Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Sara Cooke masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Uingereza na Tanzania. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi ya Waziri Lugola, jijini Dodoma leo.
Balozi wa Uingereza nchini, Sara Cooke (kushoto) akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kuhusiana na masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi ya Waziri Lugola, jijini Dodoma leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akimkaribisha ofisini kwake jijini Dodoma, Balozi wa Uingereza nchini, Sara Cooke kwa ajili ya mazungumzo ya kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini, Sara Cooke na kumuakikishia ushirikiano zaidi kati ya Wizara yake na Ubalozi huo nchini.
Mazungumzo hayo ya zaidi ya saa moja yalifanyika ofisini kwa Waziri Lugola, jijini Dodoma leo ambayo yalijadili masuala mbalimbali ikiwemo uimarishaji wa ushirikiano kati ya Wizara na ofisi ya Balozi huyo nchini.
Waziri Lugola alimuakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama kwa kuwa Wizara yake imejipanga vizuri kuendelea kuwalinda raia na mali zao pamoja na wageni wote waishio nchini.
“Mheshimiwa Balozi nashukuru sana kwa kunitembelea, najisikia furaha kwa ujio wako na karibu sana wakati wowote, Wizara yangu pamoja na nchi yangu kwa ujumla tutaendelea kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali,” alisema Lugola.
Hata hivyo, Balozi Sara alimpongeza Waziri Lugola kwa kuteuliwa na Rais John Magufuli kuiongoza Wizara hiyo na pia alimuakikishia ushirikiano zaidi kati ya Uingereza na Tanzania.
“Hongera sana mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani na pia nimefurahi kuja katika ofisini yako kufanya mazungumzo nawe,” alisema Balozi Sara.
No comments:
Post a Comment