ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 8, 2019

SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA WAZEE WALIOTUMIKA KATIKA UKOMBOZI WA NCHI NA UJENZI WA TAIFA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Mussa Sima amesema kuwa Serikali inatambua michango ya watu mbalimbali walioshiriki katika ukombozi na Nchi yetu na ujenzi wa Taifa ikiwa ni pamoja wazee wetu walioshiriki katika tukio la kuchanganya udongo tarehe 26 Aprili, 1964.

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis (Mb.) lililouliza Je, Serikali inawaangalia vipi wazee wetu wane walioshiriki katika kuchanganya udongo siku ya Muungano mwaka 1964, kwa kuwapa asante baada ya utu uzima kuwafikia.

Naibu Waziri aliongeza kuwa Kundi hili ni moja kati ya makundi mengi yaliyotoa mchango wa hali na mali katika kulijenga Taifa hili ikiwemo wastaafu na walioshiriki katika Vita vya Kagera. Hata hivyo, kwa sasa hakuna sheria mahsusi ya asante au malipo kwa watu waliofanya mambo makubwa yanayojenga historia ya Nchi.

“Kuwashirikisha Wazee hawa katika maadhimisho ya sherehe za Muungano ni sehemu ya kutambua mchango wao na kukumbuka tukio muhimu la uchanganyaji wa udongo wa Tanganyika na Zanzibar. Ushiriki wao huwezeshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Aidha, pamoja na wazee hawa, yapo makundi mengine ya wazee ambao kwa namna moja au nyingine walitoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa ambao pia hualikwa kushiriki katika maadhimisho hayo mfano Viongozi Wastaafu na Wanasiasa Wakongwe” alisema Waziri Sima.

Aidha Naibu Waziri Sima akijibu swali la Mh Jaku Hashim Ayoub (B.L.W) lililouliza Kwa mujibu taarifa rasmi ya Serikali Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iliyotolewa mwaka 2014, Kisiwa cha Latham (Fungu Mbaraka) ni mali ya Zanzibar tangu kilipotangazwa rasmi mwaka 1898. Hata hivyo zipo taarifa zilizothibitishwa kuwa Serikali ya Muungano kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliiandikia SMZ kuwataarifu kwamba Kisiwa hicho ni cha Tanzania Bara:-

Je, Serikali hizi mbili ambazo ni ndugu wa damu watakaa kutatua kero hii ya muda mrefu; na Je, Serikali haioni kuwa umefika muda muafaka kulifanyia kazi suala hilo.

Waziri Sima alisema kuwa Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya mabadiliko ya Katiba sura ya 83 Ibara ya 2 (1) inatamka wazi kuwa eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar pamoja na sehemu ya bahari ambayo imepakana na nchi za Kenya, Shelisheli, Comoro na Msumbiji. Hivyo basi, kwa mujibu wa tafsiri ya mipaka hiyo, Kisiwa cha Latham (Fungu Baraka) kiko ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na pia hakuna mgogoro wa umiliki wa eneo la kisiwa hicho kwa vile kimo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments: