Aliyekuwa Mbunge na Naibu Waziri Mstaafu wa Tanzania, Mama Shamim Khan akitunukiwa Tuzo ya Juu (Pravasi Bharatiya Samman Award ) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind tarehe 23 Januari, 2019. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu wa Mauritania, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh nchini humo.
Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkubwa wa 15 wa Diaspora wa India uliofanyika katika mji wa Varanasi, Utter Pradesh, India
Picha ya pamoja
Mama Shamim Khan katika picha ya pamoja na Afisa Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Dkt. Kheri Goloka baada ya kupokea Tuzo tarehe 23 Januari, 2019.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Yah: Mama Shamim Khan atunukiwa tuzo ya juu ya heshima na Mhe. Ram Nath Kovind, Rais wa India
Mbunge wa zamani na aliyekuwa Naibu Waziri kwenye Wizara mbalimbali nchini, Mama Shamim Khan ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima (Pravasi Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, Mhe. Ram Nath Kovind. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa 15 wa Diaspora wa India (15th Pravasi Bharatiya Divas 2019) uliofanyika kwenye mji wa Varanasi, Uttar Pradesh tarehe 23 Januari, 2019.
Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi uliwahusisha viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya India akiwemo Waziri Mkuu wa Mauritania, Mhe. Pravid Kumar Jugnauth, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Sushma Swaraj, Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Mambo ya Nje ya India, Mhe. Gen [Dr.) V. K. Singh na Waziri Kiongozi wa Jimbo la Utter Pradesh, Mhe. Yogi Adityanath.
Mama Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii hususan katika masuala ya akina mama na kudumisha amani na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini.
Wakati akimtunuku tuzo hiyo, Rais Kovind alieleza kutambua mchango mkubwa wa Mama Shamim Khan katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na Serikali ya Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi zao. Aidha, alimpongeza kwa utumishi uliotukuka.
Kwa upande wake, Mama Shamim Khan alimshukuru sana Rais Kovind na kueleza kufarijika kwake kwa kutunukiwa Tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwake. Aidha, Mama Shamim Khan alipongeza juhudi za Serikali ya India kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na India na amemuomba Mhe. Rais Kovind kuendelea kusaidia juhudi za Serikali ya Mhe.Rais Dkt. John P. Magufuli katika kuwaletea maendeleo watanzania.
Tuzo hiyo hutolewa kwa raia wenye asili ya India ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mama Shamim Khan bali kwa Tanzania kwa ujumla. Mama Shamim Khan aliongozana na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dkt. Kheri Goloka kwenye hafla hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
24 Januari 2019
No comments:
Post a Comment