Amesema ili kufikia lengo la upandaji miti milioni 10.5 kwa mwaka katika ngazi ya mkoa ataunda timu maalumu ya kukusanya miche ya miti na kuomba wadau kuwasaidia kwenye kampeni hiyo kwa lengo la kuifanya Arusha iwe ya kijani.
Mkuu huyo ametoa agizo hilo Jumamosi Aprili 9, 2022 katika shule ya msingi ya Serikali ya mchepuo wa kiingereza ya Enaboishu Academy iliyopo wilayani hapa katika kilele cha upandaji miti mkoa wa Arusha.
Amesema katika maadhimisho hayo fedha zimekuwa zikiombwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ila hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa,hivyo kuanzia maadhimisho ya mwakani hawapaswi kuomba fedha.
“Tuna wadau wengi kweli hapa, hii miti inawezekana hata wakurugenzi tusitumie fedha zetu, tatizo letu moja tukienda kwa hawa tunaomba hela hapana tuombe miti. Hebu tuache utaratibu wa kuomba hela tuombe miti,huu mchezo wa watu kupewa hela hizi fedha haziendi kwenye miti,”amesema
“Mwaka huu nimeona watu wanaomba fedha kuhusu haya maadhimisho, mwaka kesho hakuna mtu kutoa fedha kwenye siku ya mazingira mimi nimepiga marufuku,”
Mongella amesema ataanzisha timu maalumu ya kukusanya miche ya miti hasa ya matunda ambayo itapandwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule na kuomba wadau wanaotaka kusaidia kampeni hiyo wamuunge mkono kwa kupeleka miti siyo fedha.
“Haya mapambo tungenunulia miti, tungenunua miti mingapi?
“Kwenye mkoa huu mdau ikitokea sijui Mkurugenzi wa halmashauri anakuomba hela sijui mkoani usitoe, sema Mkuu wa Mkoa alikataza hadharani,”
Mkuu huyo aliagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani Arusha kuhakikisha wanapanda miti milioni 1.5 kila mwaka ili kufikia lengo la upandaji miti milioni 10.5 kwa mkoa mzima.
Awali akitoa taarifa ya mkoa, Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Arusha, Julius Achiula amesema katika msimu wa mwaka 2020/2021 idadi ya miti iliyopandwa katika mkoa huo ni miti zaidi ya milioni mbili huku iliyostawi ikiwa miti milioni 1.6 sawa na asilimia 78.
Amesema wanaendelea kusimamia kampeni ya upandaji na utunzaji miti inayoelekeza kila halmashauri ya wilaya kupanda miti milioni 1.5 na kuwa halmashauri zimekuwa zikitekeleza agizo hilo ingawa hazijaweza kufikia malengo tangu kutolewa kwa agizo hilo mwaka 2009.
Naye Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini, Lewis Nzali aliwaomba wadau wa mazingira kushirikiana katika kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ikiwamo kutokukata miti.

No comments:
Post a Comment