Advertisements

Wednesday, March 20, 2019

PROF. KABUDI AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UAE NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi alipomtembelea katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Machi 2019. Mazungumzo hayo yalijikita katika kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kudumisha na kukuza uhusiano baina ya Tanzania na UAE. 
Waziri Mhe. Kabudi akimsikiliza Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Mhe.Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi walipokutana kwa Mazungumzo Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yakiendelea.
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Khalifa Abdulrahman Al-Marzooqi, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini. 

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika tarehe 20 Machi 2019 kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo Dar es Salaam, Prof. Kabudi alimshukuru Mhe. Balozi Al-Marzooqi kwa kupata fursa ya kukutana naye na kwamba, Tanzania inathamini mahusiano na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Aidha, alimweleza Balozi huyo kuwa, Wizara chini ya uongozi wake itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa, mahusiano yaliyopo kati ya nchi hizi mbili yanaimarishwa.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Al-Marzooqi ametumia mazungumzo hayo kumpongeza Mhe. Prof. Kabudi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumhakikishia ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha mahusiano yaliyopo yanaimarishwa.

Mhe. Balozi Al-Marzooqi aliongeza kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu una nia ya kuimarisha mahusiano yaliyopo na umepanga kufungua Ubalozi mdogo (Consulate General) Zanzibar. Pia, Mhe. Balozi alimuarifu Mhe. Waziri kwamba ana mpango wa kuutembelea Mkoa wa Dodoma ili pamoja na masuala mengine, kujionea eneo walilopewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za ubalozi na makazi kwa lengo la kujipanga kuliendeleza.

Kadhalika, Prof. Kabudi na Mhe. Balozi Al-Marzooqi wamekubaliana kuendeleza ushirikiano kwenye maeneo ya uwekezaji ambapo Balozi huyo ameonesha nia ya kuendelea kushawishi wawekezaji kutoka nchini kwake kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta za utalii, hoteli, viwanda na utoaji wa huduma. Pia ameahidi kuwashawishi wafanyabishara wakubwa na wadogo kutoka UAE kuja nchini ili kujionea fursa za biashara zilizopo.

Prof. Kabudi amemuhakikishia Balozi Al-Marzooqi kuwa, Tanzania ni eneo bora la uwekezaji na biashara na kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara zingine zitaendelea kuweka mazingira mazuri ya kupokea wawekezaji na wafanyabiashara kutoka maeneo yote duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
20 Machi 2019

No comments: