Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Phaustine Kasike(kushoto) akikagua maandalizi ya awali ya shamba la mahindi alipofanya ziara ya kikazi leo Novemba 17, 2019 katika Kambi ya Magereza – Katesh iliyopo wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara. Kulia ni Mkuu wa Magereza Mkoani Manyara, ACP. Lipina Lyimo.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa pili toka kulia) akikagua moja ya trekta linalotumika kwa shughuli za Kilimo katika Kambi ya Magereza – Katesh iliyopo wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara, leo Novemba 17, 2019 alipotembelea Kambi hiyo.
Moja ya maghala ya kuhifadhia mazao mbalimbali yanayozalishwa katika Kambi ya Magereza – Katesh iliyopo wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akikagua mradi wa tofali za saruji ambazo zinafyatuliwa katika Gereza la Babati tayari kwa ujenzi wa nyumba za Maafisa na askari wa kituo hicho.(Picha zote na Jeshi la Magereza).
Na ASP. Lucas Mboje, Hanang;
KAMBI ya Magereza Katesh imepewa malengo mahususi ya kuzalisha mahindi ili kutosheleza mahitaji ya chakula cha wafungwa na mahabusu katika magereza yote ya Mkoa wa Manyara.
Hayo yamebainishwa leo na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike alipotembelea kambi hiyo kwa lengo la kujionea hatua mbalimbali za awali za maandalizi ya kilimo katika msimu 2019/2020.
Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa kambi ya Katesh ni moja ya eneo la kimkakati katika kutimiza lengo la uzalishaji wa chakula cha wafungwa na Mahabusu katika Mkoa wa Manyara.
“Kambi ya Magereza Katesh ni eneo ambalo lina fursa kubwa ya ardhi yenye rutuba na inayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na ya kibiashara hivyo lazima tuhakikishe kuwa tunafanikisha malengo tuliyopewa na Serikali kuhusu uzalishaji wa chakula cha wafungwa,” amesisitiza Jenerali Kasike.
Kwa upande wake Mkuu wa Kambi hiyo, Mkaguzi wa Magereza Nasoro Juma amesema kuwa katika msimu wa kilimo 2019/2020 tayari wameanza maandalizi ya awali na wanatarajia kulima ekari 150 za mahindi na ekari 50 za zao la arizeti ili kufanikisha lengo la mahitaji ya chakula cha wafungwa katika Magereza ya Mkoa wa manyara.
Kambi ya Magereza Katesh ilianzishwa rasmi mwaka 2009. Kambi hii ina ukubwa ekari 300 ambapo ekari 200 ndizo zinazofaa kwa shughuli za kilimo cha mahindi, Arizeti na mazao mengineyo ya kibiashara ikiwemo zao la dengu.
No comments:
Post a Comment