Advertisements

Friday, May 17, 2019

Samatta achukua ubingwa Ubelgiji, sherehe kuanza leo

By Eliya Solomon, Mwananchi

Dar es Salaam. Hatimaye KRC Genk, anayoichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ wametangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji ambayo ni maarufu kama Jupiler Pro.

KRC Genk wametangazwa kuwa mabingwa wapya wa Jupiler Pro baada ya kutoka sare ugenini ya bao 1-1 na Anderlecht huku wapinzani wao, Club Brugge wakipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Standard Liège.

Matokeo hayo yanamaana kwamba chama la Samatta pamoja na kuwa wamesaliwa na mchezo mmoja kwenye Ligi ndogo yaani Play Off kabla ya msimu huu wa 2018/19 kumalizika, wamefikisha idadi ya pointi ambazo hakuna timu inayoweza kuzifikia.

Sare ya bao 1-1 ambayo Genk wametoka usiku wa jana, wamefikisha jumla ya pointi 51 huku wapinzani wao, Club Brugge wakisaliwa na alama zao, 47 kwenye nafasi ya pili.

Sherehe za kuusheherekea ubingwa huo kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo ni kwamba, zitaanza leo, Ijumaa kwa kuzunguka mji wao wa Genk, wakiwa kwenye basi maalumu ambao litakuwa wazi.

Hivyo mashabiki wa wadau mbalimbali wa KRC Genk watapata nafasi ya kuwaona nyota wao, akiwemo Samatta ambao wameifanya timu hiyo kutwaa ubingwa wa nne tangu kuanzishwa kwake, 1988.

No comments: