ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 4, 2018

WANANCHI WA LINDI, PWANI KUPATA MAWASILIANO YA UHAKIKA

 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Chihuta, Mtama mkoani Lindi kuhusu upatikanaji wa huduma za mawasiliano wakati wa ziara yake mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (alyeinua mikono) akijadiliana na Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Sara Chiwamba kuhusu upatikanaji wa mawasiliano kwenye kata ya Marui wakati wa ziara yake Wilayani humo ya kukagua ukosefu wa mawasiliano. Wa kwanza kulia mwenye kofia nyeupe ni Mbunge wa jimbo hilo Zuberi Kuchauka.
 Wananchi wa kijiji cha Chihuta, Mtama mkoani Lindi wakimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) namna wanavyotega mawasiliano kwenye simu zao wakati wa ziara yake ya kukagua changamoto za mawasiliano mkoani humo.
Wananchi wa kijiji cha Marui, Wilaya ya Liwale mkoani Lindi wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano mkoani humo.


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amewahakikishia wananchi wa baadhi ya vijiji ambavyo havina mawasiliano mkoani Lindi na Pwani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli inahakikisha kuwa wananchi waishio kwenye vijiji hivyo wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika

Nditiye ameyasema hayo akiwa kwenye ziara yake ya kukagua changamoto za hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo ya Liwale, Lindi Vijijini, Mtama, Kibiti na Rufiji kwenye mkoa wa Lindi na Pwani baada ya kupata kilio kutoka kwa wabunge wanaowakilisha wanananchi wa maeneo hayo wakati wa kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania cha mwezi Novemba mwaka huu

Amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni sekta inayoshika nafasi ya pili kwa kuchangia pato la taifa katika kipindi cha mwaka 2016/2107 kwa kiwango cha asilimia 13.1 ambapo mawasiliano yana changui kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu na mawasiliano ndiyo kila kitu. “Wananchi mkiwasiliana kwa kununua vocha, kupiga simu na kutumia intaneti, Serikali inatoza kodi kidogo, ambayo wala haiumizi na wala mwananchi hausikii, lakini Serikali inapata mapato yake,” amesema Nditiye.

Amefafanua kuwa ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano ambapo  hadi sasa asilimia 94 ya wananchi wote wanawasiliana kwa kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unatoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili ziweze kupeleka huduma za mawasiliano kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.

Mkuu wa Wilaya ya Liwale Sara Chiwamba amemshukuru Nditiye kwa ziara yake Liwale na kufika Mirui kuzungumza na wananchi ambao wana kiu ya kupata mawasiliano. “Tuna imani mawasiliano yatapatikana kwa kuwa mawasiliano yanasaidia ulinzi na usalama na Wilaya yetu itaenda kufunguka,” amesema Chiwamba.

Naye Mbunge wa Liwale Zuberi Kuchauka amemweleza Nditiye kuwa mradi huu wa mawasiliano kwenye kata ya Mirui ni miongoni mwa miradi sita inayotekelezwa na UCSAF na ni matumaini kuwa hadi Januari 2019, Mirui watakuwa wameunganishwa na dunia kupitia mawasiliano. Pia ameongeza kuwa anamshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kujipambanua kuwa ni Rais wa Serikali ya wanyonge, “kweli tunaona anawatetea wanyonge na anatembea kwenye kauli yake, tunashukuru amewakomboa wakulima wa korosho,” amesisitiza Kuchauka.

Vile vile, Mkuu wa Wilaya la Lindi Shaibu Ndemanga amemshukuru Nditiye kwa kufika na kufanya mkutano na wananchi wa kijiji cha Chihuta kilichopo Mtama, Lindi kwa kuwa wamekosa mawasiliano kwa muda mrefu angali wana uchumi mzuri wa korosho. Nditiye amesema kuwa, “nitafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Chihuta mnapata mawasiliano kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni maendeleo,”.  Nditiye ameilekeza UCSAF ifike Chihuta ndani ya mwezi mmoja ifanye utafiti na kujenga mnara wa mawasiliano. Pia ameongeza kuwa kwenye jimbo la Mtama ipo miradi nane ya mawasiliano na miradi mingine sita inaongezwa na mwezi Machi mwakani na zabuni nyingine itatangazwa na UCSAF ili kampuni za simu ziweze kuomba kwa lengo la kujenga minara ya kufikisha huduma za mawasiliano ili wananchi wawasiliane.

Pia ametembelea na kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na changamoto zilizopo kwa wananchi katika maeneo ya  Mbuchi na Mchukwi Wilayani Kibiti ambapo amebaini uwepo wa ukosefu wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi waishio maeneo hayo na wanaofika kupata huduma kwenye hospitali ya Mchukwi ambapo amebaini kuwa Kampuni ya Halotel ilifika na kufanya tathmini ya kujenga minara kwenye baadhi ya maeneo hayo ambapo imechukua muda bila kurejea na kukamilisha kazi hiyo. 
Nditiye ameielekeza UCSAF iwasilishe ofisini kwake ndani ya wiki moja orodha ya minara inayoendelea kujengwa, ambayo imesimama kujengwa kwa kipindi cha miezi sita hadi sasa na ambayo haijaanza kujengwa. Pia, UCSAF ihakikishe kampuni za simu zinaongeza nguvu ya mawasiliano kwenye minara ya maeneo ya Mchukwi ili wananchi waweze kupata mawasiliano ya uhakika nyakati zote 
Naye Mbunge wa Kibiti Ali Seif Ngando amemhakikishia Nditiye kuwa mnara ukikamilika watautunza kwa kuwa utawasaidia wananchi kupata masoko ya bidhaa na fursa mbali mbali. Pia, Mkuu wa Wilaya hiyo Gullam-Hussein Shaban Kifu amemuomba Nditiye awasaidie ili kampuni ya Vodacom iweze kufika kwenye Hospitali ya Mchukwi ili waongeze nguvu ya mawasiliano ya mnara wao ili wananchi, wagonjwa na wataalam wa tiba wanaotoka nje ya nchi kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwenye hospitali hiyo waweze kupata mawasiliano na huduma za intaneti

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF Mhandisi John Mukondya amekiri uwepo wa ukosefu na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye maeneo hayo na amepokea maelekezo ya Nditiye ili kuhakikisha kuwa wanafika maeneo hayo kwa kushirikiana na kampuni za simu kufanya utafiti ili kujenga minara ya kuwawezesha wananchi kuwasiliana

No comments: