Advertisements

Thursday, January 17, 2019

MAJALIWA AKAGUA UJENZI WA MJI WA SERIKALI ENEO LA IHUMWA DODOMA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Jengo la Wizara ya Maji wakati alipokagua ujenzi wa Mji wa Serikali  katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Januari 17, 2019.  Wanne kulia ni Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Watano kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde na wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Januari 17, 2019. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua  ujenzi wa Jengo la Ofisi ya  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati alipotembelea Ujenzi wa Mji wa Serikali kwenye eneo la Ihumwa jijini Dodoma Januari 17, 2019. Watano kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo na watatu kulia ni Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua Ujenzi wa Mji wa Serikali kwenye eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Januari 17, 2019. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa jengo la Ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali unaojengwa eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Januari 17, 2019. Wapili kulia ni  Waziri wa Elimu, Sayansi ya Tekinolojia, William Ole Nasha na kushoto ni Katibu  wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuratibu Mpango  wa Serikali  wa Kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,  akizungumza na Saidi Kiwape (kushoto) ambaye ni fundi wa kusuka nondo wakati alipokagua ujenzi wa Jengo la Ofisi za Wizara ya Nishati kwenye eneo la Ihumwa unapojengwa  Mji wa Serikali jijini Dodoma, Januri 17, 2019. Wapili kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, watatu kulia ni Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujezi wa tangi la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni moja za maji  kwa ajili ya kuhudumia Mji wa Serikali unaojengwa katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Januari 19, 2019.  Katikati ni Katibu wa Kikosi Kazi  cha kitaifa cha Kuratibu  Mpango wa Serikali wa Kuhamia Dodoma, Meshck Bandawe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 KASI YA UJENZI MJI WA SERIKALI INARIDHISHA - WAZIRI MKUU

*Ataka kampuni ya Mzinga Holdings isimamiwe kwa karibu
*Ahimiza tarehe ya mwisho ni Januari 31, mwaka huu
ZIKIWA zimepita siku 20 tangu akague ujenzi wa mji wa Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na ujenzi unaoendelea katika eneo la Mji wa Serikali lililoko Ihumwa.

Hata hivyo, amesema kampuni ya ujenzi ya Mzinga Holdings inahitaji kusimamiwa kwa karibu zaidi ili ikamilishe ujenzi wa majengo yake kabla ya Januari 31, mwaka huu. “Nitakuja kukagua kazi na kupokea funguo za ofisi siku hiyo,” amesema.

Ametoa kauli hizo leo mchana (Alhamisi, Januari 16, 2019) mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ambaye alianza kukagua ujenzi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, ametembelea majengo ya wizara zote na kubaini bado kuna changamoto zinazojitokeza kutokana na utendaji wa mazoea miongoni mwa watumishi wa Serikali.

Akiwa katika jengo la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri Mkuu alipokea malalamiko kutoka kwa meneja mradi, Bi. Selemina Rwehumbiza kwamba aliandaa certificate tangu tarehe 13 Januari lakini hadi sasa hajapata malipo. Alipofuatilia, alijibiwa na mshauri mwelekezi kwamba wamepokea certificate hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 16, 2019).

“Kama kazi hii muhimu ya Mheshimiwa Rais, na anayesimamia ni Waziri Mkuu inacheleweshwa hivi, je akija mwananchi wa kawaida huko ofisini kwenu atachukua muda gani kupatiwa huduma?,” Waziri Mkuu alimhoji Mshauri Mwelekezi wa mradi huo kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Mhandisi Hilary Msaki.

“Huu ni mfano halisi wa malalamiko yanayotoka huko nje kwamba Serikali haijibu barua za wananchi. Sasa nyaraka kutoka hapa Mtumba inachukua wiki nzima kwenda mjini, na mtu bado hajajibiwa. Sielewi ni kwa nini barua iende hadi mjini, wakati wakandarasi wako huku. Kwa nini ninyi msipokee hizo nyaraka na kuzikimbiza mjini kisha mrudishe majibu hapa site?”, alihoji Waziri Mkuu.

“Kuanzia sasa, kazi zote mpokee ninyi, na ninyi ndiyo mzipeleke huko mjini na kurudi na majibu hapa site kwa wateja wenu, kwani wakandarasi wote wako hapa,” alisisitiza.

Akiwa katika eneo la Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri Mkuu alielezwa na Waziri Ummy Mwalimu kwamba wana changamoto ya kutopatiwa taarifa za maendeleo ya mradi. “Tangu mradi unaze hatujapewa taarifa hata moja, wakurugenzi wapo wanakuja, lakini mshauri mwelekezi hatupi ripoti yoyote juu ya huu mradi,” alisema.

Alipohoji ni kwa nini taarifa hazitolewi, Waziri Mkuu alibaini kuwa hata watu wa TEMESA pia hawakuwepo kwenye zoezi hilo la ukaguzi. “Niliagiza TBA wahamie hapa, nao wameweka ofisi yao hapa hapa. Nimeulizia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wako wapi, nikaambiwa wako mjini. Ni kwa nini hawako hapa?” alihoji.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu alisema pamoja na spidi anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora unaotakiwa (quality).

Alisema kwa ujumla kazi nyingi zimeboreshwa tangu alipokagua mradi huo Desemba 27, mwaka jana. Aliitaka TBA kwa kushirikiana na Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa/Mkurugenzi wa Dodoma wawasimamie wakandarasi na hasa wale wa Mzinga ili kazi yao ikailike kwa wakati.

“Nimesisitiza katika kila site, zile kazi ndogondogo zisizohitaji ujuzi au ufundi mkubwa, zigawiwe kwa vijana ili kuongeza kasi lakini tuzingatie ubora wa kazi,” alisisitiza.

Desemba 27, mwaka jana, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali na kubaini kuwa baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi inayotarajiwa na Serikali. Siku iliyofuata aliitisha kikao cha Mawaziri wote, Makatibu Wakuu na wakandarasi wao ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini. Kikao hicho alikifanyia hukohuko Ihumwa.

No comments: