ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 8, 2019

TIMU NANE ZATINGA HATUA YA NANE BORA ASAS SUPER LEAGUE 2019

 Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Iringa (IRFA) Cyprian Kuyava akisalimiana na moja ya timu ambayo imetinga hatua ya nane bora ligi ya ASAS SUPER LEAGUE mkoani Iringa
 Mkuu wa wilaya ya kilolo Asia Abdalah akiwa na viongozi wa chama cha soka mkoa wa Iringa wakisalimiana na wachezaji wa timu ya Young Stars ambayo nayo imetinga hatua ya nane bora
NA FREDY MGUNDA, IRINGA

TIMU za 8 zilizokuwa zikishiriki ligi soka daraja la tatu mkoa wa Iringa inayojulikana kwa jina la Asas Super league  2019 zimefanikiwa kuingia hatua ya nane bora katika kuelekea kumpata bingwa wa mkoa atakayeondoka na kitita cha milioni mbili.

Timu zilizofanikiwa kuingia hatua ya nane bora ni,Mafinga Academy Fc, Mkimbizi Fc, Young Stars, Ismani Fc, Irole Fc,Kalinga Fc, Kidamali Fc timu moja kati ya Nzihi na Mbegamwekundu atajihakikishia kuingia katika nane bora za ligi hiyo mkoani hapa.

Wakati timu hizo zikiingia katika nane bora timu za Acosato fc, African Wanderas hizo zimeshuka daraja hadi la nne wakati timu za Mapanda Fc, Mshindo fc na Magulilwa zikicheza mchezo wa mtoano kuendelea kubaki ligi hiyo ama kuungana na walioshuka daraja. 

Katika ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Maziwa ya Asas mchezaji, Emmanuel Geka wa Kidamali Fc anaendelea kuongoza kwa ufungaji wa magoli baada ya kufikisha magoli 8 huku akifatiwa kwa karibu na wachezaji, Riziki Kelvin (Ismani Fc) na Luka Duma (Irole Fc) wenye mabao 7 kila mmoja.

Wachezaji wanaofatia katika mashindano hayo ni Baraka Athuman (Mafinga Academy) mwenye magoli 5 huku wachezaji Kelvin Msafiri (Kalinga Fc), Conrodgers Mhavile (Irole fc) na Mohamed Rashid (Ismani fc) wakiwa na magoli manne.

Na katika mechi zilizopigwa juzi Upendo Fc ilitoshana nguvu na timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Iringa kwa goli 1 – 1 yaliyofungwa na Elisha Chuma (Chuo cha Iringa) na Jemin Fred kwa upande wa Upendo Fc.

Wakati michezo mingine ilikuwa kati ya Ismani fc dhidi ya Acosato ambapo Isman waliibuka na ushindi wa magoli 4 -1 kwa magoli yaliyofungwa na Mohamed Rashid, Riziki Kelvin na Razack Kibuga huku goli la kufutia machozi kwa upande wa Acosato likifungwa na Mohamed Salufu.

Mchezo mwingine ulikuwa kati ya  Kidamali Fc dhidi ya Irole fc ambapo Kidamali walishindwa kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani na kukubali kipigo cha mabao 3 -1 kwa magoli ya Luka Duma aliyefunga mawili, Conrodgers Mhavile .

Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Iringa, Cyprian Kuyava akizungumza na Tanzania Daima alivipongeza vilabu vyote vilivyofuzu hatua ya nane bora licha ya changamoto zilizojitokeza kutokana na ugumu wa mashindano hayo mwaka huu.

Kuyava alisema kwamba kuna baadhi ya timu zimecheza kwa nidhamu kubwa hali iliyosababisha kuweza kufuzu katika hatua hiyo kubwa kabisa na kuwapongeza waamuzi, makamishna na wasimamizi wa ligi kwa umakini na umahiri wanaoendelea kuonyesha katika ligi ya Asas.

Aidha alizipongeza timu zote zilizoshiriki ligi hiyo kwa nidhamu, ushindani weredi mkubwa wakati wote wa mashindano hayo yalipokuwa yakifanyika katika hatua za makundi na kuzitaka timu zilifuzu hatua ya nane bora kufanya maandalizi mazuri kuweza kuibuka na ubingwa.

Alisema kuwa changamoto zilizojitokeza katika hatua ya makundi zinatakiwa kufanyiwa kazi katika hatua ya nane bora ili kuweza kumpata bingwa mshindani katika ligi za mabingwa ya mikoa Tanzania Bara.

 Bingwa wa mashindano hayo atapata kombe na sh. 2,000,000,jezi seti moja,mipira mitatu, na nafasi ya kushiriki ligi ya mikoa.  Mshindi wa Pili shilingi 1,000,000, Mipira 2, Jezi Seti 1, Cheti cha Ushiriki huku Mshindi wa Tatu - Tsh 500,000/=, Jezi Seti 1

No comments: