ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 3, 2019

Dk. Mdede aahidi kuisapoti Nzihi Fc mabingwa wa Mkoa wa Iringa

Mdau wa Michezo  Dkt.Musa Mdede akiwa ameshika kombe la ushindi la timu ya Nzihi FC wakati wa tukio hilo la kuwapongeza.

 Na Andrew Chale.
Mdau wa Michezo na aliyekua mgombea Ubunge Jimbo la Kalenga Mwaka 2015, Dkt.Musa Mdede ameahidi kuisapoti timu ya soka ya  Nzihi mpaka kufika daraja la kwanza baada ya ubingwa wa kihistoria wa mkoa walioupata hivi karibuni.

Ameyasema hayo jana alipohudhuria sherehe ya kuipongeza timu ya Nzihi Fc iliyofanyika katika Ofisi za kijiji cha Nzihi iliyopo Wilaya ya Iringa Vijijini.

Katika sherehe hiyo Dk.Mdede alitoa kiasi cha fedha shilingi laki moja ( 100,000/-)  kama zawadi kwa ushindi walioupata vijana hao kama hamasa huku pia akiwahidi kuwasaidia kufikia malengo yao makubwa katika michezo.

Katika  mashindano ambayo Nzihi iliibuka mabingwa, yalishirikisha jumla ya timu 22 kutoka mkoa wote wa Iringa.

"Shabaha yetu ni kuona Nzihi Fc inafika daraja la kwanza.Tutaisapoti timu yetu kadri ya mahitaji yake, kwani Nzihi Fc ni fahari ya Kata yetu ya Nzihi, Jimbo letu la Kalenga na Mkoa wa Iringa kwa ujumla" Alisema Dk.Mdede.

Aidha Dk.Mdede ameahidi kutoa vifaa mbalimbali vya michezo kama mipira,fulana za mazoezi, koni kwa ajili ya mazoezi  na vitu vingine mbalimbali vya msaada wa timu hiyo.

Dk. Mdede amesema vifaa hivyo anatarajia kutoa kabla  ya kuanza kwa mashindano ya kanda ambayo Timu hiyo ya Nzihi Fc itashiriki kama mwakilishi wa mkoa wa Iringa.

Aidha, katika sherehe hiyo ilihudhuliwa na wananchi, wadau na Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesera ambaye akuwa mgeni rasmi, Diwani wa Kata ya Nzihi, Stephen Mhapa pamoja na viongozi wengine akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa vijijini.

Mdau wa Michezo  Dkt.Musa Mdede wa kwanza kushoto waliokaa akiwa pamoja na wachezaji  wa Nzihi FC wakati wa tukio hilo la kuwapongeza.

Mdau wa Michezo  Dkt.Musa Mdede wa akizungumza katika tukio hilo juu ya kuisaidia Nzihi FC wakati wa tukio hilo la kuwapongeza jana .
 

No comments: