ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 18, 2019

WADAU WATENGENEZA MKAKATI WA UTALII

Na Grace Semfuko-MAELEZO

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya kuboresha sera yake ya 2003 sasa imeingia katika hatua ya kuandaa mkakati wa utekelezaji wa muda mrefu wa Sekta hiyo na Mshauri Elekezi, Profesa Samwel Wangwe yuko na wadau wa utalii nchini, jijini Dar es Salaam katika kutengeneza Mkakati wa Muda Mrefu utakaotumika katika sekta ya Utalii, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika Sekta hiyo muhimu kwa pato la Taifa.

Wawakilishi wa Vyama 13 vinavyounda Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT) wamekutana katika Hotel ya New Africa kutoa mawazo yao na kubaini yapi yawe katika Mkakati, ambapo mwelekeo, mfumo na msukumo wamesema vitalenga katika masuala mbalimbali yakiwemo, kukuta uwelewa wa watu kuelewa dhana ya Utalii wa Tanzania, kuutangaza nje Utalii wa Tanzania pamoja na kuangalia ni kwa namna gani Taifa litanufaika na Utalii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilola Utalii nchini, Bw. Richard Rugimbana amesema kuwa maboresho ya Sera ya 2003 yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii ni mazuri na kukamilika kwa sera kunawusaidia wadau kusonga mbele kuboresha mifumo na miongozo ili hatimaye kuendesha sekta hiyo kwa ufanisi mkubwa.

“ Ni sera nzuri na iwapo tunayoyajadili yatafanyiwa kazi tutakuwa katika eneo zuri la utalii nchini Tanzania kwani sisi tunaongoza kwa kuwa na maeneo mengi na makubwa ya utalii katika nchi za Afrika na Duniani” alisema Rugimbana.

Naye Mshauri elekezi wa kazi hiyo Profesa Samuel Wangwe alisema Sekya ta Utalii inatoa zaidi ya asilimia 25 ya mapato yafedha za kigeni na hivyo kuimarishwa kwa Sera hiyo kutasaidia kuongeza pato hilo ambalo ukuaji wake utasaidia kuimarisha shughuli za kijamii nchini.

“Utalii wetu Tanzania kiuchumi unakua sana, kitendo cha Serikali kushirikisha sekta binafsi zinazounda Shirikisho la utalii kitasaidia sana katika kukuza uchumi huo kwani wao pia wanajiona kama sehemu ya utalii katika Taifa letu, asilimia 25 ya fedha za kigeni zinazoingia nchini kutokana na sekta ya utalii itaongezeka kutokana na kuimarishwa kwa Sera hii kiuchumi” alisema Profesa Wangwe Mshauri Elekezi


Mwezi Mei mwaka 2018, Waziri Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamis Kigwangala wakati akifungua kongamano la kupitia rasimu ya sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 linalofanyika jijini Dodoma na kuwashirikisha wadau wa sekta ya utalii nchini kutoka sekta binafsi na za umma alisema ukuaji wa sekta ya utalii Tanzania umeongezeka kutoka Dola bilioni 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola bilioni 2.2 mwaka 2017.

Alisema ongezeko la mapato hayo ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017 ambapo Sekta ya utalii inachangia takriban asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni (foreign exchange earnings).


Mwisho.



No comments: