ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 30, 2019

Serikali yatenga fedha za ndani kupeleka umeme wa Gridi Katavi

 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makalla (wa kwanza kushoto) wakiwa katika Mkutano na wananchi wa Kijiji cha Kapalala (hawapo pichani) wakati walipofika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na Bi. Salma Karamba, mkazi wa Kijiji cha Ifukutwa wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi ambaye ameunganisha umeme kwenye nyumba yake kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata utepe kuashiria kuwashwa rasmi kwa umeme katika Kijiji cha Ifukutwa wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ( wa pili kushoto) akikagua mitambo ya umeme wa mafuta katika kituo cha kuzalisha umeme cha Mpanda wilayani Katavi. Kituo hicho kinazalisha umeme wa kiasi cha megawati 3.5.

Na Teresia Mhagama, Katavi
Imeelezwa kuwa, Serikali imetenga fedha za ndani, kiasi cha Dola za Marekani milioni 70 kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 kutoka Tabora hadi Katavi ambayo itawezesha Mkoa wa Katavi kuunganishwa na gridi ya Taifa.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani mkoani Katavi wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya umeme katika Wilaya ya Mpanda, Nsimbo na Tanganyika ambapo aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makalla.

“Serikali imeamua kujenga mradi huu ili Mkoa wa Katavi uachane na kutumia umeme wa mafuta ambao ni ghali kwani shilingi milioni 21 zinatumika kila wiki kuendesha mitambo hii, hivyo gharama za uendeshaji zinakuwa kubwa tofauti na mapato yanayoingia.” Alisema Dkt. Kalemani.

Alieleza kuwa, njia hiyo ya umeme ya kV 132 itakuwa na urefu wa kilometa 284 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020 kwani taratibu za ujenzi zimeshaanza.

Akiwa katika kituo cha kuzalisha umeme cha Mpanda, Dkt Kalemani alisema kuwa, mwaka jana kituo hicho kilikuwa na mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2.6 lakini mwaka huu imeongezwa mashine ya tatu na kufanya kituo hicho kuwa na uwezo wa megawati 3.75, hivyo kukidhi mahitaji ya umeme ya Mkoa wa Katavi kwa sasa.

Aidha, Dkt Kalemani aliwapongeza wafanyakazi wa TANESCO katika Kituo hicho kwa kutumia shilingi milioni 100 tu kwa kazi ya uboreshaji wa kituo pamoja na uhamishaji wa mashine hiyo ya tatu ya kufua umeme ambayo ilikuwa wilayani Loliondo.

“ Nataka niwapongeze watumishi hawa wa TANESCO kwani Mkandarasi kutoka Uholanzi alisema kuwa gharama atakayotumia kwa ajili ya kazi hiyo ya uhamishaji wa mashine ni shilingi bilioni mbili lakini niliagiza wataalam wetu kuwa tuihamishe wenyewe na wametumia shilingi milioni 100 tu.” Alisema Dkt Kalemani.

Katika ziara yake wilayani Nsimbo, Waziri wa Nishati alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Kapalala ambapo pia aliwasha umeme katika Kijiji hicho na kumuagiza mkandarasi kampuni ya CRCC kupeleka umeme katika vitongoji vyote vya Kijiji hicho.

Vilevile, katika ziara yake wilayani Tanganyika, Dkt Kalemani alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Mchakamchaka na Ifukutwa na kuwasha rasmi umeme katika Vijiji hivyo.

No comments: