadi ya picha ya moyo kutoka kwa Gavana wa Jimbo la Shandong lililopo mjini Beijing nchini China Yu Xiao-ming alitembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Gavana wa Jimbo la Shandong lililopo mjini Beijing nchini China Yu Xiao-ming akizungumza kuhusu kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya jimbo hilo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Picha na Genofeva Matemu – JKCI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na Gavana wa Jimbo la Shandong lililopo mjini Beijing nchini China Yu Xiao-ming wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa JKCI na wajumbe kutoka China mara baada ya kumalizika kwa ziara ya kutembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Na Anna Nkinda – JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kutanua huduma zake kwa kutoa matibabu ya moyo kwa kuwafuata wananchi wenye matatizo hayo katika hospitali za kanda zilizopo hapa nchini.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na ujumbe kutoka jimbo la Shandong lililopo mjini Beijing nchini China waliotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Prof. Janabi alisema Tanzania ni nchi kubwa na ina idadi kubwa ya watu hivyo basi ili huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi ni lazima wawafuate katika Hospitali za Kanda.
“Lengo letu la baadaye ni kuhakikisha huduma tunayoitoa katika Taasisi yetu inawafikia wananchi wengi zaidi wenye matatizo ya moyo walioko mikoani pia kutoa mafunzo kwa madaktari walioko katika hospitali za Kanda kwa kufanya hivyo tutasaidia wagonjwa wa moyo kupata matibabu kwa wakati”, alisema Prof. Janabi.
Aidha Prof. Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 idadi ya wagonjwa wa moyo wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi imeweza kupungua kutoka wagonjwa 159 kwa mwaka 2012 hadi kufikia wagonjwa wawili kwa mwaka 2017.
Prof. Janabi alimalizia kwa kuzitaja changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hii ni kutokana na idadi ya wagonjwa kuongezeka kutoka wagonjwa 100 kwa mwaka 2016 hadi kufikia wagonjwa 300 kwa mwaka 2018 .
Aliomba Taasisi ipatiwe nafasi za mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wafanyakazi wake pamoja na kuongezewa idadi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini China ambao Serikali ya nchi hiyo inawatuma kufanya kazi katika Hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo JKCI.
Kwa upande wake Gavana wa Jimbo la Shandong Yu Xiao – ming aliipongeza Taasisi hiyo kwa huduma bora ya matibabu ya moyo wanayoitoa kwa wananchi na kuahidi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya njema ya moyo.
Yu Xiao - ming alisema magonjwa ya moyo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza lakini yanawasumbua watu wengi ila kama yataweza kudhibitiwa mapema kwa watu kupewa elimu na kufanya upimaji wa afya zao mara kwa mara itasaidia wananchi kutoyapata magonjwa hayo kirahisi.
“Hivi karibuni jimbo letu limesaini mkataba wa kushirikiana na Taasisi hii, nitakahikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa wakati hii ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuongeza idadi ya madaktari wa China kuja kufanya kazi hapa na kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wafanyakazi wa Taasii hii”, alisema Yu Xiao - ming.
Mwezi wa nane mwaka huu Taasisi hiyo ilisaini mkataba wa kushirikiana na jimbo la Shandong na Hospitali ya magonjwa ya Moyo ya Fuwai iliyopo mjini Beijing nchini China wa kutolewa kwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wafanyakazi na kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo ambazo zitasaidia kuwajengea uwezo wataalam wa afya.
No comments:
Post a Comment