ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 9, 2019

Dela la kuazima Halichafuki

WANAKWAMBIA ndege wafananao huruka pamoja nashanga wee bundi sijui utaruka na nani? Hehe heeeiyaaaaaa! Shoga mji wa moto huu, unaweza kukoroga maji ya baridi ukajua ni chai! Acha nijimwayemwaye, wee shangaa kama mkulima wa vitunguu anayesubiri kuvuna nyanya, kutwa umbea umekujaa kama bomba la choo cha kupanga mana kutwa kufunguliwa na kufungwa! Haloooo eeeh!

Shoga leo nina furaha, siyo kila siku kuchamba siku moja moja kusifia! Kama umevaa vizuri nisiseme, kama umepatana na bwana wako na uliniomba ushauri nisiseme! Shuuuutuuuu! Leo nipo na wanaume ambao hawajui mwanamke anapenda nini, kutwa kushinda kazini akirudi usiku hata kile chakula ambacho anakuta kimeshafunuliwa anashindwa kukila, upo nyonyo?

Mwanaume akishaacha hela ya matumizi basi, anajua kila kitu kitajiendesha chenyewe; watoto wataenda shule, yeye akirudi kama siyo kufikia kwenye TV basi kwenye simu, anachati utadhani ameagizia gari Ulaya tena linakuja na begi la pesa ndani yake, hehee heeeiyaaaaa! Nicheke miye shoga mbavu zangu zipate kuishi!

Ngoja niwang’ate sikio tu wanaume wa namna hii! Sifuri nayo ni namba japo inasahaulika! Acha kuwa na akili ya mamba anaikimbia mvua nchi kavu anaingia mtoni! Mwanaume lazima ujue kutenga muda wa kukaa na mwenza wako! Hata mara moja au mbili kwa wiki, mtoe ‘out’ kwani sh. Ngapi? Hooovyoooo! Kama ulikuwa hujui jua sasa, dela la kuazima hata iweje halichafuki na likichafuka haliazimishwi hiloo, upo nyonyo? Hii ni sawa na mwanamke ukimtoa out hawezi kusahau hata mara moja, kwanza atakuthamini maradufu kuliko hata kumuachia vijihela vya matumizi!

Mwanamke anatakiwa kutunzwa, kupetiwa! Kubadilishiwa mazingira, leo umemtoa out siyo kula chakula cha mchana tu hadi chakula cha usiku, mkabadilisha na staili zenu zile, kwa nini lisikae akilini hilo? Kwa nini usimteke, hata ukichepuka kuna kitu kitampiga moyoni na kukusamehe! Wareeee reeeeeee!

Sasa wee zubaa kutwa mwanamke unamuweka ndani kama TV flatscreen inasubiri wageni uwawekee muvi, ukiwa mwenyewe unaangalia hadi katuni na taarifa ya habari! Shoga niishie hapa maana miye tena kwa kuanza kutapika kama dela na mtandio! Tukutane tena wiki ijayo shosti yangu. Ni mimi Shangingi Mstaafu ukipenda unaweza kuniita Anti Naa, Kungwi wa Makungwi GPL

No comments: