ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 9, 2019

KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Kingu asisitiza ufanisi na uwajibikaji wa viongozi wizarani

Na Mwandishi Wetu, MOHA
KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, ametoa wito kwa wakuu wa idara kwenye taasisi, vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo katika Wizara hiyo, kutelekeza wajibu walionao ili kuongeza uwajibikaji.
 
Meja Jenerali Kingu aliyasema hayo Mjini Dodoma jana alipofanya kikao cha pamoja na wakuu wa idara hizo.
 
Idara hizo ni Utawala, Wakimbizi, Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Huduma kwa Wakimbizi.
 
Kikao hicho kilijadili mchakato wa ajira kwa watumishi wa idara zilizopo chini ya Wizara hiyo, upandishaji vyeo, taratibu za uteuzi na nidhamu katika vyombo vya ulinzi na usalama.
 
“Naipongeza Wizara kwa kuandaa mkutano huu ili kujadili changamoto, mafanikio, idara ya utawala na rasilimali watu ina jukumu kubwa zikishughulika na watu, watumishi.
 
“Pia idara hizi ndio kiungo katika uratibu, uwezeshaji kwenye taasisi na vyombo vilivyopo chini ya Wizara ili kuleta mafanikio zaidi kama watatekeleza wajibu wao ipasavyo,” alifafanua.
 
Meja Jenerali Kingu alisema idara hizo zina jukumu kubwa la kuzishauri mamlaka ndani ya taasisi, vyombo husika kwani kukiwa na tatizo ina maana kuna mahali hakuko sawa.
 
Alisisitiza suala la kutolewa mafunzo ya kitaaluma kwa watumishi wote ambayo tatazingatia usawa.

“Suala la kuajiri watu kwa upendeleo lisipewe nafasi, tuajiri watumishi wenye sifa kwa manufaa ya taasisi,” alisisitiza.
 
Alizungumzia suala la wastaafu kucheleweshewa malipo yao akitaka wapunguziwe adha wanayoipata na kutaka yafanyike maandalizi mapema ili kuondoa kero, kasoro zilizopo na malalamiko ambayo si ya lazima.
 
Alisisitiza umuhimu wa kila mkuu wa idara kufuata sheria, taratibu za utumishi wa umma hasa pale ambapo watumishi wanapofanya makosa ili yasiweze kujirudia.
 
Akizungumzia majukumu ya viongozi hao, Meja Jenerali Kingu aliwataka wasisubiri kukumbushwa wajibu wao, kila kiongozi ayatambue majukumu aliyonayo na kuyatekeleza kwa ufanisi yakiwemo ya wastaafu, nidhamu, uhamisho kwa watumishi.
 
Aliwataka wakuu wa idara kushirikiana na watumishi ili kuwe na mpangilio mzuri wa kazi, kuongeza ufanisi na uwajibikaji.
“Naamini idara zote zilizopo chini ya Wizara hii zina watendaji wazuri wanaojua wajibu wao na wachapakazi hivyo tuwatumie, kuwepo na mpango mkakati wa kuondoa kero mbalimbali.
 
“Kero hizo ni pamoja na suala la kama mishahara, stahiki za watumishi na upadishaji vyeo…utakuta mtumishi kapanda cheo muda mrefu lakini anapata mshahara wa zamani usiolingana na nafasi mpya aliyonayo, kuwepo mabadiliko,” alisisitiza.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Emanuel Kayuni, alimshukuru Meja Jenerali Kingu kwa maagizo aliyotoa na kuahidi yatafanyiwa kazi.

No comments: