ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 7, 2018

Mgombea urais upinzani pasua kichwa 2020

Mwaka 2015, wapinzani walipata mgombea urais katika dakika za mwisho baada ya jina la aliyekuwa akipewa nafasi kubwa kupeperusha bendera ya CCM, Edward Lowassa kukatwa na chama hicho.

Ilikuwa kama dodo lililodondoka chini ya mchongoma, lakini kwa wachache ikawa kero; Dk Wilbrod Slaa, aliyegombea kwa tiketi ya Chadema mwaka 2010 na Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alikuwa akigombea kwa tiketi ya CUF, wakajiengua kwenye vyama vyao.

Lakini nguvu ya Lowassa ikawa kubwa zaidi kwa upinzani ambao ulishajipanga kwa kuunganisha nguvu ya vyama vinne; Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Nguvu yake ilidhihirika katika matokeo ya urais. Lowassa, ambaye alipewa fursa hiyo na Chadema, akashika nafasi ya pili, lakini si kama ile iliyowahi kushikwa na Augustine Mrema (NCCR mwaka 1995), Lipumba (CUF, 1995, 2000, 2005, 2010) na Dk Slaa (Chadema, 2010).

Lowassa alipata karibu mara tatu ya kura ambazo wagombea waliopita wa upinzani walikuwa wanapata. Alipata kura milioni 6.07, akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, John Magufuli. Idadi hiyo ni rekodi kwa upinzani tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992.

Wagombea wa vyama vingine; ACT-Wazalendo, UPDP, TLP, NRA, Chauma na NDC hawakuweza kufikisha hata asilimia mbili ya kura zote, wakiwaacha Magufuli (asilimia 58) na Lowassa (39.97) wakitamba.

Kabla ya uchaguzi huo wa mwaka 2015, kulikuwa na matarajio kuwa Dk Slaa na Profesa Lipumba wangesimamishwa na vyama vyao kugombea tena urais hadi suala la Lowassa lililopoibuka wakati wagombea wakijiandaa kuchukua fomu.

Lakini sasa ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, si Lowassa au mwanachama mwingine yeyote anayeonekana kuwa na nguvu za kupambana na Rais Magufuli, ambaye kwa utamaduni wa CCM ni dhahiri kuwa atapewa nafasi nyingine amalizie kipindi chake cha miaka 10.

Ukimya katika upande huo unatokana na mazingira ya kisiasa yanayosababisha vyama kuzuiwa kufanya mikutano ambayo ingeweza kuonyesha wanachama wanaochomoza na hivyo kufikiriwa kuwa ndio wanaoweza kupewa nafasi.

Hali hiyo inawafanya wachambuzi wa mambo ya kisiasa, kuwatazama wagombea wa upinzani wa miaka iliyopita kuwa ndio wenye uwezekano wa kuteuliwa kupeperusha bendera zao.

Hata muungano wa upinzani, maarufu kwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliomwezesha Lowassa kutingisha siasa za uchaguzi, unaelezwa na wachambuzi hao kuwa hauna nguvu hiyo tena. CUF, ambayo ilikuwa mshirika muhimu Ukawa kutokana na nguvu yake Zanzibar, imekumbwa na mgogoro wa muda mrefu uliosababisha kuwa na makundi mawili; la kwanza likimuunga mkono katibu wake mkuu, Maalim Seif Hamad Sharif na jingine likiwa chini ya Profesa Lipumba ambaye hakuna shaka atapewa tena nafasi ya kugombea urais.

Soma Zaidi:

Maswali tata, majibu tata ya Profesa Lipumba

Mambo 5 Maalim Seif anatakiwa kuyafanya ili kumnusuru kisiasa

Lakini wachambuzi hao wanatoa tena nafasi kwa mawaziri wakuu wa zamani waliohamia upinzani, Lowassa na Frederick Sumaye, aliyekuwa kivutio kwenye kampeni za Ukawa, kupewa bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Wawili hao walitoka CCM katika kipindi cha uchaguzi wa 2015 na kusababisha mtikisiko mkubwa na wamekuwa msaada mkubwa kwa Chadema.

Mwanasiasa mwingine anayetajwa kuwa ni miongoni mwa wanaoweza kuwania nafasi hiyo ya juu nchini, ni mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji akiendelea kuuguza majeraha baada ya kushambuliwa kwa risasi nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana.

Vilevile, wapo wanasiasa kama mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye amewahi kuwania nafasi hiyo mwaka 2005. Lakini si wote wanaompa nafasi Mbowe, ambaye anasifika kutokana na kuijenga Chadema hadi ikawa chama kikuu cha upinzani, kutokana na utamaduni wa chama hicho kutompa mgombea nafasi nyingine.

Mbowe ni kiongozi wa Kambi Upinzani Bungeni (KUB), wadhifa ambao hutazamwa kama wa ‘marais wanaosubiri kuingia Ikulu”.

Mjadala wa wanasiasa wa wapinzani wanaoweza kuteuliwa kupeperusha bendera ya kambi hiyo 2020 ni mkubwa na unaonyesha suala hilo ni pasua kichwa, hasa kutoka Chadema na wengine wakimtazama Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo.

Wachambuzi wa siasa za Tanzania wanaona uwezekano wa Chadema kupata mgombea nje ya chama hicho, hasa CCM kama ilivyofanya kwa Lowassa mwaka 2015. Hapo ndipo jina la Lazaro Nyalandu linajitokeza.

Huyu ni kada wa Chadema aliyehamia kutoka CCM na kupoteza ubunge wake wa Singida Kaskazini Oktoba mwaka jana na hajajitokeza kuwania nafasi nyingine katika chama chake kipya. Mwaka 2015 akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alikuwa miongoni mwa watia nia 42 waliojitokeza ndani ya CCM.

Soma Zaidi:

Upinzani unavyoyumba baada ya kuisha uchaguzi

Kwa mujibu wa ibara ya 7 (7)(16) ya katiba ya Chadema, moja ya kazi za Kamati Kuu ni kufanya utafiti wa wagombea urais na mgombea mwenza na kuwasilisha ripoti yake Baraza Kuu, ambalo hupendekeza majina kwa mkutano mkuu ambao una mamlaka ya kuwateua.

Kupitia utaratibu huu vilevile, si rahisi kwa makada wanaotaka kuwania nafasi hiyo ‘kujipitishapitisha’ au kutangaza nia ya kuwania kwa kuwa kazi ya kuwatafiti hufanywa na Kamati Kuu.

Kwa mazingira hayo na matokeo ya chaguzi ndogo zinazoendelea, baadhi ya wananchi wanadhani upinzani umekwisha na hawaoni mtu ambaye ataweka ushindani mkali kwa mgombea wa CCM.

“Nikiangalia kwa haraka sioni ambaye amejitosheleza kumtikisa mgombea wa CCM kwa sababu hatuwaoni majukwaani,” anasema Amon Kisimba, mfanyabiashara, mkazi wa Tabata.

Lakini Omary Mustapha kutoka Mbezi, anaona Lowassa bado anafaa kupeperusha bendera ya upinzani kwa sababu ana wafuasi wengi.

“Nyota yake bado inang’aa, Watu wanampenda na akiongea jambo anakuwa na mawazo mazuri,” anasema.

Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Filbert Rwegasira anatofautiana na maoni hayo ya wananchi.

Yeye anaona upinzani umekosa umoja ambao ungewapa nguvu za kushindana na CCM na anaona njia pekee ni kuungana kuwa chama kimoja.

“Tuliona kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 baadhi ya vyama vya upinzani vilipokubaliana kumuunga mkono mgombea mmoja, vilipata kura nyingi za urais na idadi ya wabunge ikaongezeka,” anasema mwanazuoni huyo.

Dk Rwegasira anadhani Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki ndiye anayefaa kutokana na uwezo wake wa kujieleza, kuchambua mambo na kutetea anachokiamini.

“Pamoja na kwamba amejeruhiwa, nadhani bado ana mvuto wa kugombea nafasi ya urais upande wa upinzani. Ni mtu ambaye akiwa anazungumza utapenda kumsikiliza na anakuwa na hoja,” anasema.

Hata hivyo, anaonya kwamba bila muungano baina yao, mgombea wa upinzani hawezi kushinda katika uchaguzi kwa sababu kura zao zitagawanyika na kuipa ushindi CCM.

Kwa upande wake, Profesa Gaudence Mpangala kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) pamoja na kuangalia zaidi mambo ya kisheria na kimfumo kuwa ndio kikwazo cha upinzani, anamuona Lissu kama chaguo zuri kwa wapinzani.

“Suala la nani atagombea mwaka 2020 ni gumu, lakini tuwaachie wenyewe tuone. Binafsi nadhani Lissu anaweza kuwa kivutio kikubwa kwenye uchaguzi ujao,” anasema.

Profesa Mpangala anamtaja pia Lowassa kuwa bado ana nguvu kwenye medani za siasa za Tanzania.

Anasema mbali na mapungufu madogomadogo ya kibinadamu, bado anafaa kuwa kiongozi wa nchi hii.

Akizungumzia suala hilo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana alisema uchaguzi wa mwaka 2020 utakuwa wa kawaida sana na hautakuwa na ushindani mkali kama uliopita.

Alisema kwenye uchaguzi huo, watu wenye umri mkubwa zaidi ya miaka 65 hawatakuwa na nafasi, badala yake nafasi kubwa itatolewa kwa vijana wenye uwezo na ushawishi mkubwa kama Lissu na Zitto Kabwe.

“Chance (nafasi) ya mtu kama Lowassa na Sumaye kugombea uchaguzi ujao ni ndogo. Nafasi ya Mbowe pia ni finyu, kwanza alishawahi kugombea huko nyuma. Wanatakiwa vijana wenye ushawishi,” anasema Dk Bana.

“Usishangae Lissu akaja kugombea urais. Yupo pia Zitto Kabwe. Ni vijana ambao wana uzoefu na siasa, hata wasipogombea wao wataibuka vijana wengine kama wao ambao watapewa nafasi hiyo. Muda wa miaka miwili iliyobaki kufika 2020 bado ni mrefu,” anasema.

Dk Bana alibainisha kwamba uchaguzi ambao kiongozi wa nchi anatetea nafasi yake huwa ni mgumu kwa wapinzani, hata hivyo anauona uchaguzi huo kwamba hautakuwa na msisimko mkubwa kama uliopita.

Anasema bado wapinzani wana nafasi ya kujipanga upya na kuandaa mazingira kulingana na mahitaji ya wakati. “Ana uwezo wa kujenga hoja na kuitetea kwa nguvu zote.”

Soma Zaidi:

Lowassa: Nitagombea tena urais mwaka 2020

Lipumba: Lowassa alikuwa mzigo mzito kumnadi

Lowassa: Njia ya Ikulu 2020 nyeupe


No comments: