ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 10, 2019

AFISA TARAFA ITISO ATOA ONYO KWA WANANCHI WANAOHUJUMU MIUNDOMBINU YA MAJI


 Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akizungumza na wanachi wa Kijiji cha Chenene  wakati wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa kero za wananchi kijijini hicho kilichopo Tarafa ya Itiso
 Mkaguzi wa Polisi Tarafa ya Itiso Insp.Makweba Misana akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chenene wakati wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa kero za wananchi kijijini hicho kilichopo Tarafa ya Itiso
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Dodoma Dr.Godfrey Mbabaye akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chenene (Tarafa ya Itiso)  wakati wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa kero za wananchi kijijini hicho kilichopo Tarafa ya Itiso
 Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akiteta jambo na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Chamwino Mhandisi Christina Msengi  wakati wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa kero za wananchi kijijini Chenene kilichopo Tarafa ya Itiso
 
 Baadhi ya Wanachi walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Chenene ili kupata mrejesho wa utekelezaji wa kero za wananchi kijijini Chenene kilichopo Tarafa ya Itiso
 Afisa Tarafa itiso Remidius Emmanuel Akifafanua jambo katika kisima cha kijiji cha Haneti baada ya Meneja wa RUWASA Mkoa we Dodoma Dr.Godfrey Mbabaye  akiongozana na ujumbe wake kufika katika eneo la kisima.


AFISA Tarafa wa Itiso, wa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Remidius Emmanuel amewataka wananchi waishio katika Kijiji cha Chenene wilayani humo, kutunza miundombinu ya maji na kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi  pale wanapobaini wananchi wachache wanao hujumu miundombinu hiyo.


Remidius ameyasema hayo katika mkutano wa Wananchi wa Kijiji hicho walipokuwa wakitoa mrejesho wa utekelezaji wa kero za wananchi kijijini hapo. Pamoja na mambo mengine Mkutano huo pia ulilenga kuhamasisha wananchi hao kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha katika orodha ya Daftari la wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.


Pia mkutano huo ulilenga kutoa mrejesho wa hatua mbalimbali za utekelezaji na utatuzi wa kero zinazowakabili wanakijiji hicho.


Mapema Remidius amesema uwepo wa Meneja wa RUWASA mkoa wa Dodoma Dk. Godfrey Mbabaye, viongozi wenzake na wataalamu wengine kutoma RUWASA katika mkutano huo ni hatua muhimu ya kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, .Binilth Mahenge kuhakikisha mkanganyiko uliopo katika mradi wa maji kijijini hapo unatatuliwa.


Julai 9, .2019 Dk. mahenge akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Chamwino katika kata ya Haneti aliagiza uongozi wa RUWASA kufika kijijini hapo kusikiliza madai ya wananchi juu ya mfumo wa kisima cha maji ili watoe majibu na ufafanuzi wa kitaalam na kutatua kero zote zinazojitokeza katika mradi wa maji kijijini hapo.


Dk. mahenge alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mmoja wa wananchi waliohitaji kujua ni lini kero yao hiyo itapatiwa ufumbuzi.


Akizungumza baada ya kutembelea kisima cha maji kijijini hapo,Meneja wa RUWASA Mkoa wa Dodoma Dk. Godfrey amesema tatizo kubwa lililoleta mkanganyiko kwa wananchi hao ni kutokana na ukosefu wa taarifa za uhakika juu ya mradi huo hatua iliyoleta sintofahamu miongoni mwa wananchi hao.


" Hatuwezi kupuuza malalamiko ya wananchi hawa, wataalamu wetu watapiga kambi kupitia upya mfumo wa mashine na kisima chenu, tunasisitiza sana pale mnapobaini tatizo katika mradi huu hakikisheni mnatoa taarifa kwa wataalam wetu na kuepuka kutumia watu ambao hawana ujuzi na mifumo ya miundombinu ya visima vyenu. " Amesema Dk. Mbabaye.


Akifafanua juu ya dhana ya ongezeko la matumizi ya mafuta katika mashine ya maji amesema kufuatia mabadiliko ya mfumo wa pump unaoendeshwa na  mashine kwenda mfumo wa Umeme (Submersible Pump) mabadiliko hayo yanaendana na ongezeko la mafuta ingawa amesema kufuatia matarajio ya umeme katika Kijiji hicho kutasaidia kumaliza kabisa utumiaji wa mafuta.


"Viongozi hawa wanaposhindwa kutimiza wajibu wao na mimi kama kiongozi wa Tarafa ninakuwa sehemu ya tatizo, kwa hiyo niombe radhi kwa makosa yaliyofanywa na uongozi wa kijiji.Lakini naleta masikitiko yangu kwenu.


Kabla ya uongozi wa kijiji kusoma mapato na matumizi ya kijiji hicho, Diwani wa kata hiyo Mhe. Peter Chidawali amewahakikishia wananchi wa Chenene kwamba kero zote zote zinazokabili kijiji hicho tayari zimetatuliwa na nyingine zikiendelea katika hatua mbalimbali za utatuzi ikiwa ni pamoja na Malipo ya miezi tisa (9) mnara wa TTCL kwa kijiji hicho jambo ambalo lipo katika hatua za mwisho na hii ni baada ya kuwasiliana na Uongozi wa TTCL mkoa wa Dodoma,Alisema Chidawali.


Kwa upande wake Mkaguzi wa polisi wa Tarafa ya Itiso Insp.Makweba Misana amewataka wananchi hao kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za wahalifu na amesema watahakikisha wanawatia nguvuni wale wote walioshiriki kuhujumu miundombinu ya maji kijijini hapo.


Mbali na kijiji cha Chenene, ujumbe wa RUWASA ulitembelea kijiji cha Haneti na kufika katika Kisima cha maji baada ya kupokea taarifa za kuharibika kwa pampu ya maji iliyopelekea sehemu ya kijiji hicho kukosa maji.

No comments: