ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 1, 2018

TRAFIKI WAOMBA RUSHWA WASHTAKIWA KWA WAZIRI MKUU

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa CCM  Sabasaba uliopo Lushoto, Oktoba 31, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wananchi wa Lushoto wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa  hadhara kwenye uwanja wa CCM Sabasaba akiwa  katika ziara ya mkoa wa Tanga Oktoba 31, 2018.


*Waziri Mkuu akabidhi majina hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa hatua

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela orodha ya matrafiki wanaodaiwa kuwaomba rushwa madereva wa noah wilayani Lushoto.

Majina ya trafiki hao wanadaiwa kuomba rushwa kwa madereva wa noah wanaofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya wilaya hiyo yaliwasilishwa kwa Waziri Mkuu kupitia mabango.

Waziri Mkuu alimkabidhi majina hayo jana jioni (Jumatano, Oktoba 31, 2018) baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Sabasaba, Lushoto mjini.

Baada ya kumkabidhi majina hayo alimuagiza afanye uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili askari hao na kisha awasilishe taarifa kwake leo Alhamisi Novemba 1, 2018.

Mbali ya wananchi kuwasilisha malalamiko hayo, Pia mbunge wa Lushoto, Shaaban Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua kero hiyo inayowakabili wananchi.

Awali, Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto katika ukumbi wa chuo cha Mahakama Lushoto ambapo aliwasisitiza wafanye kazi kwa bidii.

Alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haina msamaha na mtumishi wa umma asiyetaka kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi.

Alisema watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuwahudumia wananchi kwa kutumia taaluma zao.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Tanga alisema Serikali haina msamaha na mtumishi asietaka kubadilika na kufanya kazi.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma wahakikishe fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka Wakuu wa Idara kutumia kitabu cha ilani ya uchaguzi cha CCM cha mwaka 2015/2020 kwa sababu kina maelekezo wanayopaswa kuyatekeleza.

“Kitabu kile kina maelezo ya msingi yaliyotolewa na Rais. Dkt. Magufuli ambayo yanatakiwa yapewe kipaumbele cha utekelezwaji, wakuu wa Idara ni muhimu musome na kutekeleza.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa wilaya wahakikishe wanasimamia utekelezwaji wa maelekezo yote yaliyoainishwa kwenye kitabu cha Ilani katika maeneo yao.

Kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na kwamba suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba na kuwapongeza wakazi hao kwa kutunza misitu.

Alisema maeneo mengi nchini wananchi wamekata miti na kusababisha kukauka kwa vyanzo vya maji, ambapo ni tofauti na wilaya ya Lushoto ambayo bado ina misitu minene.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wote wa vijiji na kata waainishe sehemu  zote zenye misitu na vyanzo vya maji katika maeneo yao na wahakikishe wanayalinda.

Alisema mtu yeyote atakayebainika kuharibu mazingira hayo iwe kwa kuchoma au kukata miti achukulie hatua kali. “Ni marufuku mtu yeyote kukata miti bila kibali cha Serikali.”

Nae, Mbunge wa Lushoto Shekilindi alimuomba Waziri Mkuu awasaidie katika kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa katika jimbo hilo ikiwemo ya afya.

Mbunge alisema kwa sasa hospitali ya wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu wa mashine ya xrey, hivyo kusababisha wananchi kusafiri hadi Korogwe au Tanga kufuata huduama hiyo.

Waziri Mkuu alisema tayari ameshamuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kupeleka mashine ya x-rey katika hospitali hiyo.

No comments: