ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 14, 2020

Mwamnyeto rasmi Yanga mchakato umemalizika hivi

By Mwandishi wetu
KWA dili lilivyo, Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba imebaki kutangazwa tu Bakari Nondo Mwamnyeto kuwa mchezaji mpya wa Yanga, baada ya wadhamini wa klabu hiyo GSM kumaliza shoo yote.

Awali, Simba walikuwa wamepania kumaliza ishu ya beki huyo, lakini vigogo wa Coastal Union wakaja na masharti magumu huku wakala wa mchezaji akidai thamani yake si chini ya Sh100milioni.

Kigogo aliyesimamia shoo hiyo ya Mwamnyeto, imebainika kuwa ni Mhandisi Hersi Said wa GSM kwa niaba ya Yanga ya Mwenyekiti Msomi, Dk Mshindo Msolla.

Inaelezwa kuwa Dk Msola anaiva sana na Mwamnyeto na alishampa maneno matamu muda mrefu ila ishu ikawa kimya

Mwanaspoti linafahamu kwamba Hersi alitinga barakoa yake na kuwasha gari mpaka Tanga kuweka ishu sawa na klabu ya mchezaji huyo kimya kimya huku Simba wakiwa wametulia zao ndani wakisubiri corona imalizike ingawa tayari walishapeleka ofa yao kwa njia ya mazungumzo ya simu na ikakataliwa kwa madai kuwa ni ndogo.

“Ninachofahamu ni kuwa msimu ujao GSM watatudhamini Coastal Union ikiwa ni moja ya makubaliano ya dili hili la Mwamnyeto na kila kitu kiko wazi,” alisema mmoja wa mabosi wa klabu hiyo mwenye ushawishi mkubwa.

Habari zinasema Coastal Union watapata udhamini wa Sh70milioni kila mwaka kutoka GSM ambayo ni makubaliano tofauti na mchezaji, ambaye sasa wameshapewa ruksa na wanamalizana naye juu kwa juu kuhusu maslahi binafsi.

Mwamnyeto amebakiza takribani miezi 13 katika mkataba wake na Coastal.

Jana, Mwanaspoti lilimsaka Mwamnyeto katika kupata uhakika huo ambapo, licha ya kukwepakwepa alithibitisha kwamba yuko katika hatua za mwisho msimu ujao kuvaa jezi za Yanga.

“Tunaendelea vizuri na kila kitu kipo sawa, najua uongozi wa Coastal Union ulishamaliza upande wao na Yanga na sasa bado huku kwetu kidogo tu tutamaliza,” alithibitisha beki huyo ambaye ni beki wa Taifa Stars.

Ingawa gharama kamili ya usajili huo haijawekwa wazi taarifa kutoka ndani ya familia ya beki huyo ni kwamba, Mwamnyeto ataitumikia Yanga kwa miaka mitatu kuanzia msimu ujao huku gharama kubwa zikitumika kuanzia usajili mpaka mshahara wake.

Kitendo cha Yanga kumchukua Mwamnyeto ni kama kombora la kwanza walilorirusha kwa Bilionea wa Simba, Mohamed Dewji ‘MO’ ambaye bodi yake ndio ilitangulia kumhitaji beki huyo lakini wakachelewa kisa gharama ni kubwa.

Hata hivyo, kutokamilika kwa dili hilo Coastal Union wametaja kuwa ni utata wa meneja wa Mwamnyeto, Kassa Mussa ambaye kwa sasa yupo nchini Italia.

Inadaiwa kuwa kupanda bei ya beki huyo kumetokana na msimamo wa Mussa, ambaye amekuwa akibadilika kila kukicha huku Mwamnyeto mwenyewe kitambo alishakubali kila kitu.

Habari zinasema kwamba Mussa anataka Mwamnyeto aende kucheza soka la kulipwa Ulaya.

No comments: