ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 26, 2018

Vigogo Chadema, CUF watoa siri ya hamahama Bara

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji
By Waitara Meng’anyi na Noor Shija, Mwananchi wmeng’anyi@mwananchi.co.tz

Rorya/Zanzibar. Watendaji wakuu wa vyama vikubwa vya upinzani, Chadema na CUF wametoa siri ya sababu za wabunge na madiwani kuvikimbia vyama hivyo.

Watendaji hao, makatibu wakuu, Dk Vincent Mashinji (Chadema) na Maalim Seif Sharif Hamad (CUF), kwa nyakati tofauti walitoa siri hiyo walipokuwa wakizungumzia wimbi la hamahama ya wabunge, madiwani na viongozi wa ngazi za chini wa vyama hivyo.

Hadi sasa CUF imekimbiwa na wabunge wawili kutoka majimbo ya Kinondoni (Dar es Salaam) na Liwale (Lindi), Chadema wabunge saba wa Ukonga (Dar es Salaam), Monduli (Arusha), Serengeti (Mara), Ukerewe (Mwanza), Siha (Kilimanjaro), Babati Mjini na Simanjiro yote ya Manyara.

Akizungumza katika mkutano wa ndani wa viongozi wa Chadema Wilaya ya Rorya uliofanyika katika mji mdogo wa Shirati, Dk Mashinji alisema licha ya kukimbiwa na wabunge hao waliotimkia CCM, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kiko madhubuti na kitaendelea kuwa imara kutokana na nguvu ya wanachama na wananchi wanaokiunga mkono.

Dk Mashinji alisema wabunge wanne kati ya saba wa Chadema waliotimkia CCM hawakupikwa wala kulelewa kisiasa na chama hicho cha upinzani, bali walikuwa viongozi na makada wa CCM waliohamia upinzani.

“Yawezekana wamekamilisha walichotumwa Chadema ndiyo maana wanarejea walikotoka. Lakini msitishike maana tuko na tunaendelea imara kuliko tulivyokuwa awali,” alisema.

Alisema James ole Millya (Simanjiro), Dk Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga) na Joseph Mkundi (Ukerewe) walikuwa makada wa CCM.

“Hawa wote walikuwa makada na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM kabla ya kukimbilia Chadema tulikowaamini na kuwapa dhamana ya uongozi,” alisema Dk Mashinji.

“Wabunge waliohama waliolelewa, kukuzwa na kupikwa na Chadema ni Paulina Gekul (Babati Mjini) na Marwa Ryoba wa Serengeti. Wengine wote walihamia Chadema wakitokea CCM, yawezekana wamemaliza kazi yao iliyowaleta.”

Aliwataka viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho kutokatishwa tamaa na hali hiyo badala yake, wawe imara kukipigania na kukijenga chama hicho.

“CCM haiwezi kukabiliana kisiasa na Chadema na hii inadhihirisha nguvu na uwezo wa Chadema kisiasa. Msitishike wala kuvunjika mioyo kwa changamoto tunayoyapitia hivi sasa kwa sababu hakuna mafanikio bila kukabiliana na kuzishinda changamoto,” alisema Dk Mashinji.

Alitumia mifano ya Biblia kuwataka wajumbe wa kikao hicho alichosema kinalenga kuiimarisha Chadema kuendelea na mapambano bila kugeuka nyuma, wasije kugeuka nguzo ya chumvi kama ilivyokuwa kwa mke wa Luti.

“Mbegu haiwezi kuota bila kwanza kupandwa na kufa. Lengo la wote ndani ya Chadema ni kutatua matatizo yaliyopo na kusonga mbele tukiwa imara zaidi,” alisema.

Maalim Seif aguswa

Wakati Dk mahinji akisema hayo, mwenzake Maalim Seif alionyesha kuguswa na wimbi la wabunge na viongozi wa upinzani upande wa Tanzania Bara kuhamia CCM akisema hiyo inaonyesha ukosefu wa upinzani wa kweli kutoka moyoni.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Maalim Seif huku akionyesha kuguswa na wimbi la wabunge na viongozi wa vyama vya upinzani Tanzania Bara kuhamia CCM, alisema katika medani ya siasa, kuna tofauti kati ya Zanzibar na Tanzania Bara kwa kuwa wanasiasa wa Zanzibar wamejengwa zaidi kiitikadi katika vyama vyao tofauti na wale wa Bara.

Maalim Seif alisema anaamini wimbi hilo la hamahama linaweza kuendeleza zaidi Tanzania Bara huku viongozi hao wakisahau ahadi na majukumu waliokabidhiwa na wananchi wao.

Alisema ni vigumu kwa mwanasiasa yeyote au mwanachama aliyeshibishwa itikadi halisi ya chama chake kuyumba na kuja na hoja za kuunga mkono jitihada za Rais.

Heche ataja nguzo tatu

Awali, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche alitaja nguzo muhimu katika ujenzi wa chama kuwa ni umoja, ushirikiano na kujitolea kwa hali na mali bila kuogopa vitisho wala kununulika kwa fedha wala ahadi za vyeo.

“Tunalenga kuimarisha chama kwa kutatua na kumaliza changamoto zote ili kufikia lengo la kushika dola tukiwa imara kisiasa na kimfumo,” alisema Heche.

Mbali ya Heche, Kiongozi wa Oparesheni za Chadema Kanda ya Serengeti, Benson Kigaila aliwakumbusha wananchi wa Rorya kuwa jimbo hilo liliwahi kuongozwa na mbunge kutoka chama cha upinzani aliyeshinda uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, lakini likarejea CCM kutokana na wanachama kutoimarisha chama chao.

Mwaka 1995, Mabere Marando alishinda kiti hicho kupitia NCCR-Mageuzi akichuana na mbunge wa muda mrefu na machachari enzi hizo Edward Oyombe Ayila (marehemu).

“Rorya ni waanzilishi wa kuunga upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995; lazima mrejeshe heshima hiyo katika chaguzi zijazo na hilo haliwezi kufanikiwa bila kwanza kujiimarisha ndani ya chama na ndio maana tumeanzisha operesheni ya Chadema msingi,” alisema Kigaila.

Chadema msingi

Operesheni ya Chadema ni Msingi inayoendelea hivi sasa nchini mkakati wa chama hicho wa kujiimarisha katika ngazi ya chini kabisa ya uongozi wa chama hicho. Kwa vijijini ni vitongoji na mjini ni mitaa.

No comments: