Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa dini kuhubiri amani, upendo na mshikamano kwa watanzania ili kusaidia Taifa kusonga mbele kimaendeleo.
Akizungumza leo Mjini Bagamoyo mkoani Pwani, katika misa maalum ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 ya kanisa Katoliki nchini Tanzania, Rais Magufuli alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi hao wa dini kuhubiri upendo na amani kwa watanzania wa dini na makabila yote.
“Nataka muhubirie watanzania kuhusu upendo, amani na mshikamano, kwa vile naamini kuwa itasaidia kuondokana na matendo maovu na kwa njia hiyo tutaweza kulipeleka Taifa mahali pazuri”, alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alitolea mfano matendo maovu yanayotakiwa kukemewa na viongozi wa dini na ambayo jamii inatakiwa kuyaepuka kuwa ni rushwa, wizi na vitendo vya ubakaji.
Aidha, Rais Magufuli amelipongeza kanisa Katoliki nchini Tanzania kwa kuweza kufikisha miaka150 ya uinjilisti na kwa kubeba jukumu kubwa la kuisaidia jamii katika kutoa huduma za elimu na afya.
“Kazi nyingine kubwa iliyofanywa na kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka 150 ni kutoa huduma katika vituo 777 vya elimu, ikiwa shule za awali 228, shule za msingi 262, shule za sekondari 173 shule za ufundi 110 na vyuo vikuu 4, pamoja na vituo vya afya zaidi ya 100 vilivyopo nchini nzima”, alisema Rais Magufuli
Sambamba na hilo, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini zote, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zainazowakabili viongozi hao wa dini.
Aidha, Askofu wa Jimbo la Mpanda na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Gervas John Nyaisonga, alimpongeza Rais Magufuli kwa kutimiza miaka mitatu tangu kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuongeza kuwa amedhihirisha kwa vitendo kuwa anapenda viwango, nidhamu katika kazi na ulipaji kodi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni, aliwashukuru viongozi wa Serikali na kanisa kwa kupata heshima ya kuwakilisha nchi yake katika maadhimisho hayo muhimu.
Naye, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dkt. Detlef Waechter, alisema kuwa kanisa Katoliki nchini Tanzania limeendelea kukua na Serikali ya Ujerumani itaendeleza urafiki na ushirikiano uliokuwepo kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuendelea kusaidia jamii katika masuala ya elimu na afya.
Mnamo mwezi Machi mwaka 1868 wamishionari waliingia Bagamoyo mkoani Pwani, kwa lengo la kueneza injili ya kanisa Katoliki ambapo baadaye injili hiyo ilienea katika nchi mbalimbali ikiwemo Uganda, Kenya na Malawi.
Sikukuu ya maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilisti ya kanisa Katoliki imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanisa kutoka ndani na nje ya nchi, viongozi wa wastaafu wa Serikali, watendaji wa Serikali, pamoja na maelfu ya waumini wa kanisa Katoliki nchini.
mwisho
No comments:
Post a Comment