By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Baada ya Chadema kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amesema uamuzi huo unawanyima fursa wagombea wa chama hicho waliopitishwa, waliokata rufaa kupinga kuenguliwa.
Leo jioni Alhamisi Novemba 7, 2019 mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza uamuzi wa chama hicho mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha kamati kuu.
Katika maelezo yake, Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai amesema kuendelea kushiriki uchaguzi huo
utakaofanyika Novemba 24, 2019 ni kuhalalisha ubatili, akibainisha kuwa takribani asilimia 85 ya wagombea wao nchi nzima wameenguliwa.
Katika maelezo yake Jafo amesema, “ingawa ni haki yao lakini nimeshangazwa na uamuzi wao kwa sababu kila kitu kipo wazi. Kanuni haijamfunga mtu yeyote kudai haki ya kukataa rufaa.”
“Kweli kuna fomu zina makosa katika kujaza lakini mchakato wa rufaa unaendelea hadi leo kesho. Huenda leo baadhi ya uamuzi kwa wagombea waliokataa rufaa utatolewa lakini nashangaa kujitoa kwao.”
Amesema kujitoa kwa chama hicho si rekodi kwa madai kuwa wanawakosesha haki wagombea wao hasa wa vijijini waliokata rufaa.
“Ni vyema Chadema wangetafakari kwa undani kabla ya kufikia uamuzi huo,” amesema Jafo akivitaka vyama vingine vya upinzani kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment