Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi ya Sekretarieti hiyo jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kushoto ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mst. Mhe. Harold Nsekela
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mst. Mhe. Harold Nsekela (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kuhusu majukumu ya ofisi yake wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, alipoitembelea ofisi hiyo kuhimiza uwajibikaji jijini Dodoma.
Baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao cha kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika katika ofisi ya Sekretarieti hiyo jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitia saini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma kwa ajili ya kuhimiza uwajibikaji.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA YATAKIWA KUWACHUKULIA HATUA KALI ZA KINIDHAMU VIONGOZI WANAOKIUKA KIAPO CHA MAADILI
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetakiwa kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi wanaokula Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu na kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni lakini wanashindwa kutekeleza kiapo hicho.Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, alipofanya ziara ya kikazi makao makuu ya ofisi hizo jijini Dodoma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu wake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, baadhi ya viongozi wamekuwa wakila Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu na kusoma Tamko la Rasilimali na Madeni lakini maisha na tabia zao ni tofauti kabisa na viapo wanavyoapa, hivyo ameisisitiza Sekretarieti ya Maadili kutumia sheria kuwawajibisha viongozi wa namna hiyo kwani ni mzigo kwa taifa.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema viapo na matamko ni lazima viendane na uhalisia, hivyo ameitaka Sekretarieti hiyo kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua bila uwoga wowote kwa kiongozi anayeenda kinyume kwani kiongozi wa namna hiyo anakosa sifa ya kuwa kiongozi bora.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema ni lazima kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na viongozi ambao hawana maadili mema ili kuleta maendeleo kwa taifa.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa Sekretarieti hiyo kuishi na kufanya kazi katika maadili mema ili wawe mfano kwa wanaowasimamia katika suala zima la maadili.
“Ni lazima maadili mema yaanzie kwetu sisi ili tunapozungumza na kutoa elimu ya maadili kwa viongozi tuwe kioo kwani huwezi ukazungumzia maadili kwa viongozi kama wewe mwenyewe huna maadili, hivyo ni lazima kuonyesha mfano,” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu, Mhe. Harold Nsekela amesema, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma yanazingatiwa ipasavyo.
Mhe. Nsekela ameyataja majukumu ya Sekretarieti kuwa ni pamoja na kupokea matamko ya viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni yanayopaswa kutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa na Sheria, kupokea na kushughulikia malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka kwa wananchi na kufanya uhakiki wa Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma wanaotajwa na Sheria.
Mhe. Nsekela ameyataja baadhi ya matarajio ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa ni kujenga na kuimarisha maadili ya kitaifa na kuyafanya yawe sehemu ya jamii ili kuzuia mmomonyoko wa maadili katika nchi kwa kujumuisha somo la maadili katika mitaala kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, kufanya marekebisho ya Sheria zinazohusu ukuzaji wa maadili nchini ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Kudhibiti Mgongano wa Maslahi.
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 23 JANUARI, 2019
No comments:
Post a Comment