ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 12, 2019

MKUTANO WA SADC NGAZI ZA MAWAZIRI KUENDELEA KESHO HUKU PROF. PALAMAGAMBA AKIKAGUA PIKIPIKI ZA KUONGOZA MISAFARA YA VIONGOZ

Mkutano wa Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unatarajiwa kuanza kufanyika jumanne ya August 12,2019 ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi anatarajiwa kukabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa ngazi za Mawaziri.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa pikipiki mpya zinazotarajiwa kutumiwa katika mapokezi ya viongozi na wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa SADC unaoendelea Jijini Dar Es Salaam,waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema serikali imekuwa ikiendelea na maandalizi mbalimbali ya mapokezi ya viongozi hao ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri ikiwemo magari na pikipiki achilia mbali hotel watakazofikia viongozi hao.

Aidha Prof. Kabudi kwa niaba ya serikali,ameeleza kuridhishwa na kufurahishwa kwa namna vyombo vya habari Nchini vinavyoripoti kizalendo Mkutano unaoendelea wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) jambo ambalo limeongeza uelewa wa wananchi kuhusu SADC na kuvitaka kuendelea kufanya hivyo katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya nchi.

Katika tukio jingine Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Denmark Nchini Tanzania Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet.

Katika mazungumzo yao Prof. kabudi amemkaribisha Balozi huyo mteule nchini na kumhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini huku Balozi Mteule Mette Norgaard Dissing-Spandet akiipongeza serikali kwa mageuzi ya haraka inayoyafanya ili kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na kuongeza uwajibikaji serikalini.

No comments: