Advertisements

Wednesday, November 14, 2018

WAKURUGENZI WATAKIWA KUZINGATIA AFUA ZA LISHE KATIKA BAJETI ZA HALMASHAURI KUKABILIANA NA UDUMAVU KWA WATOTO

 Mkurugenzi Msaidizi Sera, kutoka Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Bw.Eleuter Kihwele  akizungumza na baadhi ya viongozi  na Wataalam Lishe wa mkoa wa Simiyu, katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe Mkoani Simiyu kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018.
 Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Bi. Mariam Nakuwa   akiwasilisha mada kuhusu mipango na bajeti ya masuala ya lishe Mkoani Simiyu kwa baadhi ya viongozi  na Wataalam Lishe wa mkoa wa Simiyu, katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akisisitiza jambo katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe Mkoani Simiyu kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018.
 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Kai.B. Mbaruk akizungumza na baadhi ya viongozi  na Wataalam Lishe wa mkoa wa Simiyu, katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe Mkoani Simiyu kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018 wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu.
 Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani akichangia hoja katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe Mkoani Simiyu kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018 wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu.
 Diwani wa Kata ya Dutwa  Mhe.Mapolu Nunde Mkingwa akichangia hoja katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe Mkoani Simiyu kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018, ambapo alimwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe.Richard Buyamba.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt.Seif Shekalaghe akichangia hoja katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe kwa mwaka 2019/2020 Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Kuelekea katika kipindi cha maandalizi ya  bajeti ya mwaka 2019/2020 wito umetolewa kwa  Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Simiyu na maeneo mengine kote nchini kuyapa kipaumbele masuala ya Lishe katika mipango na bajeti za Halmashauri zao, ili kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Sera, kutoka Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Bw.Eleuter Kihwele wakati mafunzo maalum yaliyotolewa kwa baadhi ya viongozi na maafisa Lishe, katika kikao cha Maandalizi ya Mipango ya Bajeti ya Afua za Lishe Mkoani Simiyu kwa mwaka 2019/2020 kilichofanyika Mjini Bariadi, Novemba 12, 2018.

Kihwele amesema takribani asilimia 34 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchi nzima wana udumavu, hivyo ipo haja ya kutilia mkazo suala la lishe ili kutoathiri maendeleo ya ukuaji wa watoto, uwezo wao wa kufikiri na maendeleo yao kitaaluma(shuleni).

“Asilimia 34 ya watoto wa  nchi nzima wenye umri chini ya miaka mitano wana utapiamlo, suala hili linaathiri sana watoto, mfano matokeo yao shuleni na uwezo wa kufikiri, ndio maana serikali imeweka lishe kama kipaumbele na Ofisi ya Rais TAMISEMI kama wasimamizi tunapita kwenye Halmashauri nchi nzima kuhamasisha uzingatiaji wa masuala ya lishe katika bajeti ya mwaka 2019/2020” alisema

Ameongeza kuwa katika mafunzo yanayotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Viongozi pia yamelenga  kuwakumbusha juu ya utekelezaji wa vipengele vya mikataba ya afua za lishe iliyosainiwa katia ya  Wakuu wa Mikoa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI na kutenga shilingi 1000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano katika bajeti zao.

Naye Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi. Mariam Nakuwa ametoa wito  kwa Halmashauri kutenga  fedha kwa ajili ya masuala ya lishe kwa kuzingatia miongozo na kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika katika shughuli zilizopangwa ili kuondokana na tatizo la utapiamlo

Aidha, Bi. Mariam amesema pamoja na kukabiliana na tatizo la utapiamlo fedha hizo zielekezwe katika huduma za utoaji wa virutubisho vya nyongeza kama vile virutubisho vya Vitamini A na vidonge vya kuongeza wekundu wa damu kwa akina mama wajawazito.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Jumanne Sagini aliwasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Simiyu kuyachukulia masuala ya lishe kama kipaumbele, huku akiwataka kuhakikisha wanafanya vikao vya kamati za lishe za wilaya kila baada ya miezi mitatu kama ilivyoanishwa  katika miongozo.

Diwani wa Kata ya Dutwa  Mhe.Mapolu Mkingwa akizungumza kwa niaba ya  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe.Richard Buyamba amesema maelekezo na mafunzo waliyoyapata watayapelekea katika Mabaraza ya madiwani na kuhakikisha mipango na bajeti zinazopitishwa zinazingatia umuhimu wa afua za lishe.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe amesisitiza viongozi na watendaji wakiwemo wajumbe wa kamati za lishe kubadilika na kuachana na mazoea katika kufanya ufuatiliaji na kutekeleza mipango ya masuala ya lishe badala yake wafanye kazi kulingana na miongozo ili kuwa na matokeo mazuri katika masuala ya lishe.

Timu ya Wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ipo katika ziara ya kuhamasisha Viongozi katika Halmshauri na Mikoa kuzingatia vipaumbele kwenye maeneo ya lishe na kupanga mipango ya bajeti inayojibu changamoto za lishe, ili kufikia malengo ya  mikataba ambayo Wakuu wa Mikoa walisaini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye usimamizi wa afua za lishe katika maeneo yao.

No comments: