Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge,Vijana na Ajira Antony Mavunde akijibu swali la Mbunge wa Temeke Abdallah Mtolea kuhusu kusitishwa kwa mbio za mwenge wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 13 wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma leo.
By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz
Dodoma. Sakata la Mwenge wa Uhuru kutakiwa usitishe mbio zake au uendelee bado limeendelea kuibuka bungeni lakini Serikali imeendelea na msimamo wake lazima mwenge uendelee kukimbizwa.
Leo Jumanne Novemba 6, 2018, mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea ameuliza kama Serikali haioni kukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa sasa hakuna umuhimu tena kwani umekuwa ukisababisha mambo mengi ikiwemo magonjwa ya zinaa ikiwamo HIV.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na Ajira na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde amesema mwenge bado una umuhimu mkubwa kwani unahamasisha masuala ya amani, haki, utu, muungano na hivyo kauli utaacha kukimbizwa itakuwa ni ngumu.
"Hivyo, Serikali inaona ni muhimu kuendelea na utaratibu wa kukimbizwa Mwenge wa Uhuru nchi nzima kila mwaka ili uendelee kufanya kazi ya kuimarisha misingi ya Taifa letu na kuhamasisha maendeleo ya wananchi," amesema Mavunde.
Naibu Waziri huyo amesema Mwenge wa Uhuru ulianza kukimbizwa mwaka 1964 mara baada ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar na muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo, Spika Job Ndugai amemkatisha Mtolea kuuliza swali la nyongeza akisema halikuwa linaendana na swali la msingi baada ya mbunge huyo kueleza hamasa ya mwenge imebaki kwa madiwani na wanafunzi huku ukisababisha maambukizi ya Ukimwi.
No comments:
Post a Comment