Advertisements

Wednesday, March 27, 2019

Polisi wazuia mkutano wa ndani wa ACT-Wazalendo

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limezuia mkutano wa ndani wa chama cha ACT-Wazalendo uliokuwa ufanyike leo asubuhi katika ukumbi wa PR, Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema wameuzuia baada ya kufanya uchunguzi na kubaini viashiria vya kutokea vurugu katika mkutano huo.
Alipoulizwa kwanini polisi wasiimarishe ulinzi ili mkutano huo uweze kufanyika, Mambosasa amesema kutokana na polisi kuwa na shughuli nyingine hawawezi kufanya hivyo na kuwataka wahusika wasubiri mpaka hali itakapotulia.
“Mkutano wa ndani hauhitaji maombi ya kibali, ila shida kipindi hiki cha mpito hivi vyama vya ACT na CUF kumekuwa na uhasama wa chini kwa chini, tumepata taarifa watu wa CUF walikuwa wamejipanga kufanya vurugu pale.”
“Kwa kuwa sisi hatukuwa na zuio, tukaona hatuna sababu ya kuacha watu wakavurugana na kuumizana. Kuna sintofahamu tukaona si kipindi sahihi za kuacha huu mkutano ufanyike kwa sasa,” amesema.
Alipoulizwa lini ACT wataruhusiwa kuendelea na mkutano huo, Mambosasa amewataka wanachama wa vyama hivyo kuwa watulivu. “leo hawawezi kuendelea lakini hali ikitulia wanaweza kuendelea.”
Awali, katibu mwenezi wa chama cha ACT, Ado Shaibu amesema kuwa polisi wamezuia mkutano huo baada ya kufika eneo la tukio na kuwataka viongozi na wanachama wa chama wote kutawanyika.
Viongozi waliotarajiwa kushiriki mkutano huo ni kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, Maalim Seif Sharif Hamad, naibu kiongozi wa chama hicho, Duni Haji, mwenyekiti taifa, Yeremia Maganja, makamu mwenyekiti Bara, Shaaban Mambo, katibu mkuu, Dorothy Semu na naibu katibu mkuu, Msafiri Mtemelwa.

No comments: