WAJUMBE wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) wametapa nafasi ya kutembelea viwanda 21vinavyofanya uzalishaji kwa ajili ya kuangalia ubora wa bidhaa na mazingira ya uzalishaji kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Wakiwa katika viwanda hivyo wajumbe hao wamekiri na kuridhishwa na ambavyo Serikali ya Tanzania namna ilivyodhamiria katika Uwekezaji katika viwanda huku wakieleza wazi Tanzania wanayo nafasi kubwa ya kumiliki soko la Jumuiya hiyo kwani kuna kila.kitu zikiwemo malighafi za uhakika.
Mjumbe kutoka nchini Afrika Kusini wa Kampuni ya Flexion Renatus Joseph amesema kwamba yeye yupo katika sekta ya viwanda vya chuma jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kwamba aliyoyashuhudia katika kiwanda cha Lodha Group of Companies yamenifanya abadili fikra zake kuhusu uwezo wa viwanda kwa nchi ya Tanzania.
Amesema amethibitisha kwa macho yake kuna matumizi makubwa ya teknolojia katika utengenezaji bidhaa za nondo na vifaa vingine vitokanavyo na chuma. “Hakika vikipatikana viwanda vingi vya namna hii SADC tutapiga hatua na tutakuwa na bidhaa zinazoleta ushindani ndani na nje ya Afrika,” amesema.
Wajumbe hao wakiwa kiwandani hapo yameelezwa kiwanda hicho cha chuma kilichopo Mkuranga mkoani Pwani ni miongoni mwa viwanda vilivyoitikia mwito wa Rais Dk. John Magufuli kwa vitendo kuhusu Tanzania ya viwanda.
Akizungumza mbele ya ujumbe wa SADC waliotembelea kiwandani hapo Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhandisi Kamara Gombe amesema Tanzania kwa sasa inazalisha tani 200,000 za bidhaa za viwanda huku mahitaji ni tani 300,000.
“Hii maana yake kuna uhaba wa tani laki moja kwenye soko. Hivyo, Kampuni ya Lodhia ni miongoni mwa wadau wa viwanda wanaohakikisha Tanzania inajitegemea katika sekta ya viwanda.Hata hivyo, mbali ya uhitaji huo wa tani laki moja bado kuna tatizo la uhaba wa soko kwa kuwa wanazalisha tani 3000 kwa mwezi
“Lakini uwezo wao ni kuzalisha tani 10,000. Kazi yetu viwanda ni kulinda viwanda vya ndani, tutahakikisha tatizo hili tunalitafutia ufumbuzi ili hizi tani 7,000 zilizobaki ziweze kuzalishwa,” amesema Gombe.
Wakati Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Toni Filbert amesema wilaya hiyo pamoja na Mkoa wa Pwani kwa ujumla wanazo fursa nyingi za uwekezaji kutokana na ardhi kubwa yenye rutuba. Vilevile, kuna bidhaa nyingi za kimkakati zinazozalishwa na wazawa.
Akitoa maelezo kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Lodhia Group of Companies, Harminder Bhachu alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1996 wakiwa wanafanya biashara ya jumla ya kuuza vyuma ambapo mwaka 2004 ndio walianza kuzalisha vyuma katika kiwanda kilichopo mkoani Arusha.
“Vilevile tuligeukia bidhaa nyingine ikiwemo mabomba ya maji, Gypsum Board, mapipa ya kuhifadhia maji na bidhaa nyingine za ujenzi kwa kuhakikisha Tanzania inajitosheleza katika vifaa vya ujenzi bila kuagiza nje ya nchi,” amesema Bhachu na kufafanua wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuwahamasisha kuwekeza kwa nguvu na pia amesaidia kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa kila kampuni bila kupendelea.
Hata hivyo katika ziara hiyo, wajumbe wa SADC pia walipata fursa kutembelea kiwanda cha kusindika matunda cha Bakhresa Group of Companies kilichopo Mwandege Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Wajumbe walivutiwa na namna ya kipekee waliyoonyesha wafanyakazi wa kiwanda hicho katika usindikaji matunda, mitambo ya kisasa na usafi wa hali ya juu pia ulionyesha ni namna gani kampuni hiyo ilivyo tayari kuliteka soko la SADC.
Akielezea uwekezaji huo mkubwa uliogharimu Dola za Kimarekani Milioni 210, Mkurugenzi wa Mahusiano Bakhresa Group, Hussein Sufian alisema kampuni hiyo ina viwanda mbalimbali vipatavyo vinne ambavyo vinasindika bidhaa za chakula.
“Soko letu baada ya kujitosheleza ndani tulijipanua katika mataifa mbalimbali ya kiafrika, kwenye muktadha wa SADC tunafikisha bidhaa zetu katika nchi saba ukiondoa Tanzania, ambazo ni DRC, Angola, Comoro, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kuisini.
“Katika kuhakikisha tunakuza ajira na kuongeza tija katika uzalishaji, kwa asilimia kubwa malighafi zetu zinatoka Tanzania. Tuna ardhi kubwa inayotuwezesha kukusanya matunda kila kona ya nchi, tunayasindika na kuuza nje ya nchi kwa kiwango cha kutosha. Asilimia 15 ya bidhaa zetu tunazisafirisha nje ya Tanzania hasa hizi nchi za SADC,” ameeleza.
Akizungumza katika kiwanda hiki, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga amesema watahakikisha wanasimamia haki za msingi za kampuni hiyo kwa sababu imewapa heshima kubwa katika Mkoa wa Pwani kutokana na kupata ajira nyingi za vijana.
Pamoja na mambo mengine wajumbe wametembelea pia kiwanda cha kusindika korosho cha Biotan kilichopo wilayani Mkuranga ambapo Katika kiwanda hiko wajumbe walijionea hatua kwa hatua namna korosho zinavyopokewa kutoka kwa wakulima, zinavyopangwa kwa daraja, zinavyochemshwa kwa kutumia mvuke hadi hatua ya kuzibangua zikiwa tayari kwa kuwekwa kwenye mifuko.
Akizungumza kiwandani hapo Bahati Mayoma ambaye ni Mkurugenzi wa Biotan Group Limited amefafanua kampuni yao kwa kiasi kikubwa kinamilikiwa na raia kutoka Australia, ndiyo maana hata bidhaa zao zinazingatia viwango vya hali ya juu kwa kuwa wanazisafirisha katika nchi za Ulaya.
Ameongeza kuwa wanaliona soko la SADC muhimu kwao kwa kuwa kitu muhimu kinachotakiwa katika kulifikia soko hilo ni kuwa na bidhaa zenye ubora ambazo zinaandaliwa katika mazingira safi na salama kwa kutumia teknolijia za hali ya juu.
“Bidhaa zetu tunazipeleka Denmark, Sweden, Ujerumani, Australia na nchi nyingine nyingi za kiafrika. Lakini kwa sasa soko letu jipya tunaangalia hizi nchi za SADC,” amesema Mayoma.
Amesema kwamba kwa mwaka uwezo wao wa kuzalisha ni tani 1500 hadi 2000, lakini wanatarajia baada ya kuliteka soko la SADC ikifika mwaka 2021 uwezo wa uzalishaji utafikia tani 5000 kwa mwaka.
Kwa kukumbusha tu SADC ni jumuiya ya kimaendeleo ya kiuchumi inayohusisha nchi wanachama 16 ambazo ni Tanzania, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ushelisheli, Comoro, Botswana, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Afrika Kusini, Mauritius na Namibia. Kwa mwaka huu mkutano wa wakuu wa nchi wanachama utafanyika Tanzania kuanzia Agosti 17 hadi 18 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC). GPL
No comments:
Post a Comment