Na. Immaculate Makilika - MAELEZO
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, imefanya jitihada kadhaa ikiwa ni sambamba na kutekeleza sera mbalimbali ambazo zimeiwezesha nchi ya Tanzania kupata mafaniko makubwa ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miaka mitatu
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, ametaja mambo 10 muhimu yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitatu na ambayo yameitangaza nchi ya Tanzania kimataifa.
Dkt. Abbasi alitaja mambo hayo kuwa ni uchumi unaoendelea kukua kwa kasi nzuri, ambapo katika mwaka 2017/18 uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 7.1 na kuongoza katika nchi zote za Afrika Mashariki, huku ukiingia katika rekodi ya kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani kama ambavyo ripoti mbalimbali za kimataifa zimeeleza.
“Uchumi wetu ni wa tisa kwa ukuaji wa kasi duniani na katika Afrika, Kusini mwa Sahara ni wanne, hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya World Economic Forum ya mwezi Machi, 2018 na kwa nchi za Afrika Mashariki uchumi wa Tanzania unaongoza kwa ukuaji” alisema Dkt. Abbasi
Kuongezeka kwa mapato ya Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Magufuli amethubutu kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza kasi ya kukusanya kodi na hivyo kuongeza mapato ya kodi ya Serikali kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi.
Kufufuliwa kwa mashirika ya umma, Dkt. Abbasi alisema kuwa kutokana na ufuatiliaji, ubunifu, uwekezaji wa Serikali ya Rais Magufuli, mashirika mengi mfano Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamkala ya Maji Safi (DAWASA) na Bandari sasa yameanza kuamka kuwa na ufanisi, kuongeza mapato na mengine kutengeneza faida.
“Baadaa ya Serikali kuchagiza mageuzi ya kiutendaji sasa kwa mwaka TTCL inakusanya shilingi bilioni 212 kutoka shilingi bilioni 102, Bandari imekusanya kutoka shilingi bilioni 703 hadi kufikia shilingi bilioni 838 kwa mwaka, TRC kutoka shilingi bilioni 23 hadi 36 kwa mwaka na DAWASA shilingi bilioni 32.4 hadi shilingi bilioni 122.4 kwa mwaka “ alisema Dkt. Abbasi
Aidha, Dkt. Abbasi alisema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu Serikali ya Rais Magufuli imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya viwanda ambapo jumla ya viwanda 3,306 viliandikishwa, na vingine vinaendelea kujengwa na baadhi vimekamilika. Halikadhalika viwanda hivyo vimeanza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambapo kati ya hivyo viwanda 251 ni vikubwa na vya kati ni 173.
Ambapo mchango wa ekta ya viwanda katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi 5.5 mwaka 2017. Kasi ya ukuaji wa Sekta ya Viwanda ilikua kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 7.1 mwaka 2017/18.
Akiendelea kufafanua mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano Dkt. Abbasi alisema kuwa Rais Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi kwa pamoja na mambo mengine, sambamba na kutimiza ahadi yake ya kuunda Makosa ya Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi
“Mpaka sasa kesi mpya 41 zimefunguliwa, na kuna maombi ya dhamana 346 yamewasilishwa katika Mahakama hii kati ya mwaka 2017 na 2018” alisema Msemaji huyo wa Serikali.
Katika sekta ya usafirishaji nako, Serikali ya Rais Magufuli imefanya mageuzi kadhaa, yaliyopelekea sekta hiyo kupata mafaniko ya kuwa na ndege nne mpya zinazoendelea kuleta mageuzi katika usafiri wa anga nchini, abiria wanaotumia ndege za ATCL wameongezeka kutoka takribani abiria 4,000 kwa mwezi hadi abiria 30,000 kwa mwezi.
Aliongeza kuwa ndege mbili aina ya Air Bus zenye uwezo wa kubeba abiria watu 132 zitawasili nchini Disemba mwaka huu, na ndege aina ya Boeing dreamliner ya pili inatarajiwa kuwasili nchini Oktoba mwaka mwakani.
Aidha, mradi wa umeme wa Stigler’s gorge utakapokamiika unatarajiwa kuzalisha megawati 2,100, sambamba na mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha standarg gauge kutoka Dar es salaam hadi Morogoro na baade Dodoma, ambapo umefikia 33% ya ujenzi.
Mafaniko mengine ya Serikali hii yanaonekana katika katika sekta ya afya, ikiwemo kujenga vituo vya Afya vya Kata 210 na kukarabati vingine vingi kufikisha idadi ya vituo vinavyotoa huduma hadi mwaka huu kuwa 7,746 kutoka vituo 7,014 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 10.4.
Dkt. Abbasi alifafanua kuwa vituo hivi pia vina wodi za kina mama na vifaa vya kisasa. Aidha, ajira zaidi ya 6,000 za kada ya afya zimetolewa. Katika miaka mitatu Zahanati zimeongezeka kutoka 6,143 mwaka 2015 hadi 6,646 mwaka huu ikiwa ni sawa na ongezeko la zahanati 503 ambapo baadhi zilijengwa na zingine kukarabatiwa sawa na ongezeko la asilimia 8.1.
Vilevile, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mageuzi ya kiutendaji ikiwemo kuongeza Bajeti ya Dawa na Vifaa Tiba kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 270 kwa mwaka huu wa fedha.
Ongezeko hilo limewezesha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kufikia asilimia 89.6 kutoka asilimia 36 mwaka 2015/16. Aidha upatikanaji wa dawa muhimu umepanda kutoka wastani wa asilimia 35 tu hadi asilimia 93.
Sekta ya madini nayo, Dkt. Abbasi alisema kuwa “Serikali iliweka lengo la kukusanya shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka kutoka kwa wachimbaji wadogo wa Tanzanite pale Mirerani. Hata hivyo kabla hata ya nusu ya mwaka huu wa bajeti kufika, tayari mapato eneo la Tanzanite yamefikia shilingi milioni 788.5 sawa na asilimia 52 ya lengo la mwaka 2018/19, hii inashadidisha kuwa uamuzi wa Mhe. Rais kujenga ukuta ulikuwa makini” alisema Dkt. Abbasi
Katika miaka hii mitatu licha ya matukio ya hapa na pale, Tanzania imeendelea, kusimama kama moja ya visiwa vya amani duniani na Taifa limeendelee kushikamana kawa kuishi kwa amani na upendo.
Aidha, Dkt, Abbasi alisema kuwa Rais Magufuli anasimamia misingi na Watanzania leo wako huru kuamua mambo yao kama Taifa, huku akisisitiza kuwa safari ya kujitegemea imeanza na mataifa mbalimbali duniani yanafahamu azma ya Rais Magufuli kwa Taifa lake.
mwisho
No comments:
Post a Comment