ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 29, 2020

TFF ikinyoosha mkono Mkude, Morrison kuikosa mechi Yanga, Simba

Mwanaspoti, TFF, Mkude, Morrison, kuikosa, Yanga, Simba, Tanzania, Mwanasport, Michezo
By OLIPA ASSA, Mwanaspoti

KAMA vielelezo vikiwekwa mezani kuna mshtuko mkubwa unaoweza kuwakumba mashabiki wa Yanga na Simba wiki ijayo.

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) inakutana mapema wiki ijayo na moja ya ajenda kuu itakayojadiliwa ni kuhusu wachezaji wawili, Jonas Mkude wa Simba na Bernard Morrison wa Yanga.

Nyota hao wanadaiwa kufanya makosa ya utovu wa nidhamu kwenye moja ya mechi zao wa Ligi Kuu Bara ambapo Mkude alimpiga kiwiko mchezaji wa Biashara United, Ally Kombo wakati Morrison alifanya kosa kama hilo kwa Jeremiah Juma wa Prisons. Uzoefu unaonyesha ni watuhumiwa wachache sana waliopona ndani ya kamati hiyo ambapo walikumbana na faini nzito.
Morrison ndiye alianza kupelekwa kwenye kamati hiyo baada ya Kamati ya Saa 72 na kubaini kwamba kosa lake linapaswa kupelekwa kwenye kamati hiyo.

Kwa upande wa Morrison ni zaidi ya wiki tangu apelekwe kwenye kamati hiyo wakati Mkude bado ishu yake ni ya moto ingawa kuna sintofahamu kuhusu siku ya kamati hiyo kukutana.
Ingawa kuna ugumu wa kufahamu ni siku gani kamati hiyo itakutana, chanzo kutoka ndani ya shirikisho hilo kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa wiki ijayo watakutana kuwajadili nyota hao.
Endapo kamati hiyo itakutana mapema wiki ijayo na kama nyota hao watakutwa na hatia basi watakosa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya 38 ya VPL kifungu cha 5.2 ambacho kinaeleza kwamba Mchezaji akibainika kupigana/kupiga kabla/ wakati wa mchezo au mara tu baada ya mchezo kumalizika atafungiwa michezo isiyopungua mitatu na faini ya Sh 500,000.

Kwa maana hiyo, Mkude na Morrison wakibainika na makosa hayo basi watakosa mechi tatu ikiwemo ile ya Watani wa Jadi Simba na Yanga.

Morrison amekuwa mhimili mkubwa ndani ya Yanga kwani tangu asajiliwe amecheza mechi zote kwenye kikosi cha kwanza kutokana na umuhimu wake katika kuasisti na kufunga jambo ambalo kama atakutwa na hatia itakuwa ni pasua kichwa kwa mashabiki wa Yanga na benchi la ufundi.
Simba kupitia kwamba Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa imeonekana kutoshtuka sana na kinachoendelea huku wakisisitiza wanategemea TFF itende haki.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabu alisema Yanga ndiyo itakuwa na pengo kubwa kutokana na aina ya uchezaji wa Morrison ukilinganisha na Mkude ambaye kuna wachezaji wa kuchukua nafasi yake.

“Simba pana unafuu kwa sababu kuna wachezaji wengi wa kucheza nafasi ya Mkude, ila Yanga Morrison ni Morrison tu pengo lake haliwezi kuzibwa na Mrisho Ngassa wala Deus Kaseke na mechi kama hiyo wapenzi tunahitaji kuona vikosi hivyo vikiwa vimekamilika, ”alisema.

Naye mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema; “Morrison ana majukumu mengi uwanjani, analazimisha mashambulizi muda wote anakuwa analeta presha kwa wapinzani ila kwa Simba hawana hasara kubwa mfano kocha akichezesha mfumo wa 4-3-3 Gerson Fraga anaweza akamudu nafasi ya Mkude, hivyo kwao sio hasara kubwa kama kwa Yanga,” alisema Mayay.

No comments: