ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 18, 2019

Uhusiano ni kubebeana udhaifu, usichoke kirahisi

ULIMWENGU wa uhusiano wa kimapenzi kwa sasa una sarakasi nyingi. Unaweza kumuona mtu fulani yupo ‘smart’, ukadhani ni bora kuliko uliyenaye, kumbe wapi bwana, ana majanga yake, afadhali hata huyo uliyenaye sasa. Kila mmoja ana kasumba yake. Huyu atakuwa mkali, huyu ni mpole, lakini ana ukorofi wake mwingine ambao ukiujua, unaweza ukasema afadhali ya yule mkali. Kuna mwingine unaweza kukuta ni mnywaji wa pombe na anavuta sigara, lakini ni mstaarabu kuliko hata yule asiyekunywa pombe wala kuvuta sigara.

Ndiyo maana sasa hivi mwanaume ukikutana na mwanaume mwenzako akakuelezea anayoyapitia kwenye uhusiano wake, unaweza kujiona wewe ambaye ulikuwa unaamini unapitia magumu kumbe si lolote, si chochote. Kuna wengine ni hodari wa kuzungumza. Unakuta mwanaume ni muongeaji kwelikweli, kila kitu anakijua yeye na hakubali kushindwa. Kuna wanawake wana gubu kwelikweli, kila kitu kwake yeye ni tatizo.

Nyumbani hataki kuona wageni zaidi yako. Wakati mwingine hata wewe mpenzi wake hataki kukuona zaidi ya kuwa yeye mwenyewe. Ukifika atakukorofisha tu ilimradi, mara atakuambia hiki mara kile, mwisho wa siku mnagombana. Kuna mwingine yeye suala la usafi limempitia kushoto, akiwa na wewe yeye mambo yake ni shaghalabaghala. Unajitahidi kuweka vitu kwenye mpangilio mzuri, lakini yeye akija hajali. Anatupatupa tu vitu hovyohovyo, unakereka kwelikweli.

Unaweza kukuta hata usafi wa mwili kwa maana ya kuoga au kupiga mswaki, kwake ni tatizo. Huyo ndiye mpenzi wako ambaye itafika mahali itabidi mlale wote chumba kimoja, mpeane haki ya tendo la ndoa na mambo mengine kadha wa kadha.

Kumbe basi ni vyema kujifunza kwamba, kwenye uhusiano, suala la kubebeana udhaifu ni la msingi sana. Mmekutana ukubwani, kila mmoja amelelewa kwenye mazingira tofauti, hivyo si rahisi unavyoishi wewe, basi na mwenzako ataishi hivyo. Siyo rahisi kile ambacho wewe unaona hakikupendezi, basi na mwenzako hakitampendeza, la hasha. Wewe unaweza kuwa unachukizwa na jambo fulani, mathalan kulala bila kuoga, lakini mwenzako hilo siyo ishu kabisa.

Anaporudi jioni, analala vizuri tu na usingizi unamchukua kabisa hata kama hajaoga. Kuoga jioni au usiku siyo lazima kwake, ataoga asubuhi akiwa anajiandaa kwenda kwenye mihangaiko yake. Watu wa namna hiyo wapo wengi tu. Au mathalan kuna baadhi ya watu huwa wanapenda kuona matatizo ya kwao tu. Matatizo ya wenzao hayawagusi. Huu ni ubinafsi, kwenye uhusiano unaweza kusababisha wapendanao wakashindwa kuelewana.

Hivyo basi, unatakiwa kuhakikisha kwamba ili uweze kuishi vizuri na mpenzi wako, ujifunze kubeba udhaifu wake. Amini kwamba ni tabia, kuibadilisha ni vigumu, lakini taratibu anaweza kubadilika kutokana na wewe.

Wewe ndiye uwe kioo katika lile ambalo mwenzako analifanya. Wakati mwingine yawezekana usitumie nguvu kubwa sana katika kumuelekeza, lakini matendo yako tu yanaweza kumfanya abadilike. Mpe nafasi ya kujifunza kupitia wewe. Wewe uwe mwalimu wake. Si tu kwamba wewe ni mwalimu, pia kwake unaweza kuwa mwanafunzi katika baadhi ya mambo kwani hata wewe inawezekana kuna udhaifu wako. Kubali kujifunza pia. Mtafika mahali kwa pamoja mtafanana kwa mambo mengi.

Epuka sana kumsemasema kutokana na udhaifu wake, tumia hekima katika kumsema. Mwelekeze kwa vitendo zaidi, lakini pale inapolazimika kuzungumza naye, tumia lugha rafiki ya kimapenzi kumkosoa na bila shaka ataelewa. GPL

Instagram & Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

No comments: