Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mhe. Hemedi Suleiman Abdalla alipowasili Uwanja wa Ndege wa Chakechake kisiwani Pemba leo tarehe 06 Januari 2020 kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi Kituo cha Ubunifu wa Kisayansi kwa niaba ya Vituo 22 vya Unguja na Pemba katika Kijiji cha Pujini Wilaya Chake chake Mkoa wa kusini Pemba ikiwa ni moja ya Shamrashamra za kuelekea kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayotegemewa kuadhimishwa tarehe 12 January 2020 katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo ya Ujenzi cha Kituo cha Ubunifu wa Kisayansi kwa niaba ya Vituo 22 vya Unguja na Pemba katika Kijiji cha Pujini Wilaya Chake chake Mkoa wa kusini Pemba baada ya kuweka Jiwe la msingi ujenzi wa Vituo hivyo leo tarehe 06 Januari 2020 ikiwa ni moja ya Shamrashamra za kuelekea kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayotegemewa kuadhimishwa tarehe 12 January 2020 katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.Kulia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Simai Mohammed Said.
Viongozi na Wananchi wa Pujini kisiwani Pemba wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassa wakati alipokuwa akihutubia Wananchi wa Pujini Wilaya ya Chakechake Kisiwani Pemba baada ya kuweka Jiwe la Msingi Kituo cha Ubunifu wa Kisayansi kwa niaba ya Vituo 22 vya Unguja na Pemba leo tarehe 06 Januari 2020 ikiwa ni moja ya Shamrashamra za kuelekea kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayotegemewa kuadhimishwa tarehe 12 January 2020 katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Viongozi na Wananchi wa Pujini katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Pujini Wilaya ya Chakechake Kisiwani Pembalepo Januari 06,2020 baada ya kuweka Jiwe la Msingi Kituo cha Ubunifu wa Kisayansi kwa niaba ya Vituo 22 vya Unguja na Pemba ikiwa ni moja ya Shamrashamra za kuelekea kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanayotegemewa kuadhimishwa tarehe 12 January 2020 katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN,
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA JENGO LA KITUO CHA UBUNIFU WA KISAYANSI PUJINI PEMBA TAREHE 6 JANUARI, 2020 KUELEKEA MADHIMISHO YA SHEREHE ZA
MIAKA 56 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
Mhe. Riziki Juma Pembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
Mhe. Simai Mohamed Said, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali;
Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba;
Mwakilishi wa Benki ya Dunia;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mliopo;
Dkt. Idris Muslihi Hija, Katibu Mkuu - Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali;
Ndugu Viongozi wa Taasisi mbalimbali mliohudhuria;
Wazee wetu, walimu na wanafunzi mliopo;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana
Assalam Alaikum!
Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutuwezesha kukutana leo katika tukio hili kubwa na muhimu kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Pili, ninayo furaha kubwa na shukrani kwa heshima mliyonipa kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hili la kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kituo cha Ubunifu wa Kisayansi hapa Pujini. Nimejulishwa kuwa jiwe hili la msingi nimeliweka kwa niaba ya vituo vingine ishirini na mbili (22) vitakavyojengwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Naushukuru Uongozi wa Wizara pamoja na kamati nzima iliyoshiriki kutayarisha na kufanikisha shughuli hii muhimu ikiwa ni shamra shamra za kuadhimisha miaka 56 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964. Matayarisho haya ni ishara ya wazi ya kuyathamini Mapinduzi yetu matukufu na matunda yake.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza Wananchi wa hapa Pujini na maeneo yote ambako vituo vya aina hii vitajengwa, kwa kupata bahati ya kusogezewa maendeleo haya ya kukuza vipaji vya wanafunzi katika fani za sayansi. Aidha, niwapongeze pia wananchi wote mliojitokeza kwa wingi kushuhudia shughuli hii. Huu ni uthibitisho kwamba Mapinduzi ya Zanzibar siyo tu yametupa uhuru wa kweli na heshima, bali pia yametukomboa kifikra na kukuza uzalendo wetu kwa nchi yetu.
Pongezi maalum kwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa jitihada kubwa inayofanywa na Serikali yake katika Maendeleo ya Elimu Nchini. Katika kipindi chake bajeti ya Maendeleo ya Elimu imeongezeka kutoka asilimia 21 mwaka 2013/14 hadi kufukia asilima 61 mwaka 2017/2018. Bajeti ya elimu kwa ujumla nayo imeongezeka zaidi ya mara sita kutoka mwaka 2013/2014. Hii ni hatua kubwa kwenye sekta ya elimu. Vile vile, sitokuwa nafanya uadilifu kama sikumpongeza Mheshimiwa Riziki Pembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali na ngazi zote za uongozi wa Wizara kwa kuhakikisha kwamba wanatekeleza vyema Sera na Mpango wa Maendeleo ya Elimu, na matokeo yake ni haya tunayoyaona.
Ndugu Wananchi;
Serikali zetu zote mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinajitahidi kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu bora na katika mazingira mazuri ya kujifunzia kuanzia ngazi ya elimu ya Maandalizi mpaka Sekondari. Ujenzi wa majengo haya ni ushahidi kwamba serikali imejiandaa vya kutosha kuweka miundombinu bora ya elimu itakayomwezesha mtoto kupata elimu bora ya sayansi na yenye stadi sahihi. Naamini kwamba pindi majengo haya yatakapokamilika na kuanza kutumika ufaulu wa watoto wetu kwenye masomo ya Sayansi na Hisabati utaongezeka sana.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu ya skuli zetu ili kuongeza nafasi zaidi za masomo na hivyo, kuwawezesha watoto wote kupata haki yao ya msingi ya elimu. Huu ni mkakati wa Serikali katika kuendeleza malengo ya Mapinduzi yetu ya mwaka 1964 ya kuwapatia elimu bila ya malipo wananchi wote wa visiwa vya Unguja na Pemba bila kujali itikadi zao, dini, siasa rangi na nyinginezo. Mambo haya yote yanayofanywa ni kuziendeleza na kuzifanya ziishi fikra na maoni ya muasisi wa Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi, Amin.
“Mzee Abeid Amani Karume, ameuwawa na amezikwa. Lakini kilichokufa na kuzikwa ni kiwiliwili chake tu, fikra, Ahadi na Malengo ya Mapinduzi zitaendele kudumu milele.”
Ndugu Wananchi;
Sote ni mashahidi wa jitihada kubwa zinazofanya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Awamu zote, na sasa chini ya Mheshimiwa. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika kuendeleza fikra za muasisi wa Taifa hili za kufuta ujinga. Mheshimiwa Dkt. Shein amefuta ada na michango yote katika elimu ya lazima. Jambo hili ni kuendeleza kwa vitendo lengo moja kuu la Mapinduzi ya Zanzibar la kufuta ujinga, kuwapa uwezo wa utambuzi wa kwa kutenda wananchi wa Zanzibar, kwa ajili ya maendeleo yao.
Jukumu letu wananchi ni kuendelea kulinda na kuthamini matunda haya ya Mapinduzi ili tuendane na karne hii ya sayansi na teknolojia bila kuharibu mila, tamaduni na silka zetu. Naomba nisisitize sana jambo hili kwa vijana na watoto wetu ambao mara nyingi wanatumika kubeba agenda ambazo wala hawazijui. Inasikitisha kuona vijana na watoto wetu wanashawishiwa na watu wasiopenda maendeleo kubeza jitihada zinazofanywa na Serikali yao.Sote tushirikiane katika kuwaelimisha vijana na watoto wetu kuhusu mwelekeo wa nchi yao, kwani kwa kufanya hivyo watafahamu na kushiriki katika jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo. Rai yangu kwa vijana, kataeni kwa nguvu zenu zote kucheza ngoma msiyojua malengo yake. Ongezeni jitihada katika masomo yenu kwa manufaa yenu, familia zenu na Taifa letu kwa jumla. (Akili za kushikiwa)
Ndugu Wananchi;
Kituo hiki nilichokiweka jiwe la msingi kitatumiwa na wanafunzi pamoja na walimu wao. Niwaombe kukitumia kituo hiki kwa malengo yaliyokusudiwa ili tupate matokeo tunayotarajia. Aidha, yapo mambo machache yakusisitiza kwenu ili kuleta ufanisi katika kituo chetu hiki.
1. Upo msemo wa wahenga usemao “Kitunze Kidumu”. Niwaase kutunza majengo na miundombinu yote ya vituo hivi kama mchango wenu katika kuthamini jitihada kubwa za Viongozi wetu wa Serikali ya Mapinduzi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Washirika wetu wa Maendeleo (World Bank);
2. Kuwe na ushirikiano wa dhati kati ya walimu na wanafunzi katika kupeana taarifa mbalimbali na kurekebisha kwa haraka pindi itokeapo hitilafu ya aina yoyote katika kituo chetu;
3. Uongozi uandae kanuni na miongozo kwa watumiaji (user’s manual or guidelines) ili kuwasaidia watumiaji wa kituo hichi na kukifanya sehemu sahihi ya kuzalisha wataalamu wenye nidhamu na kuthamini vya kwao;
4. Vituo hiki ni mali ya umma, Andaeni utaratibu wa matengenezo ya kila mwaka yaani “Periodic Maintenance” ya kituo kwa kujumuisha majengo pamoja na vifaa vyake vya Kisayansi ili kuimarisha na kudumisha ubora wa vituo hivi; na
5. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ifuatile kwa karibu sana suala la vifaa vya tahadhari ili madhara yoyote yasitokee katika vituo hivi muhimu vya Sayansi. Wizara tuwe waangalizi wazuri wa vituo hivi.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu naomba kwa mara nyingine nichukukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali kwa jinsi anavyosimamia na kushirikiana na Watendaji na Viongozi wenzake kuona Elimu ya Zanzibar inakuwa bora kama kauli mbiu ya Wizara inavyosema 'Elimu Bora Kwanza. Hatuna budi kuendelea kumuunga mkono kwa kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapata elimu inayolenga kukuza uchumi ili hatimaye kufikia uchumi wa kati na baadae uchumi mkubwa. Tusisahau kwamba hizi ni nguvu za wengi, watoto wanapata taaluma itakayowasaidia katika maisha yao, lakini pia elimu huwaelekeza vijana wetu kutunza mila na desturi zetu kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa utamaduni wetu. Wito kwa vijana wetu na jamii kwa ujumla ni kujiepushe na mazonge ya kidunia ikiwemo madawa ya kulevya, rushwa, maambukizi ya ukimwi na thakala kubwa iliyotukabili ya udhalilishaji.
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Mwisho kabisa, naomba kuwapongeza na kuwashukuru wote walioshiriki katika kuhakikisha kuwa shughuli yetu hii inafana kwa kiwango kikubwa. Pongezi pia kwa Kamati ya maandalizi iliyonialika kuwa Mgeni Rasmi, ni heshima kubwa kwangu binafsi lakini pia kwa Taifa kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huu mkubwa na wa mfano hapa Zanzibar, kwenu nyote nasema asanteni sana. Ombi langu kwa wananchi wote ni kuendelea kujitahidi kila siku kuwa wazalendo na kuchapa kazi kwa weledi, uadilifu na nidhamu ya hali ya juu kwa ajili ya manufaa ya Taifa letu.
Mungu yabariki Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
Mungu Ibari Tanzania
Mapinduziiii …. Mapinduziiii… Mapinduziii
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment