Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ameweka wazi jinsi alivyokuwa akiumizwa na kauli za upinzani dhidi ya uongozi wake.
Akifungua Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Dodoma jana, Pinda alisema kuna kipindi wakati wa uongozi wake, wapinzani walikuwa wakiinyooshea kidole Serikali yao kuwa ni dhaifu haina makali, hivyo walikuwa wanataka kiongozi mkali na mwenye uamuzi mgumu.
Alisema alikuwa haipendi kauli hiyo na ilikuwa ikimkera kwa sababu ilimlenga na yeye, lakini akasema sasa anashangaa kuona wapinzani haohao wameanza kulalamika tena juu ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli ambaye ndiye kiongozi wa aina waliyekuwa wakitamani kumpata.
Pinda aliteuliwa kuwa waziri mkuu na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete baada ya Edward Lowassa kujiuzulu.
Mwaka 2015, alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kugombea urais lakini jina lake liliondolewa katika hatua za awali.
Jana, mstaafu huyo alitumia jukwaa la UVCCM kutoa yaliyo moyoni mwake ikiwa ni miaka mitatu ya tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015.
Alisema Rais Magufuli ndiye kiongozi ambaye Watanzania walikuwa wanamhitaji kutokana na uthubutu alionao katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Wakati ule kauli hii ilikuwa inaniudhi kwa sababu ilikuwa inanilenga mimi lakini sasa hivi tena ambapo Mungu amesikia kilio chao na kuwapa JPM wameanza kulalamika tena, ni jambo la kushangaza,” alisema Pinda.
“Wakati fulani kuna baadhi ya watu huwa wananiuliza, hivi mzee na wewe si ulikuwa unautaka urais, nawajibu tu aka huyuhuyu ndiye anayefaa, mimi ni miongoni mwa watu wanaomkubali sana Magufuli.”
Alisema Rais Magufuli ametekeleza miradi iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambayo serikali nyingine zilishindwa kuitekeleza kwa kisingizio cha kuogopa gharama kubwa.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge na serikali kuhamia Dodoma.
Alisema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ulikuwa mgumu kutekelezeka kutokana na kuangalia gharama hasa kutokamilika kwa miundombinu ya aina mbalimbali.
“Siyo kwamba tulikuwa hatujui kama tunatakiwa kuhamia Dodoma, ila utekelezaji wake ndiyo uliokuwa mgumu kwa sababu kila ukitaka kuhamia unakuta hakuna maji, barabara bado hazijajengwa na miundombinu mingine, kwa hiyo unajikuta unaendelea tu kusubiri mpaka muda wako unaisha bila mafanikio,” alisema.
Alisema hata siku Rais Magufuli alipotangaza kwamba Serikali inahamia Dodoma, wengi hawakuamini kwa sababu jambo hilo lilikuwa halijatengewa bajeti na wala vikao vya chama vilikuwa havijalipitisha.
“Kama Magufuli angesikiliza maneno ya watu, miradi mingi pamoja na ununuzi wa ndege isingewezekana,” alisema.
Akizungumzia suala la watumishi hewa, Pinda alisema hata katika uongozi wao liliwatesa hadi wakafikia uamuzi wa kuanza kuwalipa mishahara dirishani.
Awali, akizungumzia utendaji kazi wa UVCCM, mwenyekiti wa umoja huo Mkoa wa Dodoma, BillChidabwa alisema wameanza mchakato wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wote mkoani Dodoma kwa kushirikiana na Sido pamoja TRA.
No comments:
Post a Comment